Kaimu Meneja wa Uwanja wa Taifa
Bw. Julius Mgaya (kushoto) akimuonyesha Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye jinsi Kamera za CCTV
zinavyoweza kumnasa mtu akifanya jambo lolote baya ndani ya Uwanja wa
Taifa wakati alipotembelea kukagua marekebisho ya miundombinu ya uwanja
huo leo 11 Desemba, 2016 Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye, Kaimu Meneja wa Uwanja wa Taifa Bw.
Julius Mgaya pamoja na Waandishi wa habari wakiangalia hatua
iliyofikiwa ya urekebishaji wa viti na miundombinu mingine ya uwanjani
hapo wakati alipotembelea kukagua marekebisho ya miundombinu ya uwanja
huo leo 11 Desemba, 2016 Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye (kulia) akiwa ameongozana na Kaimu
Meneja wa Uwanja wa Taifa Bw. Julius Mgaya pamoja na Waandishi wa habari
wakielekea kuangalia hatua iliyofikiwa ya urekebishaji wa viti na
miundombinu mingine ya uwanjani hapo wakati alipotembelea kukagua
marekebisho ya miundombinu ya uwanja huo leo 11 Desemba, 2016 Jijini Dar
es Salaam.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye akiangalia namna Kamera za CCTV
zinavyofanya kazi ya kubaini matukio yanayoendelea ndani ya Uwanja wa
Taifa wakati alipotembelea kukagua marekebisho ya miundombinu ya uwanja
huo leo 11 Desemba, 2016 Jijini Dar es Salaam.
Na Benedict Liwenga-WHUSM.
Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye leo ametembelea Uwanja wa Taifa
Jijini Dar es Salaam ili kukagua shughuli za marekebisho ya miundombinu
inayoendelea uwanjani hapo ikiwemo kukagua ufanisi wa Kamera za
kufuatilia matukio Uwanjani pamoja na marekebisho ya viti vya kwenye
majukwaa.
Katika ziara yake Waziri Nape
amekagua namna Kamera za CCTV zinavyokuwa na uwezo wa kubaini matukio
mbalimbali yanayoendelea uwanjani ambapo ameridhika na utendaji kazi wa
kamera hizo na kusisitiza zitumike ipasavyo ili kuwabaini wahusika
wanaoharibu miundombinu ya uwanja.
Amesema kwamba kazi ya kubaini
waharibifu wa miundombinu kwa sura katika uwanja huu kwa kutumia hizi
kamera yataongeza hali ya usalama kwenye uwanja na pia kusaidia
kufuatilia matukio ya kihalifu Uwanjani kama vile kuvunja viti”, alisema
Mhe. Nape.
Aidha, amesema kwamba ukarabati wa
uwanja unaoendelea sasa pinid utakapokamilika utaufanya uwanja huo kuwa
salama zaidi na ndiyo maana kamera nyingi zimeweka ili kuendelea
kubaini matukio yanayoendelea ndani na nje ya mipaka ya uwanja ikiwemo
milangoni.
“Kwa sasa uwanja wetu utaweza
kushughulika na mtu mmoja mmoja anayehujumu miundombinu yetu, kwasababu
kamera zetu zina uwezo mkubwa wa kumtambua mtu kwa sura pindi awapo
uwanjani kuanzia magetini”,alisema Mhe. Nape.
Ameagiza ukarabati wa miundombinu
uendelee ikiwemo mageti na viti uendelee kufanyika kwani yeye
anachosubiria ni kukabidhiwa uwanja huo siku ya tarehe 13 Desemba mwaka
huu na siku hiyo ndiyo itafahamika thamani ya ukarabati uliofanyika kwa
ujumla.
Aidha, amegusia suala la Mkataba
ulioingiwa kati ya Serikali na Klabu ya Yanga African ambapo amesema
kwamba, Serikali iliingia Mkataba na Klabu ya Yanga African ya kutumia
uwanja wake wa Taifa pamoja na uwanja wa Uhuru tarehe 1 Desemba, 2016
kwa muda wa mwaka mmoja yaani mpaka tarehe 30 Novemba,2017.
Amesema kwamba, kutokana masharti
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) pamoja na Shirikisho la
Mpira wa Miguu la Afrika (CAF), vilabu vyote vinavyoshiriki michezo ya
Kimataifa vinatakiwa kuonyesha uthibitisho wa umiliki wa uwanja au
viwanja vitakavyotumika katika mechi zao au kuonyesha mkataba walioingia
ambapo mechi hizo zitachezwa.
“Kwa kuwa klabu ya Yanga haina
Uwanja wake, walileta ombi Wizarani, la kuingia Mkataba na Mmiliki wa
Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru yaani Serikali. Serikali iliona ni
busara kuingia mkataba na Klabu ya Yanga African ili pale ambapo
watahitajika kutaja uwanja watakaotumia waweze kutaja Uwanja wa Uhuru au
Uwanja wa Taifa”, alisema Mhe. Nape.
Kwa muktadha huo, Klabu ya Yanga
itaendelea kutumia uwanja wa Uhuru ambao haukujumuishwa katika maamuzi
ya kufungiwa na hauna tatizo la kukarabatiwa.
Amesisitiza kuwa, Serikali ina nia
njema kwa vilabu vyake na wadau wote wa Michezo na Serikali inafanya
shughuli zake kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni, hivyo amevitaka
Vilabu vyote viwe na utamaduni wa kufuata sheria, taratibu na Kanuni
katika kutekelea majukumu yao.
EmoticonEmoticon