Jeshi la Magereza limesaini Mkataba (MoU) na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Technoserve
– Tanzania kushirikiana katika ufundishaji wa wafungwa mafunzo ya
Ujasiriamali wakiwa wanakaribia kumaliza vifungo vyao magerezani ili
stadi hizo ziwasaidie kumudu maisha mapya baada ya kutumikia adhabu zao.
Programu hii itaendeshwa katika Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Mfuko wa “Master Card” kwa
vijana wa kike na kiume wenye umri kati ya miaka 18 hadi 30 hivyo
wafungwa walioko katika Magereza yaliyomo Mkoani humo na wengine wenye
sifa toka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ili kupata mafunzo kupitia
progamu ya uimarishaji wa maendeleo ya vijana vijijini kupitia biashara “STRYDE” inayoendeshwa na Taasisi hiyo.
Takwimu za sasa zinaonesha kwamba
kati ya asilimia 30 na 35 ya wafungwa wanaomaliza vifungo vyao hurejea
magerezani.Hivyo, mafunzo haya yatalenga kuwafanya wanapomaliza vifungo
vyao waweze kupata maarifa ya kuanzisha shughuli zao wenyewe za
kujipatia kipato halali na kuacha vitendo vya uhalifu katika jamii
wanamoishi vinavyowafanya kurejea magerezani.
Aidha, mafunzo haya ya
Ujasiriamali yatajikita katika kuwafundisha kilimo biashara, matumizi
mazuri ya fedha binafsi, uwezo wa kutumia ujuzi, ubunifu na tafakari ya
kina katika kufanya maamuzi, mpango biashara, mawazo ya biashara na
uwezo wa kuandaa mpango biashara n.k.
Ushirikiano huu ni mkakati
endelevu wa Jeshi la Magereza katika kuboresha Programu za Urekebishaji
wa wafungwa magerezani ili wawe raia wema na wenye tija katika jamii na
Taifa kwa ujumla.
Program za Ujasiriamali kwa wafungwa zinaendeshwa pia katika baadhi ya Magereza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Dorcas International na New Life in Christ katika Gereza la Karanga – ushonaji viatu, ufumaji na uokaji mikate, Gereza Arusha – uokaji mikate, ufundi seremala na ufumaji.
Jeshi la Magereza linawakaribisha
wadau wa ndani na nje kushirikiana katika urekebishaji wa tabia za
wafungwa ili wawe na michango chanya katika jamii na Taifa kwa ujumla.
EmoticonEmoticon