Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Ummy Mwalimu amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa kuhakiki takwimu za
chanjo na kuzitawanya wilaya kwa wilaya ili kuhakikisha vituo vyote
vinapata chanjo zilizopo.
Waziri Ummy ametoa agizo hilo
leo mjini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa kuhusu upungufu wa baadhi ya
chanjo katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Waziri Ummy amesema kuwa licha
ya kuwa na uhaba wa chanjo, kuna baadhi baadhi ya wilaya ambazoo chanjo
ya aina moja haipo wakati wilaya nyingine chanjo hiyo ipo.
“Licha ya uhaba wa chanjo, kuna
baadhi ya wilaya ambazo chanjo ya aina moja haipo ila wilaya nyingine
chanjo hiyo ipo, kwa mfano chanjo ya kifua kikuu kwa manispaa ya Dodoma,
kuna chanjo dozi 6540 wakati wilaya za Bahi, Chamwino na Chemba hakuna
kabisa chanjo hiyo”, amefafanua Waziri Ummy..
Hata hivyo Waziri Ummy amewataka
Waganga hao Wakuu wahakikishe wanapitia takwimu hizo ndani ya mikoa yao
ili kuweza kuzitawanya chanjo hizo kwenye wilaya zote ambazo hazina au
zenye upungufu.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa
ili kukabiliana na upungufu chanjo nchini, Wizara hiyo imenunua na
inategemea kupokea chanjo kiasi cha dozi milioni mbili za kinga dhidi ya
Kifua Kikuu (BCG) Septemba 28, mwaka huu, chanjo ya Polio dozi milioni
mbili Septemba 19, 2016 na chanjo ya Pepopunda dozi 1,240,000 Septemba
26, mwaka huu.
Pia Waziri Ummy amesema kuwa
Wizara imepokea fedha kutoka Hazina kwa ajili ya ununuzi wa chanjo
nyingine za Surua na Rubella na zitategemewa kutumwa Shirika la
Kimataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) mbao ndio wanunuzi wa
chanjo nchini.
Mbali na hayo Wizara hiyo
inaendelea kuwahimiza wananchi hasa wazazi na walezi wenye watoto wa
umri wa kupata chanjo, kuwa mara wapatapo taarifa ya uwepo wa chanjo
zilizokosekana wawapeleke watoto wao ambao hawakupata chanjo au
kukamilisha chanjo kulingana na ratiba ili kuweza kukamilisha chanjo zao
na kuwahakikishia usalama wa afya watoto wao.
Zaidi ya hayo, Serikali
inawahakikishia wananchi wote kuwa huduma za afya ikiwemo chanjo
zinaendelea kutolewa nchini bure, hivyo wananchi waendelee kutumia
huduma hizo wakati wote kwani chanjo ni haki ya msingi kwa kila mtoto.
Chanjo ambazo zilikuwa na
upungufu nchini ni pamoja na chanjo kwa ajili ya kukinga ugonjwa wa
Surua na Rubella (MR) Kifua Kikuu (BCG), Polio (OPV) na Pepopunda (TT)
ambazo hutumika kwa watoto kuanzia wanapozaliwa hadi miaka miwili na
kina mama wajawazito kulingana na mwongozo wa chanjo uliotolewa na
Wizara ya Afya ili kuwakinga na magonjwa hayo.