Kutoka Kushoto ni Eng Sadick Chakka Mhandisi wa Maji Wilaya ya Ikungi, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji jumanne Mtaturu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally J. Mwanga, na Kulia ni Abel Suri Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Wakuu wa Idara na Vitengo, na Madiwani wakisikiliza hotuba ya Mkuu wa Wilaya hiyo
liyesimama ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi akisisitiza jambo
Umakini umeonekana wazi wakati wa uwasilishwaji wa hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya ikungi Miraji Jumanne Mtaturu
Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii ambaye ni Diwani wa Kata ya Issuna Steven Misai akitoa neno la shukrani kwa hotuba ya mkuu wa Wilaya ya ikungi
Na Mathias Canal, Singida
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu
amewaonya baadhi ya wanasiasa hususani madiwani katika Wilaya hiyo kupitia
matamko yao ya kuzuia ukusanyaji wa ushuru au kupiga vita vizuizi vilivyowekwa
katika kata zote.
Madiwani hao wanatumia vibaya Uelewa mdogo wa wananchi
kwa kuwazuia kuchangia shughuli za maendeleo na ulipaji kodi hivyo amewaagiza
madiwani wote kuacha kuwatumia wananchi kwa muktadha wa kuwanyima ufahamu
bali wawe mstari wa mbele kuwaelimisha kwa kushirikiana na wataalamu
wanaopita kukusanya kodi katika maeneo yao.
Dc Mtaturu ameyasema hayo wakati wa kikao chake cha kwanza cha
Baraza la madiwani la Wilaya hiyo tangu alipoteuliwa na Rais John Magufuli kushiriki
kwenye baraza la madiwani ambapo pamoja na hotuba yake hiyo amewapongeza
madiwani wote kwa kuaminiwa na kuchaguliwa kwa ajili ya kuwawakilisha
wananchi katika kata zao.
Dc Mtaturu amesema kuwa Baraza la madiwani ndio
injini kuu ya maendeleo ya Wilaya, hivyo kama kukiwa na Baraza lisilotimiza
wajibu wake kamwe Wilaya haiwezi kutoka kwenye kadhia iliyopo hususani
katika sekta ya Kilimo, Mifugo, uvuvi, elimu, afya na miundombinu.
“Wilaya yetu bado ina changamoto nyingi sana,
Natambua Wananchi wengi bado ni masikini kama sio wenye kipato cha
chini sana, Natambua Wananchi wengi wanajishughulisha na Kilimo na Ufugaji
ingawa wapo Wachimbaji wadogo wa Madini na Wafanyabiashara pia lakini
natambua huduma za jamii pamoja na miundombinu ni changamoto kubwa sana”
“Tumekuwa Wilaya ya kuomba chakula cha msaada kila
mwaka, maambukizi ya Virusi vya Ukimwi VVU yanazidi kupanda, Elimu inazidi
kushuka, mapato ya Halmashauri yameshuka, wananchi wetu wamekuwa wakifuga
na kulima kilimo kile kile cha mazoea, huduma ya maji safi na salama
imeendelea kuwa changamoto kwetu, Vituo vya Afya na Zahanati havitoshelezi
mahitaji” Alisema Mtaturu
Kwenye Huduma ya Afya katika Vijiji 101 vilivyopo
Wilayani Ikungi kuna Zahanati 34, Vituo vya Afya 3 na Hospitali 2, kwa
uwiano huu zisipofanyika jitihada zaidi hali ya wananchi itakuwa mbaya
zaidi.
Hivyo Mkuu huyo wa Wilaya hiyo alisema kuwa Madiwani
wote wanatakiwa kuwa na mpango mkakati wa kuhakikisha huduma za Afya
zinapatikana kirahisi.
Katika hotuba yake Dc Mtaturu ameeleza kuwa
Ni lazima kwenye Kamati za Maendeleo za Kata (WDC) kuanzishwe mipango
ya kuhakikisha kunapunguzwa Vifo vya Wakinamama Wajawazito na Watoto
kwa kuweka mikakati itakayohakikisha Wananchi wote hawaendi umbali mrefu
kutafuta huduma za Afya.
“Katika suala hili la Afya ningependa kuzungumzia
mabadiliko katika Sekta ya Afya yanayoendelea hapa Nchini katika utoaji
wa huduma. Mabadiliko haya yana lengo la kuinua kiwango cha ubora wa
huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi na kuongeza kiwango cha uwajibikaji
kwa wasimamizi na watoaji wa huduma hizo. Ili kufanikisha lengo
hilo, madaraka, majukumu na kazi, rasilimali zaidi za afya zinahitajika
kwa kuitaka jamii kuchangia katika mifuko ya Afya ya Jamii (CHF)” Alisema Mtaturu
Katika Mfuko wa Afya (CHF) Kaya moja itatakiwa
kuchangia Tsh. 10,000/= na atatibiwa Baba, Mama na Watoto wanne kwa
mwaka mzima, hivyo Mwananchi akiuza kuku mmoja tu anatosha kumtibia
yeye mwenyewe na familia yake kwa mwaka mzima.
Mwananchi asipojiunga na huduma hii atatakiwa kutoa Papo kwa Papo
Tsh. 7,000/= pale anapougua hii elfu saba ni ya kumuona Daktari bila
dawa, Mwananchi huyu akiuguliwa na watu watano, itamlazimu kutoa Tsh.
35,000/= kwa hiyo Mwananchi ambaye hajajiunga na CHF atapata hasara
ya Tsh. 25,000/= na wakati mwingine anaweza akauguliwa akiwa hana hata
hela ya kutibiana hatimaye anahatarisha maisha ya watu wake wa karibu.
Dc Mtaturu amewataka Viongozi hao kujitafakari kwa nini waliomba
ridhaa ya kuwaongoza Wananchi wa Ikungi, kama waliomba nafasi hiyo kwa
ajili ya kuwatumikia Wananchi lakini kwenye Kata zao Shule za Sekondari
hazina Maabara, hakuna Zahanati na Kituo cha Afya, hakuna barabara,
hakuna huduma ya maji safi na salama na hakuna Shule; Wanafunzi wanatembea
umbali mrefu kufuata Shule na hawana mpango wowote ule wa kusogeza karibu
huduma hizi basi wanatakiwa kujitafakari upya.
Mkuu huyo wa Wilaya ameahidi kushirikiana na kila
Kiongozi bila kujali itikadi ya Chama chake, Dini yake au rangi yake
katika kuwaletea maendeleo Wananchi wa Ikungi.
Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya Madiwani wote
kwa hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mwenyekiti wa kamati ya huduma
za jamii ambaye ni Diwani wa Kata ya Issuna Steven Misai amesema kuwa
Hotuba ya Mkuu huyo inaonyesha taswira mpya ya kuinusuru Wilaya hiyo
katika sekta ya elimu, afya, na miundombinu.
Missai alisema kuwa maagizo ya hotuba yake yatafanyiwa
kazi na madiwani wote ili kuifanya wilaya ya Ikungi kuwa nguzo katika
sekta hizo hususani ujenzi wa maabara.
EmoticonEmoticon