Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limemwondoa Mwamuzi Hussein Athuman
kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) baada ya kupata
alama za chini ambazo hazimwezeshi kuendelea tena kuchezesha Ligi hiyo.
Mwamuzi Hussein Athuman kutoka Mkoa wa Katavi alichezesha mchezo
namba 150 uliozikutanisha timu za Majimaji ya Songea na Young Africans
ya Dar es Salaam, kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.
Kadhalika Young Africans imepigwa faini ya jumla ya Sh. 1,000,000
(milioni moja) kutokana na timu yao kutoingia vyumbani, na pia kutumia
mlango usio rasmi wakati wa kuingia uwanjani, kitendo ambacho ni kinyume
na Kanuni ya 14 (13) na (14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imetolewa kwa
kuzingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.
Mwamuzi Ngole Mwangole: Mwamuzi huyo wa kati, Ngole Mwangole wa Mbeya
amepewa barua ya onyo kali na kumtaka aongeze umakini wakati
akichezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kubainika kukataa bao
lililoonekana kutokuwa na mushkeli la Mtibwa Sugar dhidi ya JKT Ruvu
katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Licha ya kujitetea, lakini kamati haikuridhika na maelezo yake. Hata
hivyo, kwa kuzingatia kuwa Bw. Mwangole alikuwa Mwamuzi Bora wa msimu
uliopita (2015/2016) na hiyo ndiyo mara yake ya kwanza kuonekana kufanya
uamuzi uliokosa umakini wakati akichezesha, TFF imeamua kumpa onyo.
Mechi namba 141 (Mwadui FC vs Kagera Sugar). Beki wa Kagera Sugar,
Godfrey Taita anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi
baada ya mechi na kuwatolea lugha chafu na vitisho kabla ya benchi la
ufundi la timu yake pamoja na askari polisi kuingilia kati na kudhibiti
kadhia hiyo.
Mechi namba 151 (Mtibwa Sugar vs Simba). Baada ya mchezo kumalizika
mashabiki waliingia uwanjani kwa wingi na kusababisha usumbufu mkubwa
kwa wachezaji, waamuzi na waandishi wa habari. Pia kamera ya Azam Tv
upande wa goli la Kusini iliangushwa na washabiki hao.
Vilevile sehemu ya kuchezea (pitch) ya Uwanja wa Jamhuri iko katika
hali mbaya ambapo inahitaji marekebisho makubwa ili iweze kuendelea
kutumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.
TFF imebaini kuwa kitendo cha washabiki kuingia uwanjani baada ya
filimbi ya mwisho, licha ya kuwa ni kinyume cha kanuni lakini pia
kilichangiwa na askari polisi kutokuwa makini katika majukumu yao ya
kusimamia usalama uwanjani na badala yake kuelekeza umakini katika
kutazama mechi.
Hivyo, Uwanja umesimamishwa kutumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu
ya Vodacom ili kutoa fursa kwa wamiliki kufanya marekebisho makubwa
kwenye eneo la kuchezea (pitch), na pia askari polisi kupata maelekezo
ya kutosha ya jinsi ya kusimamia usalama uwanjani badala ya kutazama
mechi. Kama marekebisho hayatafanyika, uwanja huo hautatumika kwa ajili
ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.
LIGI DARAJA LA KWANZA
Mechi namba 34 (Pamba vs Friends Rangers). Kamishna wa mechi hiyo
Mnenge Suluja amepewa Onyo Kali kwa kutoripoti kitendo cha timu ya Pamba
kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na
wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni
ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 35 (Kiluvya United vs Lipuli). Timu ya Lipuli imepewa
Onyo Kali kwa kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match
meeting) ikiwa na wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni
kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Pia mshabiki wa Kiluvya United, Bw. Athuman Mzongela anapelekwa
Kamati ya Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi na kutaka kuwapiga wakati wa
mapumziko. Hata baada ya mchezo aliendelea kuwatolea lugha chafu waamuzi
na Msimamizi wa Kituo.
Mechi namba 36 (African Sports vs Ashanti United). Daktari wa Ashanti
United, Andrea Mbuguni amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh.
200,000 kwa kuondolewa kwenye benchi baada ya kumtolea lugha chafu
Mwamuzi Msaidizi namba moja.
Mechi namba 38 (Lipuli vs Mshikamano FC). Kocha wa Mshikamano FC,
Hamisi Kinonda amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000
baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kupinga muda wa nyongeza wa dakika
tano, na kumtolea lugha ya matusi Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo ni kwa
mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Wachezaji wa Mshikamano FC, John Mbise jezi namba 9, Abdallah
Makuburi (5), Ally Mangosongo (12) na kipa Steven Peter (1) wanapelekwa
Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumshambulia Mwamuzi Bryson A. Msuya.
Lakini pia Mwamuzi Bryson A. Msuya amefungiwa mwaka mmoja kwa
kutozingatia sheria ipasavyo wakati akitoa penalti dhidi ya timu ya
Mshikamano FC, na ripoti yake kufanana na ile ya Kamishna.
Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Makongo Katuma amefutwa katika orodha ya
waamuzi wanaotambuliwa na TFF kwa kuwapiga vichwa wachezaji wawili wa
Mshikamano FC wakati Mwamuzi wa Kati alipokuwa akishambuliwa na
wachezaji wa timu hiyo wakati wakipinga adhabu ya penalti dhidi yao.
Adhabu hizo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 38(1) na 38(1c) na (1e) za
Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi. Mwamuzi Katuma pia
alipata alama za chini ambazo zisingemruhusu kuendelea kuchezesha Ligi
Daraja la Kwanza.
Naye Mwamuzi wa Akiba, Hashim Mgimba ameondolewa kwenye ratiba kwa
kuonyesha muda wa nyongeza (added time) tofauti na ule alioelekezwa na
Mwamuzi. Adhabu dhidi ya Mgimba imezingatia Kanuni ya 38(1d) ya Ligi
Daraja la Kwanza.
Kamishna wa mechi hiyo Fidelis Ndenga wa Njombe ameondolewa kwenye
ratiba ya makamishna kwa taarifa yake kufanana na ile ya Mwamuzi. Adhabu
hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39(1) ya Ligi Daraja la Kwanza
kuhusu Udhibiti wa Makamishna.
Pia Kamati imetoa mwito kwa vyombo vya usalama (askari polisi)
kutumia nguvu za wastani katika kutuliza ghasia viwanjani, hasa pale
wanapotaka kushughulikia eneo linalohusu wachezaji.
Uwanja wa Kichangani umeondolewa kutumika kwa mechi za Ligi, hivyo
klabu za Iringa sasa timu zao zitatumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora
mjini humo kwa mechi zao la Ligi. Uwanja huo ulikuwa kwenye matengenezo
ambayo tayari yamekamilika.
Mechi namba 39 (Polisi Dar vs Pamba FC). Klabu ya Pamba imepewa Onyo
Kali kwa kutofika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match
meeting). Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la
Kwanza.
Mechi namba 33 (KMC vs JKT Mlale). Kocha wa JKT Mlale, Edgar Msabila
amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya
kuondolewa kwenye benchi la ufundi (orderd off) kwa kutoa lugha chafu.
Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 38 (Kimondo FC vs Njombe Mji). Kocha wa Njombe Mji, Abdul
Banyai amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa
kumtolea Mwamuzi lugha ya matusi, na kulazimisha wachezaji wake
wajiangushe ili kupoteza muda.
Mechi namba 40 (Coastal Union vs Kurugenzi). Wachezaji wawili wa
Kurugenzi; Kipa Hamza Mpatula na Optatus Lupekenya wamefungiwa mechi
tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa kosa la kupigana
wakiwa uwanjani baada ya mechi kumalizika. Adhabu hiyo ni uzingativu wa
Kanuni ya 37(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
Mechi namba 36 (Rhino Rangers vs Polisi Mara). Klabu ya Rhino Rangers
imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika
20. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 38 (Mgambo Shooting vs Rhino Rangers FC). Kocha wa
Mgambo, Moka Shabani amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh.
300,000 kwa kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi wakati timu zikielekea
vyumbani baada ya kumalizika kipindi cha kwanza. Adhabu hiyo ni kwa
mujibu wa Kanuni ya 40(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.
LIGI DARAJA LA PILI
Mechi namba 17 (Abajalo vs Burkina Faso). Klabu ya Burkina Faso
imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya
mechi (pre match meeting). Adhabu imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi
Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 18 (Cosmopolitan vs Changanyikeni). Klabu ya
Changanyikeni FC imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki
wake kuingia uwanjani kushangilia ushindi baada ya filimbi ya mwisho.
Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Pili
kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 19 (Kariakoo vs Cosmopolitan). Klabu ya Kariakoo imepewa
Onyo Kali kwa timu yake kutokuwa na daktari katika mechi hiyo. Adhabu
hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3).
Mechi namba 16 (Sabasaba vs Namungo). Klabu ya Sabasaba imepewa Onyo
Kali kutokana na washabiki wake kuwazonga waamuzi wakati wakielekea
vyumbani baada ya mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini
Morogoro kumalizika. Uamuzi huo umezingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi
Daraja la Pili.
Mechi namba 17 (Mawezi Market vs Mkamba Rangers). Mkamba Rangers
imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya
mechi (pre match meeting), na pia kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika
35. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.
Mechi namba 19 (Namungo vs Mighty Elephant). Mighty Elephant imepigwa
faini ya sh. 100,000 kutokana na wachezaji wa akiba na viongozi wake
kuingia uwanjani kushangilia bao la timu yao. Kitendo hicho ni kinyume
na Kanuni ya 14(7), na adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(47) ya
Ligi Daraja la Pili.
Malalamiko mbalimbali
Malalamiko ya klabu za Mwadui FC na Polisi Morogoro kuhusu uhalali wa
usajili wa mchezaji wa Stand United, Kheri Mohamed Khalifa na wachezaji
wawili wa Njombe Mji kucheza mechi bila leseni yamepelekwa Kamati ya
Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.
Pia maombi ya klabu ya Singida United kuhusu kubadilishiwa Mwamuzi
kwenye mechi yao yamepelekwa Kamati ya Waamuzi, wakati maombi ya
Alliance Schools, Friends Rangers FC, The Mighty Elephant na Kariakoo FC
yanayohusu uendeshaji yanashughulikiwa na Sekretarieti ya TPLB.
Kuhusu JKT Ruvu
Katika mengineyo, Kamati ilipitia maombi ya timu ya JKT Ruvu Stars FC
kubadilisha uwanja wake wa nyumbani kutoka Mabatini mkoani Pwani hadi
Mkwakwani mkoani Tanga kutokana na wachezaji wake 12 wa kikosi cha
kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi mkoani Tanga.
Ombi hilo limekubaliwa. Kwa mujibu wa Kanuni ya 6(6) ya Ligi Kuu,
TFF/TPLB zina mamlaka ya mwisho kuhamisha kituo cha mchezo kwa sababu
inazoona zinafaa na kwa wakati husika.
Kuhusu Mchezaji Venance Ludovic
Pia
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF inatarajiwa kukaa wiki
ijayo kusikiliza malalamiko dhidi ya usajili wa wachezaji mbalimbali
akiwemo mchezaji Venance Joseph Ludovic.
EmoticonEmoticon