Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dioniz Malinzi
amewataka wachezaji wa timu ya soka ya vijana wa Tanzania wenye umri wa
chini ya miaka 17 maarufu kama jina la Serengeti Boys kwenda kucheza
soka la ushindani na kurudi na kikombe nyumbani katika mashindano
maalumu ya vijana yatakayofanyika Goa, India.
Dioniz Malinzi aliyasema hayo leo Mei 9, 2016 kwenye hafla ya
kukabidhi bendera timu ya Serengeti Boys inayokwenda Goa, India
kushiriki mashindano hayo maalumu ya soka ya kimataifa kwa vijana (AIFF
Youth Cup 2016 U-16) yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini humo
(AIFF).
Katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala
jijini Dar es Salaam, Dioniz Malinzi alisema: “Msiwe na wasiwasi, wakati
wenu wa kucheza soka ndiyo huu.”
“Waziri wa Michezo, Nape Nnauye ameniagiza niwaambie kwamba Serikali
itakuwa pamoja nanyi, hivyo msiwe na wasiwasi nendeni mkacheze. Mkacheze
mpira wetu si kuigaiga eti mcheze kama Misri. Kachezeni mpira wenu, huu
ndio wakati wenu wa kucheza mpira,” aliasa Malinzi.
Wito wa Malinzi ulipokelewa kwa mikono miwili na Nahodha wa timu
hiyo, Issa Makamba aliyetamba kurudi na taji hilo mwishoni mwa mwezi
mara baada ya mashindano yanayofikia kikomo Mei 26, mwaka huu.
“Tunamshukuru Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal
Malinzi kwa namna alivyojitahidi kutuhudumia hapa kambini. Tunaahidi
tutarudi na kombe hapa,” amesema Makamba na kuongeza kikosi chako kiko
vema kama alivyotangulia kusema Mshauri Mkuu wa Maendeleo kwa timu za
Taifa, Kim Poulsen.
Naye, Balozi wa India nchini, Sandeep Arya aliyeambatana na Naibu
Balozi, Robert Shetkintong balozi amesema amefarijika kuona Tanzania
imefanikiwa kupata nafasi hiyo kushiriki michuano hiyo maalumu kwa ajili
ya kuiandaa India na fainali zijazo za Kombe la Vijana.
“Tunachofanya kwa sasa ni kukuza ushirikiano kati ya India na
Tanzania katika michezo hasa soka. Kama tunavyofahamu soka kwa sasa ni
mchezo unapendwa na watu wengi. Unagusa watu wengi na India tumeliona
hilo hivyo kwa kuendeleza mchezo na uhusiano ndiyo maana tumekuwa na
program za maendelo ya mpira. Tutauendeleza na ninaamini vijana hawa
watakuwa chache ya kuuboresha mpira wetu,” amesema.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema kwamba tangu kuanza kwa maendeleo
ya soka la vijana, mashindano hayo yamekuwa ni hatua kubwa ya maendeleo
ya soka Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa haijawahi kutokea timu kama hiyo
ikateuliwa kushiriki michezo ya shirikisho kabla ya fainali za Kombe la
Dunia kwa vijana.“Kwa kawaida au tuseme kwa mujibu wa ratiba za fainali
kubwa zinazofanyika katika nchi fulani, mwaka mmoja kabla huandaliwa
mashindano ya shirikisho kama haya. India mwakani wana mashindano
makubwa, fainali za Kombe la Dunia kwa timu za vijana na hivyo ni
wameandaa mashindano ya shirikisho ambayo Tanzania, Malaysia, Korea
Kusini, Marekani na India wenyewe tumealiwa,” amesema na kuongeza kuwa
Serengeti Boys inatarajiwa kusafiri kwenda India Jumatano Mei 11, mwaka
huu.
Wachezaji wanaoondoka ni Ramadhan Kabwili, Kelvin Kayego,
Samwel Brazio, Kibwana Shomari, Nicson Kibabage, Israel Mwenda, Nickson
Job, Ally Msengi, Issa Makamba, Maulid Lembe, Ally Ng'anzi, Asad Juma,
Kelvin Naftari, Yasin Mohamed, Syprian Mwetesigwa, Aman Maziku, Rashid
Chambo, Enrick Nkosi, Yohana Mkomola, Mohamed Abdallah, Shaban Ada na
Muhsin Mkame.
Maofisa watakaosafiri na timu hiyo ni pamoja na Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji wa TFF, Ayoub Nyenzi, Mshauri wa ufundi wa timu za vijana, Kim
Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime, Kocha wa Makipa Mohamed Muharami,
Daktari wa timu, Shecky Mngazija na mtunza vifaa Edward Edward.
Michuano hiyo itakayopigwa kwa mfumo wa ligi kwa timu tano kucheza
mechi nne, inatarajiwa kuanza Alhamisi Mei 12, 2016 na kwamba AIFF
kimeandaa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, ikiwa ni
sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la
Dunia kwa Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka 2017.
Tayari Serengeti Boys imecheza michezo mitatu ya kirafiki ya
kimataifa mpaka sasa, mmoja dhidi ya Burundi na miwili dhidi ya timu ya
vijana wa Misri (The Pharaohs) na kupata matokeo mazuri na tangu Aprili,
2016 iliweka kambi katika hosteli za TFF zilizopo Karume kujiandaa na
michuano hiyo chini ya Shime, akisaidiwa na Sebastian Mkomwa.
Ratiba
Ratiba ya michuano inaonyesha kwamba Tanzania itafungua dimba na
Marekani kwenye Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa huku mchezo wa pili
ukiwa kati ya wenyeji India dhidi ya Malysia Mei 15, mwaka huu.
Serengeti Boys watashuka dimbani tena Mei 17, kucheza na wenyeji
India mchezo wa kwanza, Mei 19 Serengeti Boys watacheza dhidi ya Korea
Kusini na mchezo wa mwisho watamaliza dhidi ya Malysia Mei 21.
Fainali ya michuano hiyo itachezwa Mei 25 ambapo kabla ya mchezo wa
fainali, utchezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo Tilak
Maidan, Vasco, Goa.
Maana ya mashindano
Kupata nafasi ya kushiriki mashindano hayo maalumu ya vijana
kimataifa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi cha Serengeti Boys,
kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za vijana barani
Afrika dhidi ya Shelisheli Juni 25 hadi Julai 2, 2016.