Mbunge
wa Tarime Vijijini, John Heche (kushoto), akizungumza na wananchi
katika kijiji cha Matongo wilayani Tarime) wakati Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye koti la Bluu) alipofika
kijijini hapo ili kuwaeleza wananchi, maamuzi ya Serikali yanayotokana
na Mapendekezo ya Kamati iliyoundwa mwezi Februari mwaka huu ili
kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi
wanaozunguka mgodi huo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye koti la
Bluu) akizungumza na wananchi katika kijiji cha Matongo wilayani Tarime.
Profesa Muhongo alifika kijijini hapo ili kuwaeleza wananchi, maamuzi
ya Serikali yanayotokana na mapendekezo ya Kamati iliyoundwa mwezi
Februari mwaka huu ili kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia
NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Baadhi
ya wananchi katika kijiji cha Nyabichune wilayani Tarime, wakimsikiliza
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani)
aliyefika kijijini hapo ili kuwaeleza wananchi, maamuzi ya Serikali
yanayotokana na Mapendekezo ya Kamati iliyoundwa mwezi Februari mwaka
huu ili kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi
wanaozunguka mgodi huo.
Kaimu
Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje akisoma Ripoti kuhusu tathmini
ya Mgogoro kati ya mgodi wa Acacia North Mara na Wananchi wanaozunguka
mgodi huo. Ripoti hiyo aliisoma mbele ya Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo (mwenye koti la Bluu) aliyefika katika kijiji
cha Matongo ili kuwaeleza wananchi, maamuzi ya Serikali yanayotokana na
Mapendekezo ya Kamati iliyoundwa mwezi Februari mwaka huu ili
kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi
wanaozunguka mgodi huo.
Na Teresia Mhagama.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ametoa agizo la
kupimwa tena kwa maji yanayotoka katika vyanzo vinavyozunguka mgodi wa
dhahabu wa Acacia North Mara ili kujiridhisha kuwa hayana athari kwa
binadamu, mifugo na mazingira.
Agizo
hilo alilitoa wilayani Tarime wakati akizungumza na wananchi katika
vijiji vya Matongo, Nyabichune, Mrwambe na Nyakungulu ambavyo
vinazunguka mgodi huo wa dhahabu.
Profesa
Muhongo alitoa agizo hilo baada ya Kamati iliyokuwa ikitathmini
migogoro kati ya Mgodi huo na wananchi kueleza kuwa matokeo ya vipimo
vya maabara vinaonyesha kuwa maji hayo yana viwango vinavyokubalika kwa
matumizi ya binadamu, mifugo na mazingira na kupendekeza kuwa wataalam
wa afya na mifugo wafanye utafiti zaidi ya suala hilo ili kujiridhisha
zaidi.
“Viwango
vinavyopaswa kutumika katika upimaji wa maji haya lazima viwe vya
Shirika la Afya Duniani (WHO) hivyo zichukuliwe tena sampuli za maji
wakati wa kiangazi na wakati wa mvua na zipimwe tena. Sampuli hizo
zigaiwe kwa makundi mbalimbali ikiwemo wananchi, Mkuu wa wilaya, Kamati
iliyofanya tathmini na mimi mwenyewe ili kila kundi lipeleke katika
maabara inayoaminika na baadaye kuwasilisha majibu ya uchunguzi,”
alisema Profesa Muhongo.
Aidha
alisema kuwa sampuli za maji atakazopatiwa yeye atazipeleka katika nchi
mbalimbali duniani ikiwemo Ujerumani na Ubelgiji ambako kuna maabara
za kisasa na zinazoaminika duniani.
Aliongeza
kuwa, vyanzo vya maji katika sehemu nyingi zenye uchimbaji mkubwa na
mdogo duniani vimekuwa vikiathiriwa na shughuli za migodi na kueleza
kuwa atawasiliana na Mamlaka zinazosimamia Sekta ya Maji pamoja Mgodi
ili kupata chanzo mbadala cha maji na hivyo kuondoa malalamiko ya
wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Aidha
aliagiza wataalam wa Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha kuwa kila
baada ya miezi mitatu wanachukua sampuli za maji katika vyanzo
vinavyozunguka mgodi huo na kuzipima ili kujiridhisha kuwa maji hayo
hayana madhara kwa binadamu, mifugo na mazingira.
Naye
Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche alimshukuru Waziri wa Nishati na
Madini kwa kuamua kuishughulikia changamoto hiyo ya maji kwa kutoa agizo
kuwa upimaji wa maji hayo uwe endelevu na kutafuta chanzo mbadala cha
maji.
Aidha
Profesa Muhongo alitumia fursa hiyo kuwaasa Wachimbaji wadogo kujiunga
katika makundi ambayo yatawawezesha kufaidika na masuala mbalimbali
ikiwemo Ruzuku inayotolewa na Serikali ambapo kwa mwaka huu, takribani
Dola za Marekani milioni 400 zinatumika kuwaendeleza wachimbaji wadogo
kupitia Ruzuku hiyo.
EmoticonEmoticon