JAMII YATAKIWA KUWAHESHIMU NA KUWASAIDIA WAZEE NCHINI

November 26, 2016
Mratibu wa Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya METDO Tanzania  Mathias Canal akimkabidhi Kaimu Mkuu wa Kituo cha Wazee KIILIMA Bi Gladness Lwiza baadhi ya mahitaji kwa ajili ya wazee waishio kituoni hapo.
Kushoto ni Mkurugenzi wa Asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya METDO Tanzania (Mining and Environmental Transformation for Development  Organization) Bw Ashraf Omary akimsikiliza kwa makini mzee aliyelala kutokana na homa kali inayomsumbua
Kushoto ni Dkt Peter Shija Mganga Mfawidhi kutoka zahanati ya Ibosa akisisitiza jambo kwa Afisa ustawi wa Jamii Wilaya ya Nyamagana ambaye pia ni katibu wa TAWSO Mwanza Bi Abigali Mhingo
 Meneja Mradi wa METDO Tanzania Bw Hussein Sungura akisaini kitabu cha wageni kwa niaba ya uongozi wa METDO Tanzania katika kituo cha Wazee KIILIMA Manispaa ya Bukoba, Mkoani Kagera
 Hiki ndicho Choo kinachotumiwa na wazee waishio kambi ya KIILIMA-Bukoba
Moja ya Mzee katika Kituo cha Wazee KIILIMA akiwa amelala kutokana na homa kali iliyokuwa inamsumbua
 Mahitaji yamepokelewa kwa furaha na wazee wote kupitia uongozi wao
Pichani katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Salum Kijuu, Kushoto kwake ni Mathias Canal Mratibu wa Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya METDO Tanzania, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kagera Ndg Charles Mafimbo, Kulia kwa Mkuu wa Mkoa ni Hussein Sungura Meneja Mradi METDO Tanzania na Mkurugenzi wa METDO Tanzania Ndg Ashrafu Omary
Mkurugenzi wa Asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya METDO Tanzania (Mining and Environmental Transformation for Development  Organization) Bw Ashraf Omary akifanya usafi katika jiko la watumishi wa kituo cha wazee KIILIMA
 Mjadala ukiendelea baada ya kazi kumalizika Kijijini KIILIMA kambi ya wazee
Kaimu Mkuu wa Kituo cha Wazee KIILIMA Bi Gladness Lwiza akipanda mti kwa ajili ya kumbukumbu
Tafakuri pana kwa Mzee Wilson Ziraimanikabla ya kukabidhiwa mahitaji na uongozi wa METDO Tanzania
 Nyumba ya kulala wazee wa kituo cha KIILIMA kilichopo Kata ya Nyakato Mkoani Kagera
 Viongozi wkibadilishana mawazo mara baada ya kuzuru kituo cha Wazee KIILIMA
Kijana ni mzee ajaye na Mzee ni kijana aliyekuwa
Hili ndilo jiko linalotumiwa na viongozi wa kituo cha KIILIMA kilichopo nje kidogo ya Manispaa ya Bukoba
Katikati ni Dkt Peter Shija Mganga Mfawidhi kutoka zahanati ya Ibosa akipata maelezo ya awali kwa Moja ya mzee aishie kambini KIILIMA kabla ya kumfanyia vipimo
Mathias Canal Mratibu wa Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya METDO Tanzania akipanda mti wa matunda aina ya Mlimao kwa ajili ya kumbukumbu ya kuzuru kituo cha Wazee KIILIMA
 Majadiliano ya namna ya kuchimba mashimo kabla kupanda miti
 Moja ya nyumba anayoishi Mtumishi wa Kituo cha wazee KIILIMA Kilichopo Mkoani Kagera
Mkurugenzi wa METDO Tanzania Bw Ashraf Omary mwenye Jembe akimsaidia kazi Mzee Wilson Ziraimani, Mzee huyu alikuwa anafanya kazi za kilimo katika mashamba mbalimbali nchini, yeye ni mkazi wa Ngara na wakati akiwa mtoto alikuwa analelewa na Mama wa kambo.
Aliwasili katika kituo cha kulelea Wazee cha KIILIMA Mwaka 1986 hapo alipo anatambaa kwani alivunjika kiuno enzi za ujana wake baada ya kuanguka mtini wakati alipokuwa anakata kuni kwa ajili kupikia.
Viongozi wa METDO Tanzania, Kiongozi wa TASWO, na Viongozi wa kituo cha Wazee KIILIMA wakipanda mti wa matunda aina ya Parachichi kwa ajili ya kumbukumbu na kampeni ya upandaji miti

Na Mathias Canal, Bukoba
 
Kukosekana kwa huduma bora na msingi kwa wazee nchini imetajwa kuwa changamoto kubwa kwa Wazee waishio katika kambi mbalimbali za serikali na zile za binafsi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya METDO Tanzania (Mining and Environmental Transformation for Development  Organization) Bw Ashraf Omary wakati akikabidhi mahitaji kwa wazee wa kituo cha KIILIMA kilichopo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.

