Mkurugenzi
wa Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Robert Kibona akiongea na waandishi wa habari
(hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa agizo la siku 60 kwa wadaiwa wa
Bodi hiyo na waajiri, ambapo takribani asilimia 72 ya wadaiwa wote
wameshawasilisha taarifa zao. Kulia ni Meneja Habari, Elimu na
Mawasiliano wa Bodi hiyo Omega Ngole.
Mkurugenzi
Msaidizi Habari, Elimu na Mawasiliano kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Cosmas Mwaisobwa (kushoto)
akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utaratibu wa
urejeshaji wa mikopo kwa wadaiwa ambao mikopo yao imeshaiva. Kulia ni
Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Robert Kibona kulia ni Meneja
Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi hiyo Omega Ngole.
Baadhi wa waandishi wa habari wakifuatiliaa mkutano huo.
PICHA NA FATMA SALUM-MAELEZO
………………………………………………………………………………………………………………
Na FATMA SALUM -MAELEZO
Jumla ya wadaiwa wapya 21,721 wa
mikopo ya elimu ya juu wamejitokeza ili kuanza kulipa madeni yao
kufuatia agizo la siku 60 lililotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu (HESLB) mnamo Machi 14 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa
Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) Bw. Robert Kibona wakati akizungumza na waandishi wa habari leo
jijini Dar es Salaam kuhusu tathmini ya agizo lililotolewa na bodi hiyo
kwa wanufaika wa mikopo na waajiri ili kutimiza wajibu wao kisheria.
Bw. Kibona alifafanua kuwa jumla
ya Shilingi bilioni 151.5 zinatarajiwa kurejeshwa na wadaiwa hao ambao
walikopeshwa ili kuwawezesha kupata elimu yao ya juu katika vyuo
mbalimbali ndani na nje ya nchi kuanzia mwaka 1994.
“Lengo la agizo lilikuwa ni
kuhahakisha madeni yote yaliyoiva yanakusanywa ili kuongeza uwezo wa
kukopesha watanzania wengi zaidi na agizo hili limeisha Mei 13 mwaka
huu.” alisema Bw. Kibona
Kwa mujibu wa Bw. Kibona, kati ya
wadaiwa waliopatikana, wadaiwa 19,528 walipatikana baada ya Bodi
kuchambua taarifa za waajiriwa zilizowasilishwa na waajiiri na wadaiwa
wengine wapatao 2,007 walijitokeza kwa hiari.
“Waajiri wana wajibu wa kisheria
wa kuwasilisha taarifa za waajiriwa wao, baadhi yao walifanya hivyo
katika siku hizo sitini na tukawabaini wadaiwa hao, tunawapongeza
waajiri kwa ushirikiano walioutoa na wanufaika wote waliojitokeza kwa
hiari” alisema Bw. Kibona.
Aidha Bw. Kibona aliongeza kuwa
Bodi imeongeza siku 30 za ziada kuanzia Mei 20, 2016 kwa wadaiwa
waliobaki kujitokeza na uamuzi huo umetokana na tathmini iliyoonyesha
kuwa kuna idadi kubwa ya waajiri na wanufaika wanaoendelea kujitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo Bw. Cosmas
Mwaisobwa alisema kuwa kiwango cha ukusanyaji wa madeni kwa mwezi
kinatarajiwa kuongezeka kutoka shilingi bilioni 2.7 zinazokusanywa hivi
sasa na kufikia shilingi bilioni 8 ifikapo mwezi Juni 2016.
Katika kipindi cha mwaka
1994/1995 hadi sasa, kiasi cha shilingi trilioni 2.44 kimetolewa kwa
wanufaika 378,504 wakiwemo wanafunzi wanaoendelea na masomo yao hivi
sasa ambao kwa sasa hawana wajibu wa kulipa hadi pale watakapomaliza au
kusitisha masomo yao.
EmoticonEmoticon