Baada ya kutekeleza ahadi ya mwanzo ya kuipeleka Madagascar kwa
ajili ya kambi ya kuivaa Afrika Kusini ‘Amajimbos’, Rais wa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amepanga kutekeleza
ahadi yake nyingine kwa kuipeleka timu ya taifa ya Tanzania ya vijana
wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kwenye kambi tulivu,
ikiwezekana nje ya nchi.
Rais Malinzi aliahidi na kutekeleza ahadi yake kuipeleka Madagascar
Serengeti Boys baada ya kuitoa Shelisheli katika michuano ya Kombe la
Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Madagascar, mwakani. Kadhalika
aliahidi kuipeleka timu hiyo nje ya nchi ambayo hata hivyo haijateuliwa
baada ya kuindoa Afrika Kusini. Ameahidi kambi hiyo itaanza Septemba
mosi, mwaka huuu.
Serengeti Boys ilipiga kambi Hosteli za TFF, zilizo Karume kwa wiki
moja kabla ya kuhamia Hoteli ya Urban Rose, katikati ya jiji la Dar es
Salaam ambako ilivunjwa kwa muda jana Agosti 22, 2016 ambako vijana
wamekwenda makwao kusalimia ndugu zao na itaitwa mwishoni mwa mwezi huu
kwa ajili ya maandalizi ya kambi ya nje ya nchi.
Serengeti Boys imebakiwa na mtihani mmoja kufuzu kucheza fainali hizo
kwa kucheza na Congo – Brazaville na mchezo wa kwanza utafanyika Dar es
Salaam, Septemba 18, 2016 kabla ya kurudiana Septemba 30, 2016, Oktoba 1
au Oktoba 2, 2016.
TFF imejipanga kwa ajili ya kambi hiyo, na kinachosubiriwa kwa sasa
ni mapendekezo ya makocha ili shirikisho itekeleze hatua hiyo ya kambi
ya utulivu.
Kocha Mkuu wa
Serengeti Boys, Bakari Shime maarufu kama Mchawi Mweusi amesema kwamba
anaamini kuwa mchezo ujao utakuwa mgumu kwa kuwa kila timu nitajipanga
kuvuka ili kucheza fainali hizo.
EmoticonEmoticon