Kuanzia mwakani kila Mwanafunzi
wa darasa la kwanza akiripoti atatakiwa kuja na mche wa mti na
ataupanda na kuutunza kwa miaka yote saba na hatapewa cheti cha kumaliza
darasa la saba kabla hajaonyesha mti wake. Katika shule zenye maeneo
madogo, miti hiyo itapandwa katika maeneo yatakayoelekezwa na Serikali
za Vijiji na Mitaa. Kwa wanafunzi wa Sekondari, itakuwa hivyo hivyo
lakini itakuwa miti mitatu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na
Mazingira Mhe January Makamba amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu
wa Rais kuanzia mwakani itatoa maagizo kwa Halmashauri zote nchini
kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anayeanza darasa la kwanza katika shule
za serikali na zile za binafsi atahitajika kufika shuleni na mche mmoja
wa mti siku ya kuanza masomo ikiwa kama moja ya mahitaji ya msingi na
kwa upande wa wanafunzi wa sekondari watapaswa kufika na miche mitatu
wakati wa kuanza masomo.
Waziri Makamba ameainisha kwamba maelekezo yatapelekwa
Wizara ya Elimu na TAMISEMI na moja ya mahitaji ya kupewa cheti cha
kuhitimu ni kukabidhi miti iliyopandwa wakati mwanafunzi anaingia kuanza
masomo hivyo atahitajika kutunza na kuhudumia miti hiyo kipindi chote
cha masomo.
Waziri Makamba ameyasema hayo wakati akishiriki zoezi la
upandaji miti na wanafunzi katika Shule ya Msingi Mlandege iliyopo
katika Kata ya Kwakilosa, Manispaa ya Iringa ambapo aliongozana na
viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Iringa. Waziri Makamba ametanabaisha kuwa
lengo la kushiriki zoezi la upandaji miti pamoja na wanafunzi hao ni
kutuma ujumbe mahsusi na wa uhakika kabisa kwamba uhifadhi,usimamizi na
utunzaji wa Mazingira ni jukumu la msingi kwa manufaa ya kizazi
kinachokuja na ndio sababu hasa ya kushiriki na wanafunzi ili waweze
kujifunza na kuelewa.
Waziri Makamba ameainisha kuwa katika shule zenye uhaba wa
maeneo yanayoweza kutumika kwa upandaji miti, maeneo mbadala
yatakayoelekezwa na serikali za vijiji na mitaa.
Waziri huyo mwenye dhamana ya Mazingira amesema hili
linafanyika ikiwa ni moja kati ya hatua mahsusi, stahiki na za maksudi
zinazochukuliwa na Serikali katika kuendana na mabadiliko ya tabia nchi
hasa ikizingatiwa kuwa asilimia 61 ya nchi yetu ipo katika tishio la
kuwa jangwa.
Vilevile Waziri Makamba amesema kuwa kuanzia tarehe 5-6
Novemba Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti na Mameya wote
watakutana Jijini Arusha Kwaajili ya kupata mafunzo na maelekezo mahsusi
yanayohusiana na Hifadhi ya Mazingira, ikiwemo upandaji miti na
utunzaji wa vyanzo vya maji
EmoticonEmoticon