Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape
Nnauye (MB) kesho Jumamosi Septemba 10, anatarajiwa kutembelea Ofisi za
Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), zilizoko
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume ulioko kwenye makutano ya barabara
za Uhuru na Shaurimoyo, Ilala jijini Dar es Salaam.
Akiwa TFF kuanzia saa 4.30 asubuhi, Waziri Nape atazungumza na
Mwenyeji wake Rais wa Shirikisho la Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil
Malinzi pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji pamoja na
Sekretarieti kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari ambao TFF
imeawaalika katika ziara hiyo.
Katika ratiba hiyo, Nape ataonyeshwa maendeleo ya michezo hususani
mashindano yanayodhaminiwa na Kampuni ya Airtel na kuratibiwa na TFF
ambako kwa mikoa mbalimbali iliyofanya vema, kesho timu za wanawake na
wanaume zitacheza hatua ya nusu fainali kabla ya fainali za Jumapili
ambazo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.