MALINZI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA KESHI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Jamal Malinzi amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Kocha
Mkuu wa zamani wa Nigeria, Stephen Okechukwu Keshi (54) kilichotokea ghafla leo
Juni 08, 2016 kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa.
Kutokana na kifo hicho, Rais Malinzi ametuma salamu
za rambirambi kwa Rais wa Shirikisho la Soka Nigeria (NFF), Amaju Pinnick,
familia ya marehemu Keshi pamoja na ndugu, jamaa, marafiki walioguswa na msiba
huo wa gwiji huyo aliyepata kuwa nahodha wa kikosi cha Taifa Nigeria ‘Super
Eagles’.
Katika rambirambi ambazo zimefika pia katika Ofisi
za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu la
Kimataifa (FIFA), Rais Malinzi amesema kuwa japokuwa Keshi ametangulia mbele za
haki, mchango wake kwenye mpira wa miguu hautasahaulika kwani atabaki kuwa
alama ya maendeleo ya mchezo wa soka.
SERENGETI BOYS KAMBINI JUNI 13, 2016
Timu ya Taifa ya vijana
chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) inataingia kambini Juni 13, 2016 kujiandaa na
mchezo wa kufuzu fainali za kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya vijana
wenzao wa Shelisheli utakaofanyika Juni 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini
Dar es Salaam.
Mchezo wa marudiano kati
ya Serengeti Boys na Shelisheli utachezwa Julai 2, 2016 huko Shelisheli.
Katika kuajindaa na
mchezo huo, Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya
vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth
Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika
Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki.
Kadhalika Serengeti Boys
ilicheza mfululizo michezo saba ya
kimataifa bila kufungwa dhidi ya Misri (2), India, Korea Kusini, Malaysia na
Marekani (USA). Kabla ya hapo timu hiyo ilicheza michezo kadhaa ya ndani na
timu za chini ya umri wa miaka 20 bila kupoteza hata mchezo mmoja.
Katika mashindano ya
AIFF, timu hiyo pekee kutoka Afrika na ambayo ilikua kipenzi cha mashabiki
katika jiji la Goha ilicheza na timu ambazo ziko juu katika hatua za juu katika
mtoano wa kuwania kushiriki Kombe la Dunia kupitia mabara yao yaani CONCACAF
(USA) na AFC (India, Korea na Malaysia).
Haishangazi nchi nyingi
za Ulaya, Asia na Marekani zimeulizia uwezekano wa timu hii kutembelea nchi zao
kwa michezo ya kirafiki.
Awali timu ya Serengeti
Boys ilipewa nafasi ndogo ya kufanya vizuri kwa sababu ya rekodi zilizokuwa
zinaiweka Tanzania katika viwango vya chini katika umri huo kwa nchi za Afrika
Magharibi na Kaskazini zilikuwa juu zaidi na vilevile ukweli wa kwamba timu
kama USA, Korea, Malasyia na India zilikuwa na bajeti kubwa iliyogharamiwa na
Serikali zao na walikuwa na vifaa vya kila namna kiasi cha kuomba magari kwa
ajili ya vifaa vya mazoezi na mechi.
Serengeti Boys ilimaliza
Mashindano ya AIFF katika nafasi ya tatu kwa kuifunga Malaysia mabao 3-0. Serengeti
Boys na Bingwa Korea hawakupoteza mchezo hata mmoja na awali walipokutana
walitoka sare ya 2-2.
TFF YAANZA KUTOA FOMU ZA LESENI KWA KLABU
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeanza kutoa fomu za Leseni za Klabu (Club
Licensing) za Ligi ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na zile za Ligi Daraja la
Kwanza ya StarTimes.
Klabu
hizo zitatumiwa fomu hizo na kutakiwa kuzijaza na kuzirejesha kabla ya Juni 19,
mwaka huu ikiwa ni siku 10 mara baada ya Bodi ya Ligi ya TFF (TPLB) kuwatuamia
fomu hizo. Klabu itakayojaza fomu hizo kwa wakati ndiyo ambayo maombi yake ya
leseni yatashughulikiwa mapema.
Tayari
TFF imeteua Kamati ya Leseni ya Klabu (Club Licensing Committee) ambayo ndiyo
yenye jukumu la kupitia maombi ya leseni kwa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja
la Kwanza na kutoa uamuzi wa kuzikubali au kuzikataa kwa kuzingatia Kanuni ya
Leseni ya Klabu.
Wajumbe
walioteuliwa kwenye Kamati hiyo inayoundwa kwa mara ya kwanza ni Wakili Lloyd
Nchunga (Mwenyekiti), Wakili Emmanuel Matondo (Makamu Mwenyekiti), David
Kivembele, Hamisi Kissiwa na Prof. Mshindo Msolla.
Klabu
zinatakiwa kuchukua fomu za maombi TFF ambapo baada ya kuzirejesha zitafanyiwa
kazi ambapo zile zitakazokuwa zimekidhi matakwa ya Kanuni husika zitapatiwa
leseni husika ili zishiriki michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi Daraja la
Kwanza ya StarTimes kwa msimu wa 2016/2017.
Kwa
klabu ambazo zitashindwa kukidhi matakwa ya leseni yanayolenga kuhakikisha
mpira wa miguu unaendeshwa kwa weledi na kupiga vita upangaji matokeo katika
maeneo matano ya wachezaji (sporting), viwanja (infrastructure), utawala
(administrative and personnel), umiliki wa klabu (ownership) na fedha
(financial), hazitapa leseni hivyo kutokuwa na sifa ya kushiriki ligi.
Klabu
ambazo zitanyimwa leseni na kutoridhika na uamuzi huo, zitakuwa na fursa ya
kukata rufani kwenye Kamati ya Rufani ya Nidhamu ya TFF. Kwa mujibu wa Ibara ya
5(3) ya Kanuni ya Leseni ya Klabu ya TFF, Kamati hiyo ndiyo itakayosikiliza
rufani zinazopinga uamuzi wa Kamati ya Leseni ya TFF.