DIWANI WA CHADEMA ASWEKWA NDANI KWA KUKIUKA MAADHIMIO YA BARAZA LA MADIWANI WILANI IKUNGI

August 06, 2016
index
Kutoka Kushoto ni Eng Sadick Chakka Mhandisi wa Maji Wilaya ya Ikungi, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji jumanne Mtaturu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally J. Mwanga, na Kulia ni Abel Suri Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
…………………………………………………………………………………….
Na Mathias Canal, Singida
Jeshi la polisi Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida limemtia nguvuni Diwani wa Kata ya Iseke kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Emmanuely Njingu kwa kosa la kukwamisha shughuli za serikali kwa kuzuia watendaji wa serikali kufanya kazi yao ikiwemo ukusanyaji wa mapato.
Njingu ambaye alikuwa mjumbe wa kamati ya fedha awali kabla ya kuwekwa nguvuni na jeshi la polisi alivuliwa ujumbe wa kamati hiyo kutokana na kukiuka taratibu na makubaliano ya baraza la madiwani jambo ambalo limepelekea kuhamishiwa katika kamati nyingine.
Akitoa taarifa ya kukamatwa kwa diwani huyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambaye ni Diwani wa Kata ya Irisia Ally Juma Mwanga amesema kuwa Diwani huyo amekamatwa kwa mujibu wa sheria hivyo yeye kama mwenyekiti hawezi kuingilia taratibu, sheria,na kanuni za serikali.
Mwanga amesema kuwa tarehe 19 mwezi Julai moja ya maadhimio ya kamati ya fedha na vikao vya baraza ilikuwa ni kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri lakini diwani huyo amekiuka makubaliano hayo kwa kung’oa mageti ya vizuizi vya barabarani kwa ajili ya ukaguzi wa mazao jambo ambalo limepelekea kuzorota kwa ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri.
Ameongeza kuwa Mjumbe yeyote anayekiuka maazimio wanayokubaliana na kutoa siri za kamati adhabu yake kisheriani kupoteza sifa ya kuwa mjumbe wa kamati husika.
Amesema diwani huyo ameondoshwa katika nafasi hiyo baada ya maridhiano ya kamati hiyo na kukubaliana kumuhamishia katika kamati nyingine ya huduma za uchumi.
“Jambo mkishakubaliana kisheria tena kwenye vikao vya kisheria maana yake linakuwa ni sheria hivyo kwa kiongozi yeyote akikiuka taratibu za kisheria zinachukua mkondo wake, kanuni za Halmashauri ni za watu wote hazichagui upande mmoja” Alisema Mwanga
Hapo jana Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu alihutubia Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ikiwa ni mara yake ya mwanzo kabisa tangu alipochaguliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo ambapo pamoja na kuzungumzia kuwepo kwa changemoto ya uhaba wa maabara, afya duni na miundombinu pia alizungumzia kuhusu ukusanyaji hafifu wa mapato jambo ambalo linairudisha nyuma Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Bajeti ya Wilaya ya Ikungi kwa Mwaka 2013/2014 ilikuwa na Shilingi 509,701,044 namakusanyoyakeyakawa ni 338,325,000 ambapo hata hivyo mwaka ulimalizika kwa kuwa na upungufuwa shilingi 171,376,044.
Mwaka 2014/2015 ilipangwa bajeti ya shilingi 631,455,000 lakini makusanyo yake yakawa ni shilingi 457,555,172 ambapo mwaka ulimalizika kwa kukusanya 173,899,828.
Mwaka wa bajeti 2015/2016 bajeti ya Halmashauri iliyopangwa ilikuwa ni shilingi 1,127,030,000 makusanyo yalikuwa ni 679,283,000 ambapo hata hivyo mwaka ulimalizika kwa kwa kuwa na upungufu wa shilingi 450,747,000 hivyo kwa miaka mitatu Halmashauri hiyo imeshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji.
Mwanga amesema kuwa Kutofikiwa malengo hayo kumesababishwa na kutopewa ushirikiano watendaji katika ukusanyaji wa mapato hii ikiwa ni kufuatia kauli za mazuio zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa.
Hata hivyo ametoa Mwito kwa viongozi wa serikali, wanasiasa, taasisi za dini na wananchi kushirikiana kwa pamoja ili kufikia malengo ya kuifanya Ikungi kukua kiuchumi .

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »