Jumla ya kikosi cha watu 35 ambao ni wachezaji na viongozi wa MO
Bajaia kutoka Algeria, wametua Dar es Salaam, usiku wa kuamkia jana
Agosti 9, 2016 na imefikia Hoteli ya Ledger Plaza, iliyoko Kunduchi
Beach nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Timu hiyo imekuja kucheza na Young Africans ya Dar es Salaam, katika
mchezo wa nne wa hatua ya Nane Bora kuwania Kombe la Shirikisho Barani
Afrika utakaofanyika Jumamosi Agosti 13, 2016 kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Licha ya kwamba Young Africans kuwa na pointi moja, bado ina nafasi
ya kushika nafasi za juu katika kundi la A ambalo msimamo wake
unaongozwa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku
Mo Bajaia ya Algeria na Medeama ya Ghana, zina pointi tano kila moja.
Wakati Young Africans wanacheza na Mo Bajaia iliyoshinda mchezo wa
kwanza huko Algeria, Medeama itakipiga na TP Mazembe.
Mchezo wa Young Africans dhidi ya Mo Bajaia utachezeshwa na waamuzi
kutoka Ethiopia ambako katikati atakuwa Bamlak Tessema Weyesa akisaidiwa
na Kindie Mussie mstari upande wa kusini na Temesgin Samuel Atango
katika mstari wa Kaskazini upande wa wakati Mwamuzi wa Akiba atakuwa
Haileyesus Bezezew Belete.
Kamishna wa mchezo atakuwa Gaspard Kayijuka kutoka Rwanda wakati
Desire Gahuka wa Burundi atasimamia ufanisi wa waamuzi wa mchezo na
Mratibu Mkuu wa mchezo atakuwa Isam Shaaban kutoka Sudan. Mratibu huyo
anatarajiwa kuwasili leo Agosti 10, 2016 wakati waamuzi watatua kesho
Agosti 11, 2016 na msimamizi wa waamuzi atatua Ijumaa Agosti 12, 2016.
Kiingilio katika mchezo huo kitakuwa ni Sh 3,000 kwa mzungunguko kwa
maana ya viti vya kijani, bluu na chungwa wakati Viti Maalumu vyenye
hadhi ya daraja B na C kiingilio kitakuwa Sh 10,000 wakati A kiingilio
kitakuwa ni Sh 15,000 kwa mujibu wa Waratibu wa Young Africans.
EmoticonEmoticon