Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MAKAMU wa rais ,Samia Suluhu
Hassan,amewataka kuwafichua watumishi mbalimbali wa halmashauri na
taasisi za serikali katika wilaya na mikoa wanaodhaniwa kufuja fedha za
serikali na kupoteza mapato lengo ikiwa ni kuzikusanya fedha na
kuzirudisha katika mikono ya wananchi waone faida yake.
Amesema serikali ya awamu ya tano
inaendelea na nguvu yake ya kukusanya mapato na kuziba mianya ya rushwa
na kupotea kwa mapato na amewasisitiza wananchi kulipa kodi pale
inapohitajika ili kusaidia na serikali kuinua mapato yake.
Aidha Samia ametoa rai kwa
wananchi mkoani Pwani kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na
usalama kulinda amani na usalama wa mkoa huo kufuatia kujitokeza kwa
mambo ambayo yameonekana kuhatarisha usalama wa mkoa hivi karibuni.
Katika hatua nyingine
amewahakikishia wakazi wa mji wa Chalinze kutatua tatizo la maji ambalo
bado ni kero kubwa ambapo ameeleza kwamba mwishoni mwa mwaka huu matunda
yataanza kuonekana.
Akizungumza na baadhi ya wananchi
wa Mlandizi na Chalinze,mkoani Pwani wakati aliposimama kuwasalimia
akielekea mjini Dodoma kikazi,alisema wananchi waiamini serikali yao
kwani imeanza kuirejesha nchi katika nidhamu ya mapato na matumizi na
kazi ya maendeleo inaendelea.
“Watanzania watajenga Tanzania
yao wenyewe na serikali yake na Tanzania inaweza kujiendesha yenyewe na
kama itategemea misaada iwe sio kwa kiasi kikubwa.”alisema.
Hata hivyo Samia aliwataka
wakulima na wafugaji kuishi kwa upendo na mshikamano baina yao pasipo
kutofautiana kwani kwa kufanya hivyo kunasababisha migogoro isiyo na
tija na wakati mwingine kuvunja amani.
Kufuatia ombi la mbunge wa jimbo
la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete ,kumeelezea kuhusu kero ya maji
inayowakabili wakazi wa jimbo hilo,Samia alisema serikali inatambua hilo
na kwasasa ipo katika mpango mzuri wa kumaliza tatizo la maji lililopo.
Alielezea kuwa WAMI yapo maji ya
kutosha lakini tatizo ni usambazaji ,hivyo wanatarajia kuvuta maji kwa
mabomba hadi eneo la Pera na kujenga matanki makubwa yenye ujazo wa lita
300,000 ,Kibiki watajenga tanki lenye ujazo wa lita 200,000 ili maji
yakifungwa kuweze kuwa na maji ya kufikisha kwa wananchi kirahisi.
Makamu huyo wa rais alisema
watajenga hifadhi nyingine ya maji pale Mazizi yenye lita mil.2 ambayo
itawezesha kutumia maji ndani ya wiki mbili bila kukatika ambapo mpango
huo upo njia na tayari mkandarasi yupo na wametanguliza sh.bil 43 ili
kazi ianze .
Samia wakati anafanya kampeni ili
kuomba kuchagulia kuingia madarakani aliahidi kuwatua akinamama ndoo
kichwani kwa kutatua tatizo la maji na kusema anashughulikia suala hilo
hadi hapo atakapowaondolea wananachi adha ya kutembea umbali mrefu
kusaka huduma hiyo muhimu.
“Nayachukua mambo yote na nitaendelea kuyafanyia kazi ,natambua
kilio chenu hasa akinamama ambao huamka usiku ama kutembea umbali mrefu
kutafuta maji”alisema Samia.
Akizungumzia suala la afya kuhusu
vifaa tiba alisema atazungumza na wizara husika kutatua kero ya vifaa
tiba,madawa na watumishi katika kituo cha afya Msoga ili kupunguza mzigo
kwa hospitali za rufaa ikiwemo Tumbi.
