Benki ya Diamond Trust (DTB) leo imesaini kuingia mkataba na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kudhamini Ligi Kuu Soka
Tanzania Bara (VPL) kwa msimu wa mwaka 2016/2017.
DTB inaungana na mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na wadhamini
wengine katika kudhamini ligi hiyo maarufu kama Ligi Kuu ya Vodacom.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla ya utiaji saini huo
iliyofanyika Hoteli ya Serena, Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa Benki hiyo,
Joseph Mabusi amesema: “Udhamini huu utasaidia zaidi maendeleo ya soka
nchini kwa kuziwezesha timu timu shiriki pamoja na jitihada zingine za
TFF. Soka inaunganisha Watanzania wa matabaka mbalimbali ambao ni wateja
wetu na si kama benki tungependa kuwa karibu nao zaidi kupitia mchezo
huu.”
Mabusi aliongeza kwa kusema: “Tunafurahi na kujivunia kuwa sehemu ya
ligi kuu na tunaamini udhamini huu utazidisha ari ya kuwahudumia
Watanzania wote.
Benki ya Diamond Trust imekuwa ikiipa kipaumbele michezo mbalimbali
ikiwemo soka, ambapo timu rasmi ya soka inayoundwa na Wafanyakazi
imefanikiwa kushinda vikombe na mataji mbalimbali ya soka likiwemo taji
la ligi ya mabenki nchini inayojulikana kama BRAZUKA KIBENKI mwaka 2015
pamoja na ngao ya hisani ya ligi hiyo mwaka 2016.
Benki pia inadhamini timu ya soka ya Agathon iliyopo Mbagala
inayoshiriki ligi soka daraja la tatu. Zaidi ya hayo benki pia
inajivunia kuwa moja kati ya wadhamini wa michuano ya CECAFA Kagame Cup
mwaka 2015.
Ligi hiyo inajumuisha timu 16 kutoka Tanzania bara zinazocheza kwa
mfumo wa mechi za nyumbani na ugenini ambazo ni Young Africans, Simba
Sports Club, Azam FC, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Mbeya City, Majimaji,
MbaoFC, African Lyon, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Tanzania Prisons, Stand
United, mwadui FC, Ndanda FC na Toto Africans.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Shirikisho la Soka
Tanznaia –TFF wakiongozwa na Rais wao Ndugu Jamal Malinzi, Wafanyakazi
wa Benki ya DTB, wawakilishi kutoka Vodacom, wadau mbalimbali wa soka
pamoja na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari
nchini.
Malinzi ameshukuru na kuupongeza udhamini huo uliotolewa na benki
hiyo na pia ameziomba taasisi nyingine kuiga mfano huo ili kukuza soka
nchini. “Kwa heshima ana furaha kubwa nawakaribisha DTB Tanzania kwenye
ligi kuu na familia ya TFF kwa ujumla.”
Benki ya Diamond Trust ina matawi 25 nchini, ikiwa na matawi kumi na
moja (11) jijini Dar es Salaam (Mtaawa Jamaat, Masaki, Morocco,
Magomeni, Mbezi, Mbagala, barabara ya Nyerere, Msimbazi - Kariakoo,
barabara ya Nelson Mandela, Upanga katika barabara ya umoja wa mataifa
na katika makutano ya barabara ya Mirambo na mtaa wa Samora).
Vile vile ina matawi katika miji ya Arusha (2), Mwanza (2) na katika
miji ya Dodoma, Kahama, Mbeya, Morogoro, Moshi, Mtwara, Mwanza, Tabora
,Tanga na Zanzibar.
DTB Tanzania ni mshirika wa mtandao wa maendeleo ya kiuchumi wa Aga
Khan - Aga Khan Fund for Economic Development (AKFED) ambao ni sehemu ya
mtandao wa maendeleowa Aga Khan Development Network).
DTB Kenya ni miongoni mwa wanahisa muhimu wa DTB Tanzania.
DTB Tanzania pia ni sehemu ya mtandao wa mabenki ya DTB Group yenye matawi zaidi ya 120 Afrika Mashariki na kati.
EmoticonEmoticon