Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kwa mara nyingine
limeipa nafasi Tanzania kwa kutoa kozi maalumu ya stamina (Physical
fitness) kwa makocha wa Tanzania wenye leseni kiwango B inayoanza leo
Agosti 22, 2016. Kozi hiyo inayoendeshwa na mkufunzi kutoka FIFA, Dk.
Praddit Dutta, raia wa India itafikia ukomo Ijumaa wiki hii.
Akifungua kozi hiyo, Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine
aliishukuru FIFA kwa namna inavyoipa nafasi Tanzania katika kozi
mbalimbali hususani za ukocha na uamuzi.
“Si kila nchi inapata privilege (fursa) kama hii. Bila shaka FIFA
inatambua uwezo wa makocha wa Tanzania kwa sasa. Mjue kuwa FIFA ina watu
wa kuwapa taarifa kila kona. Kama mngekuwa mnafanya vibaya, FIFA
wangesema Tanzania bado, kwa hiyo kozi zisipelekwe… lakini inaonekana
mnafanya vema, mngefanya vibaya msingefikiriwa,” alisema Mwesigwa
aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo.
Mwesigwa amesema kwa kuwa FIFA ina malengo chanya na Tanzania kwa
kutoa kozi mbalimbali ikiwamo hiyo ya physical fitness inayolenga kuwapa
ujuzi makocha hao kuwajengea uwezo wachezaji kuwa na stamina.
Hivyo akawataka makocha wanaohudhuria kozi hiyo kutumia fursa hiyo ya
mafunzo si kwa ajili yao peke yao bali kuendeleza ujuzi huo kwa wengine
ambao hawakubahatika kuwa sehemu ya wateule wa FIFA.
Naye, Mkufunzi wa kozi hiyo, Dk. Dutta alisema: “Bila shaka Tanzania
inakwenda kufungua ukurasa mwingine wa soka la weledi kwa kuwa na
wataalamu mbalimbali katika ukocha na uamuzi. Mnachotakiwa ni kujitahidi
kufanya vema na kozi nyingine nyingi zinakuja.”
FIFA kwa kushirikiana na Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), chini ya Mkurugenzi Salum Madadi, imepitisha
majina ya makocha 27 kuhudhuria kozi hiyo inayofanyika katika Hosteli ya
TFF iliyoko kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es
Salaam.
Makocha wanashiriki kozi hiyo ni Mohammed Muza, Samwel Moja, Nassa
Mohammed, Jemedari Said, Oscar Mirambo, Wane Mkisi, Cletus Mutauyawa,
Shaweji Nawanda, Kizito Mbano, Dennis Kitambi, Sebastian Nkoma, Fikiri
Mahiza, Nyamtimba Muga, Nassor Mwinchui, Alfred Itaeli, Henry Ngondo,
John Tamba, Kidao Wilfred, Luhaga Makunja, Mohammed Tajdin, Mohammed
Silima, Salum Ali Haji, James Joseph, Kessy Mziray, Daudi Sichinga,
Bakari Shime na Salum Mayanga.
EmoticonEmoticon