Na Mwandishi wetu Boston
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, jana aliwasili Zanzibar akitokea Ughaibuni baada ya kukamilisha awamu ya pili ya ziara yake ya Mataifa mbalimbali Ulimwenguni.
Wazanzibari wakimsikiliza Maalim Seif (Picha na swahilivilla.Blog)
Katika awamu hiyo ya pili, Maalim Seif alitembelea Marekani na kupata nafasi ya kuzungumza na Wazanzibari katika jimbo la Massachusetts. Ifuatayo ni sehemu ya mwisho ya mfululizo wa makala zetu za "Maalim Seif azungumza na Wazanzibari Boston"
Akiwa mwishoni mwishoni mwa hotuba yake, Mwanasiasa huyo Mkongwe alikariri msimamo wa CUF wa kutoitambua serikali ya Zanzibar iliyoko madarakani kwa vile haikupata ridhaa ya wananchi, akisisitiza kuwa serikali hiyo pia haitambuliki Kimataifa.
"Hatuitambui serikali ya Dakta Shein, na hakuna taifa hata moja linaloitambua", alisisitiza.
Maalim Seif alielezea kwamba, wakati wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, wafanyazi wa serikali walikuwa wakipokea mishahara yao kwa wakati. Lakini matokeo ya serikali hiyo kugomewa na wanchi na kutengwa kimataifa, kumezidisha hali ya kiuchumi kuwa mbaya kiasi kwamba serikali inashindwa kuwalipa mishahara wafanyakazi wake kwa wakati.
"Tulifikia hatua nzuri, kiasi kwamba tarehe 22-23 watu walikuwa wameshapata mishahara yao. Sasa hali imezidi kuwa mbaya kiuchumi kiasi kwamba inafika mpaka tarehe 3 watu hawajalipwa", alisisitiza.
Kama Wahenga walivyosema: "Baada ya dhiki faraja", Maalim Seif naye aliwataka Wazanzibari kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha mpito, akiwahakikishia kuwa serikali iliyopo madarakani haitodumu.
".... Wananchi wavumiliye, na mwisho serikali hii itaondoka madarakani", alisihi, na kutamba: "Tutaendelea kufanya wajibu wetu na hatuchoki. Wala wasidhani kuwa tutarudi nyuma kwa kutukamata".
Aidha alikariri wito wake kwa jamii ya Kimataifa wa kuendelea kuibana serikali akisema: "Tunaiomba Jamii ya Kimataifa waendelee kuibana serikali........, na Inshallah itaondoka" alisema huku akijibiwa kwa akauli za "Amin"
Kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi. Kwa hivyo, kukhusu vitisho vilivyotolewa dhidi yake vya uwezekano wa kukamatwa, Maalim Seif aliyewahi kuwekwa gerezani kwa miaka kadhaa alisema kuwa kukamatwa kwake siyo mwisho wa harakati za Wazanzibari kudai haki yao, akisisitiza: "Kuna Maalim Seif zaidi ya mmoja" Aliongeza kwa kuwaonya viongozi wa Zanzibar dhidi ya kuchukuwa khatua kama hiyo kwa kusema: "....Washukuru sasa hivi kuna mtu ambaye angalau anaweza kusema na watu wakamsikiliza...."
Kukhusu suluhisho la mzozo wa sasa wa kisiasa Visiwani Zanzibar, Maalim Seif alitoa rai ya kuundwa kwa serikali ya mpito itakayosimamiwa na watu wanaoheshimika na ambao hawaelemei upande wowote wa kisiasa. Jukumu kubwa la serikali hiyo ya mpito litakuwa kufanya marekebisho ya sheria za uchaguzi visiwani humo: "Khaswa khaswa Tume ya Uchaguzi", aligogoteza.
Mahakama Ya Kimataifa:
Ni vizuri kukumbusha kuwa katika awamu yake hii ya pili ya ziara zake za Kimataifa, Maalim Seif na ujumbe aliofuatana nao walifika jijini The Hague, Uholanzi, na kufikisha malalamiko ya Wazanzibari.
Alipoulizwa iwapo khatua hiyo ina umuhimu wowote, khususan kwa vile viongozi wengi wa Kiafrika wamekuwa wakitoa wito wa kujitoa kwenye mkataba wa Kimataifa unaokhusiana na mahakama hiyo, Maalim Seif alisema: "Azimio lenyewe halikupita kwenye Mkutano wa Kilele wa Umoja Wa Afrika uliopita"
"Tumejidhatiti kikweli kweli kwa hili, kama wanadhani tunatania, wasubiri", alisistiza na kuongeza: "Tumepata Wakili mahiri, na anasubiri tumpatie vielelezo zaidi tu..., kwa hivyo tuko 'serious' kwa hili" Akijibu swali kukhusu kile kilichoandikwa na baadhi ya magazeti ya Tanzania kuwa Mahaka hiyo ya Uhalifu (ICC) imeitaka CUF kukanusha madai yake, msaidizi wa Maalim Seif aliyefuatana naye kwenye mkutano huo Bwana Issa Kheri Hussein, alitupilia mbali uzushi huo na kusema kuwa hiyo ni propaganda tu.
Aidha alisema kuwa hizo ni mbinu za kuitafuta CUF itoe maelezo kukhusu kile kinachoendelea The Hague kwa vile bado watu hawajui khaswa kinachoendelea na madai yaliyomo katika shauri hilo.
EmoticonEmoticon