KATIBU Tawala wa wilaya ya Tanga (DAS),Faidha Salim
amesema wilaya hiyo itawachukulia hatua kali za kisheria walimu
wakuu wa shule za msingi na sekondari ambao watabainika shule zao kuwa na
wanafunzi hewa wanaoingizwa kwenye bajeti ya mgao wa fedha zinazotolewa kutoka
serikali .
Faidha aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Tanga Raha blog katika mahojiano maalumu kuhusu hatua ambazo watazichukua
kwa shule ambazo zitabainika kuwa na wanafunzi hewa kutokana na agizo la Rais
Magufuli la kutaka kuwepo uhakiki huo ili kuona fedha zinazotumika kihalali.
Alisema kuwa kwa wilaya ya Tanga tayari walikwisha
kuanza mchakato huo wa uhakiki kwa kutoa fomu ambazo zitapelekwa kwenye shule
zote ili kuweza kubainika uwepo wa wanafunzi hewa ambao waliingizwa kwenye mgao
wa fedha zinazotolewa na serikali.
“Unajua hivi
sasa tunachokifanya sisi kama wilaya ya Tanga kwa kushirikiana tumeanza
mchakato huo wa uhakiki hivyo tunachokifanya hivi sasa ni kupata idadi kamili
ya wanafunzi na fedha kiasi gani ambacho kilipelekwa ili kujua hatua za
kuchukua”Alisema.
“Kama
ujuavyo katika wilaya ya Tanga tuna shule za serikali za sekondari 26 na za
msingi 79 hivyo tunachokifanya ni kutoa fomu hizo na baadae watapata maelezo
kutoka kwa walimu wakuu ambao watabainika kuna wanafunzi hewa kwanini wanawapokea
wanafunzi hewa wakati wanajua kufanya hivyo ni kosa kisheria “Alisema.
Aidha alisema kuwa shule ambazo zitabainika kuwepo
kwa wanafunzi hewa walimu wakuu watashughuliwa kwa mujibu wa sheria zilizopo
kutokana na kuisababishia hasara serikali kwa kutoa fedha ambazo zinapotea.
Katika hatua nyengine,Katibu Tawala huyo alisema
kuwa hivi sasa wilaya ya Tanga inaendelea na mchakato wa uhakiki wa watumishi
hewa na wamekwisha kufikia asilimia 50 hivyo wanatarajia kukamilisha kazi hiyo
mwishoni mwa mwezi huu.
EmoticonEmoticon