“BAIKOKO NA VIBANDA VYA VIDEO VYASABABISHA ONGEZEKO LA MIMBA KWA WANAFUNZI MKOANI TANGA”

March 15, 2017
NGOMA za usiku mkoani Tanga maarufu kama Baikoko na Vibanda vya Video ambavyo vimekuwa vikionyesha mipira vimesababisha ongezeko la takwimu za mimba na kufikia wanafunzi 261 kwa kipindi cha Januari 2015 hadi Octoba mwaka 2016.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Afisa Elimu Taaluma Mkoani Tanga, Wiliamu Mapunda wakati akiwasilisha taarifa ya elimu kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Tanga (RCC).

Alisema suala hilo limesababisha ongezeko hilo ambalo ni hatari kwa ukuaji wa sekta ya elimu iwapo halitafanyiwa kazi kwa kukabiliana nalo ili liweza kutoweka kwenye jamii.

Aidha alisema katika takwimu hizo wanafunzi 55 wa shule za Msingi na 206 wa shule za Sekondari mkoani hapa hali iliyopelekea baadhi yao kukatisha ndoto zao za kuwa na elimu inayoweza kuwasaidia kukabiliana maisha.

“Mh Mkuu wa Mkoa tatizo la Mimba za utotoni limekuwa kubwa kwani kwa asilimia kubwa limechangiwa na ngoma za usiku maarufu kama Baikoko na vibanda vya kuonyeshea video kama vile mipira na kadhalika lakini tumejipanga kukabiliana nalo liweza kupata mafanikio makubwa “Alisema Afisa Elimu Taaluma huyo.

Kufuatia hali hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Martine Shigella aliwaagiza
wakuu wa wilaya kuhakikisha wanasimamia tatizo la kuwepo kwa mimba kwenye shule za msingi na sekondari kwa  kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wanafunzi wanaobainika na ujauzito ili wawataje wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali sambamba na kufikishwa Mahakamani.

Mkuu huyo wa mkoa alisema hawaweze kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kwenye sekta hiyo iwapo suala hili halitapatiwa ufumbuzi hivyo umuhimu wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kulizibiti.

“Tatizo la Mimba limekuwa kubwa sana naagiza hatua vichukuliwe kwa
wahusika na vikao vijavyo tuone ni wangapi wamekwish kufikishwa
kwenyevyombo vya kisheria nah ii ndio itakuwa mwarobaini wa tatizo
hilo “Alisema RC Shigella.

Alisema haingii akilini kuona idadi kubwa kama hiyo na kuendelea kukaa kimya na kuifumbia macho kwani bila kuwepo kwa hatua za makusudi kukabiliana na suala hilo linaweza kuathiri ukuaji wa kiwango cha taaluma hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia Makini Mkoani Tanga (Makini) Asseli Shewally alitaka kuwepo kwa ushirikiana baina ya wazazi, walimu na viongozi ili kuweza kumaliza tatizo la mimba hizo za utotoni ambazo zimekuwa tishio kubwa kwa ustawi wa mkoa.

Shewally alitaka kuwepo kwa mikakati ambayo itasaidia kukomesha
vitendo vya namna hiyo kwa kushtakiwa watu watakaobainika kujihusisha kimapenzi na wanafunzi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »