Katika kuufunga mwaka 2024 kwa huduma bora, Benki ya CRDB imefungua matawi mapya mawili mkoani Mara yaliyopo Mugango katika Wilaya ya Musoma Vijijini na Sirari wilayani Tarime.
Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema uzinduzi wa matawi hayo ni sehemu ya jitihada za Benki kuiishi kaulimbiu yake ya ‘ulipo, tupo’ kwa kuwafuata wananchi katika kila pembe ya nchi na kuwapa huduma bora za fedha kwa maendeleo yao binafsi na kuchangia uchumi wa taifa pia.
“Mkoa wa Mara una shughuli nyingi za kiuchumi kuanzia migodi mikubwa na machimbo ya madini, uvuvi, kilimo na biashara ya mpakani hivyo ni muhimu kuwa na huduma za uhakika za fedha ili kuwajumuisha wananchi kwengi katika uchumi. Ulikuwa ni mpango wa Benki yetu ya CRDB kuhakikisha tunafungua matawi haya mawili kabla mwaka 2024 haujaisha,” anasema Raballa.
Kabla ya ufunguzi wa matawi hayo mapya, Raballa amesema wananchi wa maeneo hayo walikuwa wanapata huduma za benki kupitia kwa mawakala waliotapakaa maeneo tofauti. Kwa mkoa mzima wa Mara, amesema Benki ya CRDB inao zaidi ya mawakala 600 wakiwamo 195 wanaohudumia katika Wilaya Ya Tarime na 35 Musoma Vijijini.
“Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya wateja wilayani Tarime na Musoma, Benki yetu iliona kuna umuhimu wa kuboresha huduma ili kuendana na mahitaji yaliyopo sasa na yatakayojitokeza baadaye. Tulifanya utafiti wa kina kabla ya kujenga matawi haya yatakayowahudumia wananchi wa Mugango na Sirari pamoja na maeneo jirani,” amesema Raballa.
Kutokana na uzinduzi wa matawi hayo mawili, Benki ya CRDB sasa imefikisha jumla ya matawi 10 mkoani Mara ambayo ni Musoma, Tarime, Bunda, Serengeti, Nyamongo, Rorya, Shirati, Mugango na Sirari hivyo kuifanya kuwa na mtandao mpana zaidi wa matawi nchini kuliko benki nyingine yoyote nchini.
Akifungua tawi la Sirari, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mheshimiwa Meja Edward Flowin Gowele amesema huduma za fedha ndio msingi wa maendeleo ya mwananchi binafsi, kaya na taifa kwa ujumla hivyo kilichobaki ni umakini wa wananchi kubuni miradi itakayowainua kiuchumi kwa kuzikabili changamoto zilizopo kwenye maeneo yao ili kunufaika na fursa zinazojitokeza.
“Tawi hili ni sehemu salama kwa wananchi kuhifadhi akiba zenu za fedha. Ni mahali ambapo wafanyabiashara mtapata mikopo ya kuimarisha miradi yenu na wafanyakazi nao wataweza kutimiza malengo yao. Benki ni rafiki wa kila mwananchi anayewa na kupanga maendeleo yake, tulitumie tawi hili kujinufaisha kwa kujenga uchumi imara wa kila mmoja wetu,” amesema Mheshimiwa Gowele.
Licha ya kunufaika na mikopo inayotolewa, Mheshimiwa Gowele amewahimiza wananchi wa Sirari, Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara na Tanzania nzima kwa ujumla kuwekeza kwenye Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond inayoendelea kuuzwa na Benki ya CRDB ili kupata fedha zitakazowezesha ujenzi wa barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
“Ukiwekeza katika hatifungani hii una uhakika wa kupata faida ya asilimia 12 inayotolewa kila mwaka kwa muda wote wa miaka mitano wa uhai wake. Lakini, kumiliki hatifungani hii ni sawa na kuwa na nyumba, unaweza kuitumia kama dhamana kuchukua mkopo kutoka taasisi yoyote ya fedha. Nawasihi kila mmoja wenu na Watanzania wote kwa ujumla, kuitumia fursa hii kuwekeza kwenye hatifungani hii,” amesisitiza Mheshimiwa Gowele.
Kwenye uzinduzi wa tawi la Mugango, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya amesema ni fursa kwa wananchi wa Musoma kunufaika na huduma zinazotolewa na Benki ya CRDB zikiwamo zilizo chini ya Programu ya Imbeju inayolenga kuwawezesha vijana na wanawake.
“Ufunguzi wa tawi hili umesogeza kwa karibu fursa za Programu ya Imbeju. Nawaomba wajasiriamali mlitumie tawi hili kupata mitaji wezeshi itakayosaidia kuinua biashara zenu. Hapa, mtapata ushauri wa kitaalamu ia wa namna bora ya kukuza shughuli zenu kwa maendeleo binafsi na taifa pia,” amesema Kusaya.
Sambamba na ufunguzi wa tawi la Benki ya CRDB Sirari, Benki ya CRDB imekabidhi madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzi kwa wanafunzi wa Wilaya ya Tarime. Madawati hayo yamepokelewa na Mheshimiwa Gowele aliyesema yatasaidia kupunguza uhaba uliopo katika shule za msingi na sekondai wilayani Tarime.
EmoticonEmoticon