Alisema tatizo la watumishi
karibu litamalizika,kulikuwa na idadi kubwa ya watumishi hewa hivyo
walikuwa wakiisafisha watumishi hao na hivi karibuni watafungua ajira
mpya baada ya zoezi hilo kukamilika.
Samia aliipongeza Chalinze
kumaliza tatizo la madawati ila kwenye mafanikio kunajitokeza tatizo
jingine hasa kutokana na idadi ya wanafunzi imekuwa kubwa na kuzalisha
tatizo la madarasa .
Aliwataka viongozi wa wilaya na
mkoa kuelekeza nguvu zao kujenga ,kuongeza na kukarabati majengo ya
madarasa ili watoto waweze kusoma .
Kuhusiana na ahadi ya ujenzi wa
soko na stend mjini Chalinze,amemuagiza mkuu wa mkoa huo,mhandisi
Evarist Ndikilo kuhakikisha anasimamia hatua ya tathmini ya eneo
lililopatikana kwa ajili ya ujenzi huohadi ifikapo mwezi novemba mwaka
huu.
Viwanda na uwekezaji,anasema
serikali kwasasa inasuka nguvu za viwanda na uwekezaji mkoani hapo
kujenga kwa ajili ya kutengeneza ajira na kukuza uchumi wa mkoa .
Alisema viwanda vikubwa 10
vitajengwa ikiwemo cha chuma na nondo,cha kutengeneza vigae na kusindika
matunda hivyo wananchi wawe tayari kupokea wawekezaji ili kupunguza
tatizo la uhaba wa ajira.
Akiwa Mlandizi ,Samia aliahidi
kuweka uzio kama alivyoahidi wakati wa kampeni kwenye uchaguzi uliopita
katika kituo cha afya Mlandizi kwani ni moja ya sifa ya kuandishwa kwa
kituo cha afya kupanda hadhi ya wilaya na bado wanania ya kupandisha
hadhi ya kvituo mbalimbali ili kuzipunguzia mzigo hospitali za rufaa .
Alisema soko la mlandizi bado ni
dogo ila ana taarifa kuwa kwenye eneo la Kisabi A na B kuna maeneo
yamepimwa kwa ajili ya masoko na Tamisemi wameweka mkono kidogo na
kuwahakikishia kuwa atakaa na Tamisemi kuangalia uwezekeno wa kuachia
maeneo hayo ili kuwepo na soko na stend kubwa .
Alieleza kupimwa kwa mji wa
Mlandizi ataongea na wizara ya ardhi na sasa bahati nzuri wizara hiyo
wamekuwa wepesi kufanya zoezi hilo hivyo ataweka msukumo kwa wizara ili
waweze kupimiwa na barabara ya Mlandizi-Mzenga ahadi ipo palepale
itajengwa kwa kiwango cha lami .
Anafafanua halmashauri ya wilaya
ya Kibaha Vijijini inabidi waende Kibaha mjini hivyo watajaribu
kuangalia la kufanya ili halmashauri ihamie Mlandizi na ili hali
wananachi wapate huduma kirahisi pasipo kwenda Kibaha mjini.
Awali mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani,alisema Chalinze
inashida kubwa ya maji ,hivyo serikali iangalie jambo hilo kwa jicho la
huruma,
TANROARS kuchelewesha tathmini ya eneo la soko na stend wakati
ikiwa ni ahadi ya mh rais John Magufuli kuhakikisha kunapatikana eneo la
soko na stend.
Alisema anaimani na kasi ya
serikali iliyopo madarakani na chama cha mapinduzi kuwa
watayashughulikia masuala hayo ili kurejesha imani kwa wananchi hao.
Ridhiwani alisema fedha
zinazotolewa na serikali kutekeleza masuala ya afya na miradi mbalimbali
zitoke na kufanyiwa kazi lengwa badala ya kusemwa midomoni bila kuziona
na kuzifanyia kazi.