Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akifafanua jambo
kuhusu wananchi waliovamia msitu wa hifadhi ya Kijiji. Kushoto ni Bi.
Veronica Nyasa mkazi wa eneo hilo ambae amesema yuko tayari kuondoka
endapo atapatiwa sehemu mbadala.
Uongozi wa Wilaya ya Kaliua
wakimwonyesha Waziri Makamba magogo ya miti ya asili yanayotumiwa na
wanachi katika kukaushia tumbaku kwa kutumia majiko ya kienyeji
Pichani ni moja ya majiko ya
kienyeji yanayotumia kuni/miti mingi katika kukaushia tumbaku. Waziri
Makamba amewaagiza wakazi wa Kitongoji cha Mtakuja Magharibi kutumia
majiko banifu ili kunusuru ukataji miti kwa wingi husnan ile ya asili
…………………………………………………………………
Na Lulu Mussa-Tabora
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais Muungano na Mazingira hii leo ameendelea na ziara ya kikazi katika
Mkoa wa Tabora akitokea Mkoani Kigoma.
Akiwa Mkoani Tabora Waziri
Makamba ametembelea Wilaya ya Kaliua na kukutana na changamoto kubwa ya
Uharibifu wa Mazingira na Uvamizi wa Misitu unaofanywa na wananchi.
Katika Kijiji cha Ufugala Wilaya ya Kaliua Waziri Makamba amefanya
Mkutano wa hadhara kijijini hapo na kubaini kuwa Kitongoji hicho
hakikufuata taratibu za kisheria katika kuanzishwa kwake na kimeanzishwa
ndani ya Hifadhi.
Akitoa maelezo ya Awali Mkuu wa
Wilaya ya Kaliua Bw. Abel Yeji Busalama amemueleza Waziri kuwa Kitongoji
hicho kiko ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Kijiji ambapo jumla ya Vijiji
11 viamua kutenga eneo hilo kwa ajili ya Hifadhi.
Bw. Busalama amesema kuwa wakazi hao wamekwisha amriwa kuondoka katika hifadhi hiyo na utekelezaji wake unaendelea.
Akijibu hoja zilizowasilishwa na
wakazi wa eneo hilo Waziri Makamba amesema kuwa wajibu wa Serikali ni
kuhakikisha kuwa Sheria, tararibu na kanuni zinafuatwa bila kukiukwa.
Waziri Makamba pia amesisitiza kuwa maamuzi ya matumizi bora ya ardhi
yapo mikononi mwao. “Ndugu zangu ni nyinyi wenyewe mliamua kutenga eneo
hili maalumu kwa hifadhi ya msitu wa kijiji na kufuata taratibu zote za
kisheri katika kuusajili, maamuzi yenu ya awali yatabaki palepale mpaka
mtakapofuata taratibu nyinginezo.” Makamba alisisitiza.
Aidha, Waziri Makamba ameahidi
kuwasilisha suala hilo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii na ile ya
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
“Nitaongea na Mawaziri wenzangu na kuleta timu ya wataalumu kupitia upya
mipaka ya kijiji na kuifanyia kazi” Makamba alisisitiza.
Kuhusu hifadhi ya Mazingira
Waziri Makamba amewataka wakazi wa Ufulaga kuacha tabia ya kukata miti
ya asili na kusisitiza kuwa uharibifu wa mazingira unabadilisha tabia
za watu. “Wana Ufulaga, binadamu wakiharibu mazingira kwa kiasi kikubwa
wanaanza wizi na udokozi na wanyama wataanza kuwinda watu kwa kukosa
malisho” alisema Waziri Makamba.
Waziri Makamba pia amefanya ziara
katika Wilaya ya Urambo na kubaini changamoto kubwa ya uvamizi wa
misitu na ukataji wa miti ya asili kwa ajili ya kuni za kukaushia
tumbaku.
Waziri ameliagiza Baraza la Taifa
la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutumia Sheria ya Mazingira
namba 20 ya mwaka 2004 kifungu namba 196 (1) (a na b) kupiga marufuku
ya matumizi ya majiko banifu ya kienyeji pia ukataji mkubwa wa miti ya
asili kwa ajili ya biashara ya tumbaku. Katazo hilo litawahusu Wakulima
na Vyama vya Msingi vyote vinavyojishughulisha na biashara ya tumbaku.
Waziri Makamba anaendelea na ziara yake kwa kutembelea Wilaya za Nzega na Igunga.
EmoticonEmoticon