Kocha
Mkuu wa timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles
Boniface Mkwasa Jumanne ya Julai 26, 2016 anatarajia kutangaza kikosi
kwa ajili ya kambi ya awali ya wiki moja ikiwa ni maandalizi ya kucheza
na Nigeria katika mchezo wa kukamilisha ratiba ya kuwania kucheza
fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Mkwasa
maarufu kama Masters amesema lengo la kambi hiyo itakayoanza Agosti
mosi, 2016 ni kuwaweka sawa kisaikolojia wachezaji kabla ya kuita kambi
nyingine rasmi wiki ya mwisho ya Agosti kujindaa na mchezo dhidi ya
Super Eagles ya Nigeria unaotarajiwa kuchezwa Lagos Septemba 2, mwaka
huu.
“Kikosi
change kitakuwa na vijana wengi, mimi ni muumini mkubwa soka la vijana
ambao baadhi niko nao na ambao nitawaita, lakini pia mara baada ya ligi
kuanza, nitaangalia wengine kabla ya kuwa na program ya ratiba ijayo ya
michuano mbalimbali ya kimataifa itakayotolewa na CAF na FIFA,” amesema
Mkwasa.
Taifa
Stars ilipangwa kundi G kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika (AFCON) ambazo zitafanyika Gabon, mwaka 2017. Timu nyingine
katika kundi hilo ni Nigeria, Chad na Misri ambayo tayari imefuzu baada
ya kukusanya pointi 10, Nigeria ina pointi mbili; Taifa Stars ina pointi
moja wakati Chad ilijitoa katikati ya mashindano na kukatisha ndoto za
Tanzania kucheza fainali hizo.
EmoticonEmoticon