………………………………………………………………………………………………………
Na. Immaculate Makilika- Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema katika kipindi cha uongozi
wake atahakikisha Serikali inahamishia makazi yake mjini Dodoma.
Amesema hayo leo, wakati
alipokuwa akihutibia wajumbe wa Chama cha Mapinduzi(CCM) katika
Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama hicho uliofanyika mjini Dodoma mara
baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti.
“Nitahakikisha katika awamu ya
uongozi wangu, Serikali inahamia Dodoma, najua viongozi wengine wote nao
watanifata, kwa kuwa sasa miundombinu ya Dodoma inaweza kukidhi
mahitaji yote” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli aliendelea kusema
kuwa katika kipindi cha miezi nane ya uongozi wake chini ya Serikali ya
Awamu ya Tano ameweza kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa
kuanza kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Akiongelea maeneo ya utekelezaji
katika kipindi chake Dkt. Magufuli alisema kuwa mpaka sasa Serikali
imefanikiwa kusimamia suala la utoaji wa elimu bure kwa shule za Msingi
na Sekondari nchini na kuwezesha udahili kuongezeka zaidi tofauti na
miaka iliyopita.
Aidha Dkt. Magufuli alisema kuwa
Serikali yake pia imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika ukusanyaji wa
mapato ya serikali hali itakayosaidia kuimarisha utoaji wa huduma muhimu
za jamii.
Aidha, Serikali ya Awamu ya Tano imeagiza ndege mbili mpya zinazotarajiwa kuwasili nchini Septemba mwaka huu,
Rais Dkt. Magufuli aliongeza kuwa
Serikali yake kwa kushirikiana na Serikali ya Uganda wamefanikiwa
kujenga bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima katika ziwa Alberti
nchini Uganda kwenda bandari ya Tanga ambapo mafuta hayo yatasafirishwa
sehemu mbalimbali duniani na bombahilo litazalisha zaidi ya ajira
20,000.
Vile vile, Rais Magufuli alisema
kuwa Serikali yake imeweza kurudisha nidhamu ya kazi kwa watumishi wa
umma na kuweza kuondoa watumishi hewa waliokuwa na waliokuwa wamefikia
12,500,na kuongeza kuwa kwa mwaka huu Serikali imetenga fedha za
matumizi jumla ya shilingi trilioni 29.5, ambapo asilimia 40 ya fedha
hizo zitapelekwa katika kutekeleza shughuli za maendeleo.
Mkutano Mkuu Maalum wa CCM
ulihudhuriwa na wajumbe zaidi 2,000 ulimpitisha Rais Dkt. John Pombe
Magufuli kuwa mshindi na Mwenyekiti wa Chama hicho kwa kura 2398 kati
ya kura 2398 zilizopigwa ikiwa ni sawa na asilimia 100.
Rais Magufuli anakuwa Mwenyekiti
wa awamu ya Tano baada ya kupokea uongozi huo kutoka kwa Mwenyekiti wa
Chama hicho anayemaliza muda wake Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuongoza
chama hicho kwa kipindi cha miaka 10.
EmoticonEmoticon