Bw Omary alisema kuwa Asasi hiyo yenye usajili No. ooNGO/08317 inajishughulisha na kutoa Elimu ya Mazingira kwa wananchi wanozunguka migodi pamoja na wafanyakazi wa migodini ambapo pia imejikita kuwasaidia wazee waishio katika kambi mbalimbali nchini katika huduma za kuwapatia mahitaji ya msingi ya kila siku kama vile (Chakula, na Mavazi) sambamba na kutoa huduma ya upimaji wa afya zao kupitia wataalamu wa tiba na kuwapatia dawa kwa ajili ya matibabu ya magonjwa mbalimbali.

Alisema kuwa kumekuwa na wimbi kubwa la wazee kutopatiwa huduma bora ikiwemo chakula na matibabu jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linachangia wazee wengi kufariki pasina huduma yoyote ya kitabibu sambamba na kukosa Lishe Bora.

Bw Omary ameushukuru uongozi wa kampuni ya ZONGII PUMBLING LTD ya Jijini Mwanza kwa kushirikiana na METDO Tanzania kufanikisha kupatikana mahitaji mbalimbali kwa ajili ya wazee wa kambi ya KIILIMA sambamba na kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Kagera kwa ushirikiano ulioonyesha ikiwa ni pamoja na kuruhusu madaktari kwa ajili ya kwenda kuwapima afya wazee hao.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa METDO Tanzania Bw Hussein Sungura amebainisha kadhia zinazowakumba wazee katika kituo cha KIILIMA sambamba na vituo vingine nchini kuwa ni pamoja na ukosefu wa huduma za usafiri ili kurahisisha wazee kufikishwa haraka hospitalini pindi wauguapo, Ufinyu wa Bajeti, Ukosefu wa vitendea kazi kama vile vifaa vya usafi na ucheleweshaji wa Ruzuku ya serikali.

Sungura alisema kuwa Mpaka sasa Asasi hii ya METDO Tanzania imesaidia katika maeneo mbalimbali ikiwemo tukio la Agosti 13, 2016 la kumuenzi Mwl Julius Kambarage Nyerere katika Makao ya wazee wasiojiweza BUKUMBI Mwanza, Tukio la Octoba Mosi 2016 SIKU YA WAZEE DUNIANI katika wilaya ya Shinyanga ambapo jamii ilishirikishwa kutambua changamoto zilizopo katika kituo cha Wakoma na Wazee wasiojiweza cha KOLANDOTO pamoja na Kituo cha Wakoma na  Wazee wasiojiweza cha NYABANGE BUTIAMA  na kuwa sehemu ya kuzitatua changamoto hizo.

Kutokana na kazi hiyo ya wito inayofanywa na METDO Tanzania Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Salim Kijuu ametoa wito kwa Asasi hiyo kuwekeza Mkoani Kagera katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo ili ushirikiano wa kusaidia wazee uweze kukomaa na kusaidia wazee wote nchini kirahisi sambamba na kutoa fursa kwa vijana kutambua umuhimu wa kufanya kazi sawia na kujiajiri.

Kijuu alisema kuwa kutokana na Mkoa wa Kagera kuwa na hali nzuri ya hewa na udongo wake kuwa na rutuba ni vyema Asasi ya METDO Tanzania ikafanya kazi yake kwa misingi ya katiba lakini pia inapaswa kuwasaidia vijana wengi nchini ili kuachana na uvivu walionao badala yake kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika kuisimamia na kutekeleza kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.

Akisoma taarifa ya kituo hicho Kaimu Mkuu wa Kituo cha Wazee KIILIMA Bi Gladness Lwiza alisema kuwa Kituo hicho kina jumla ya wahudumiwa 24 ambapo kati yao kuna watoto 6 waliokuwa kwenye mazingira hatarishi baada ya kutelekezwa na wazazi wao huku wengine wakipokelewa baada ya wazazi wao kufariki kutokana na janga la UKIMWI lililotokea mwaka 1984.

Hata hivyo amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza na kuwachukua watoto hao kwani kuendelea kubaki katika kituo hicho sio jambo jema kwao kwani wanachanganyikana na wazee ambao wengi wao wana matatizo ya akili.

Lwiza amesema kuwa kufuatia uharibifu wa majengo kutokana na Tetemeko lililotokea hivi karibuni Mkoani Kagera na kuharibu majengo mengi kituoni hapo imesababisha kukosekana kwa nyumba za watumishi, na choo kwa ajili ya matumizi ya wazee pamoja na watumishi wa kituo hicho.

Naye Dkt Peter Shija Mganga Mfawidhi kutoka zahanati ya Ibosa ameiomba serikali kusaidia upatikanaji wa sehemu maalumu ya kuhifadhia dawa, kutolewa mafunzo ya tiba kwa wahudumu waliopo kituoni hapo sambamba na kupatikana kwa vifaa tiba kwa ajili ya kupima damu, Sukari, MRTD, Presha na wingi wa damu.

Kituo cha Wazee KIILIMA kilichopo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera kilicho chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni moja kati ya vituo vya kulelea wazee hapa nchini ambapo awali kilikuwa chini ya kanisa la Roman Catholic na baadaye kilikabidhiwa rasmi kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwaka 1974.

Baada ya kutembelea vituo vyote vya Wazee kanda ya Ziwa METDO Tanzania inataraji kuzuru Mikoa ya Kanda ya kati kwa ajili ya kujionea changamoto za wazee mbalimbali waishio kambini na kuzifikisha sehemu husika wakiwemo viongozi wa dini, Wafanyabiashara, Serikali na Wadau mbalimbali nchini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »