Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akibonyeza king’ola kuashiria uwekaji jiwe la
msingi la Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma
Julai 302016. Kulia kwake ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Profesa Makame Mbarawa na kulia ni Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Jordan
Lugimbana. Kushoto ni Meya wa manispaa ya Dodoma, Jafari Mwanyembwa na
wapili kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Dodoma Adam Kimbisa.
Waziri
Mkuu,Kassim Majliwa akikagua upanizi na ukarabati wa uwanja wa ndege
wa Dodoma kabla ya kuweka jiwe la msingi mjini Dodoma Julai 20, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kuweka jiwe la misngi la
upanuzi na ukarabati wa uwanja wa ndege wa Dodoma mjini Dodoma Julai
20, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi
walioshiriki katika hafla ya kuweka jiwe la msingi la upanuzi na
ukarabati wa uwanja wa ndege wa Dodoma Julai 20, 2016. Kulia kwake ni
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na
kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Lugimbana.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………
Aweka jiwe la msingi upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma
Asema ahadi ya kujenga uwanja wa kimataifa Msalato iko pale pale
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Dodoma pamoja na
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kutenga eneo la bandari kavu
ili mkoa huo uweze kupokea na kuhifadhi mizigo na kurahisisha biashara
kwa mikoa jirani.
Ametoa agizo hilo leo jioni
(Jumatano, Julai 20, 2016) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mkoa
wa Dodoma mara baada ya kuweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa
awamu ya kwanza ya ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma.
“Ninazo taarifa kiwa Benki ya
Dunia kupitia shirika la Local Investment Climate (LIC) tayari wametenga
fedha kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kujenga bandari
kavu na tayari fedha hizo zimeshapokelewa na Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya
kazi hiyo.”
“Uzuri
wa mkoa wa Dodoma kuna reli. Kwa hiyo makontena yanayoenda Burundi na
mahali kwingine yatashushwa hapa na kukaa kwenye bandari kavu; hivyo,
wafanyabiashara watachukua mizigo yao hapa badala ya kupata shida ya
kuyafuata Dar es Salaam kama ilivyo sasa,” amesema.
Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano itoe wataalam ili washirikiane na CDA
kufanikisha kazi hiyo. Amesema hatua hiyo itasaidia kurahisisha wananchi
na wafanyabiashara kupata huduma hiyo kwa urahisi na umbali mfupi
tofauti na hali ilivyo sasa.
Ameuagiza pia uongozi wa CDA
utenge eneo maalum la kituo cha biashara (commercial hub)) ili Kanda
zote zinazozunguka mkoa wa Dodoma na nchi jirani wapate bidhaa
mbalimbali kutokea Dodoma. “Kutokana na upanuzi huu na fursa
zinazojitokeza, hii iende sambamba na kuwatengea maeneo maalum
wajasiriamali badala ya kuwaacha kuzagaa kila mahali,” amesisitiza
Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu upanuzi wa
uwanja huo, Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa mradi huo kutaziwezesha
ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 90 zianze kutua kwenye kiwanja hicho
na kukuza fursa za kibiashara zinazohitaji usafiri wa haraka na salama.
“Katika
Ilani ya CCM, suala la ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya viwanja
vya ndege limepewa umuhimu mkubwa sana na ndiyo maana leo tunashuhudia
utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais ambaye amewezesha upatikanaji wa
fedha za ukarabati na fidia kwa wananchi wa kata za Makole na Uwanja wa
Ndege ambao maeneo yao yametwaliwa na Serikali ili kufanikisha upanuzi
huu,” amesema.
Amesema
uzinduzi huo ni mwanzo tu wa utekelezaji wa miradi mingine ya kuboresha
na kupanua viwanja vya ndege nchini ambapo Serikali kwa kutumia vyanzo
vyake vya mapato ya ndani na ya nje, itaendelea kuboresha zaidi
miundombinu na huduma nyingine za viwanja vya ndege kama vile Mtwara na
Mwanza ambavyo amesema vitapanuliwa kufikia hadhi ya kimataifa.
Ameitaja
miradi mingine kuwa ni viwanja vya ndege vya Kigoma na Tabora ambavyo
vinaendelea kupanuliwa kwa kujenga majengo ya abiria na maegesho ya
ndege ili kufikia viwango vya huduma za kimkoa; viwanja vya Shinyanga na
Sumbawanga vitapanuliwa kwa kuboreshwa miundombinu na majengo yake
kufikia hadhi ya viwanja vya kimkoa; huku kiwanja cha ndege cha Lindi
kikiboreshwa miundombinu yake kufikia hadhi ya kimkoa na kuweza
kuhudumia viwanda vinavyotokana na uchumi wa mafuta na gesi.
Amesema
Serikali itaendelea kukamilisha ujenzi wa jengo la tatu la abiria
(Terminal 3) katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA) ambalo likishakamilika Desemba 2017 litahudumia abiria wapatao
milioni 6 kwa mwaka; ilhali kiwanja cha ndege cha kimataifa cha
Kilimanjaro (KIA) kinapanuliwa miundombinu yake na jengo la abiria ili
kiweze kuhudumia abiria milioni 1.2 kwa mwaka.
Akimkaribisha
Waziri Mkuu kuhutubia hadhara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa ameiomba Serikali iendelee kuwekeza
katika ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato ili ndege za kimataifa
ziweze kutua kwenye mkoa huo.
Mapema,
akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Dk. Leonard Chamuriho amesema Serikali imetoa
sh. bilioni 11.8 kwa ajili ya kazi hiyo na kwamba hadi sasa
wamekamilisha asilimia 60 ya ujenzi kwa kuweka lami umbali wa km.2.0
kati ya km.2.5 zinazohitaji kukamilishwa chini ya mradi huo.
Amesema
hivi sasa ndege zinazoweza kuruka na kutua kwa umbali huo zinaweza
kuanza kutoa huduma kwenye uwanja huo wakati wakiendelea kukamilisha
ujenzi wa mita 500 zilizobakia.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Eng. George Sambali alisema
ukarabati huo ulianza Juni 24, 2016 na imechukua siku 27 hadi sasa, kazi
ambayo alisema inawezesha kiwanja kutumika kwa ndege zenye uwezo wa
kubeba abiria hadi 90 na zenye mwendo wa kasi. Hata hivyo, alisema kazi
iliyobakia inatarajiwa kukamilika baada ya miezi miwili.
EmoticonEmoticon