HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE KILELE CHA SIKUKUU YA
WAFANYAKAZI DUNIANI MEI MOSI 2016 ITAKAYOFANYIKA DODOMA
Mhe. Samia
Hassan, Makamu wa Rais;
Mhe. Kassim
Majaliwa, Waziri Mkuu;
Ndugu Gratian Mukoba,
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);
Mama Nortubunga
Maskini, Makamu wa Rais wa TUCTA;
Mheshimiwa
Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;
Mhe. Tulia Ackson, Naibu
Spika;
Balozi Injinia
John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;
Mheshimiwa
Jordan Rugimbana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa
Mawaziri wote, na Waheshimiwa
Wabunge mliopo;
Bi. Mary Kawar,
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Ofisi ya Nchi za Afrika
Mashariki;
Waheshimiwa
Mabalozi mliopo;
Waheshimiwa
Majaji,
Mheshimiwa
Almas Maige, Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania;
Dr. Aggrey
Mlimuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE);
Ndugu Nicholaus
Mgaya, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA);
Viongozi wa
Vyama vya Wafanyakazi;
Viongozi na
Maafisa wa Serikali mliopo;
Wawakilishi
wa Vyama vya Siasa mliopo; Mzee Mangula,
Makamu Mwenyekiti wa CCM
Bwana Kimbisa
(Mb), Mwenyekiti wa CCM Mkoa;
Wanahabari;
Mstahiki Meya
wa Manispaa ya Dodoma;
Ndugu Wananchi;
Ndugu Wafanyakazi;
Mabibi na
Mabwana.
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na afya njema na kuweza kukutana hapa.
Leo ni siku muhimu sana. Tupo hapa kwa ajili ya kuenzi na kuthamini
mchango wa wafanyakazi wa Tanzania, wake kwa waume, walioko sekta binafsi
na ya umma, na ambao kila siku tangu asubuhi hadi jioni wamekuwa wakivuja
jasho kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Hii si mara yangu ya kwanza nashiriki Sherehe ya
Siku ya Wafanyakazi, maarufu kama Mei Mosi. Nimeshiriki
kwenye sherehe hizi mara kadhaa. Lakini leo nashiriki kipekee kabisa.
Nashiriki kwa mara ya kwanza tangu nichaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba 2015. Hivyo, napenda kuchukua nafasi
hii kuwashukuru Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA)
na Vyama vyote vya Wafanyakazi nchini kwa kunialika ili nijumuike nanyi
kwenye Sherehe hizi za Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka huu. Aidha,
napenda kuwashukuru wafanyakazi wote wa Tanzania kwa kunipa kura nyingi
zilizoniwezesha kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi hii. Naahidi kwenu
kuwa sitawaangusha.
Nitumie fursa hii pia kuwapongeza sana wananchi wa
Mkoa Dodoma chini ya Uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Jordan Rugimbana
kwa kukubali kuwa wenyeji wa Sherehe hizi pamoja na maandalizi
mazuri mliyofanya kufanikisha sherehe hizi. Sherehe zimefana, hongereni
sana! Nawashukuru pia wananchi wa Dodoma kwa kunipa kura nyingi wakati
wa uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Aidha, ninawashukuru sana Wafanyakazi na Wananchi
wote mliojitokeza hapa leo kwa wingi ili kujiunga na wenzetu duniani
kote kusherehekea siku hii muhimu ya Wafanyakazi Duniani.
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi
kwa ujumla;
Duniani kote wafanyakazi ni nguzo muhimu ya maendeleo. Hakuna taifa lolote duniani
ambalo limeweza kuendelea bila kutegemea wafanyakazi wake. Hapa nchini,
wafanyakazi wametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa letu tangu
kipindi cha ukoloni hadi sasa. Bila shaka wengi wetu hapa tunafahamu
namna wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi vilivyoshiriki kikamilifu
katika harakati za ukombozi wa nchi yetu. Baada ya nchi yetu kupata
uhuru, wafanyakazi wameendelea kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya
nchi yetu.
Nitumie fursa hii kuwapongeza wafanyakazi kote nchini kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya kwa maendeleo
ya taifa letu. Ninyi ndio mmejenga miundombinu mbalimbali tunayoitumia
hivi sasa, ninyi ndio mnahakakikisha Watanzania wanapata huduma bora
za elimu na afya lakini hata ulinzi na usalama wa taifa letu kwa kiwango
kikubwa unategemea ninyi wafanyakazi. Hongereni sana wafanyakazi!
Ndugu Wafanyakazi
na Wananchi kwa ujumla;
Kama nilivyotangulia kusema, hii ni sherehe yangu ya kwanza
ya Mei Mosi tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu.
Hivyo, napenda kutumia fursa hii adimu kuzungumza na wafanyakazi pamoja
na wananchi kwa ujumla kuhusu masuala na mipango mbalimbali ambayo Serikali
ya Awamu ya Tano ninayoingoza imepanga kutekeleza katika kipindi cha
miaka mitano ijayo.
Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuona nchi yetu
inapata maendeleo kwa manufaa ya Watanzania wote. Tumejipanga kufanikisha
utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 pamoja na Ilani ya
Uchaguzi ya Chama Tawala. Sote tunafahamu kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo
inalenga kuiwezesha nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati unaongozwa na viwanda.
Ili kutekeleza Dira ya Maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala,
tayari tumekamilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
utakaotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/21.
Mpango huu unadhima ya kujenga uchumi wa viwanda
ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Lengo kuu la Mpango huu ni kuhakikisha rasilimali
na fursa za nchi zinatumika vizuri ili kujenga uchumi wa viwanda na
kupunguza umasikini. Baadhi ya malengo mahsusi ni kuimarisha kasi ya
ukuaji mpana wa uchumi kwa manufaa walio wengi, kuongeza kasi ya kupunguza
umaskini, kuongeza fursa ya ajira kwa wote, kuongeza upatikanaji na
ubora wa huduma za jamii na kuongeza mauzo nje kwa bidhaa za viwandani.
Ndugu Wafanyakazi
na Wananchi;
Baadhi ya masuala muhimu yaliyomo kwenye Mpango wa Maendeleo ambayo tutayatekeleza
katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni pamoja na kufufua viwanda na
kujenga vipya, hususan vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi
hapa nchini, teknolojia ya kati, nguvu kazi na ambavyo bidhaa zake zitatumika
zaidi hapa nchini, ikiwemo viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi. Aidha,
tunakusudia mazingira ya uzalishaji na uendeshaji biashara kwa kuhakikisha
tunajenga miundombinu ya nishati ya umeme, reli, barabara, maji, madaraja,
vivuko, bandari, viwanja vya ndege na TEHAMA. Tunalenga pia kuhakikisha
kuwa panakuwepo ardhi kwa ajili ya uwekezaji na upatikanaji wa rasilimali-watu
yenye ujuzi. Halikadhalika, tutaboresha sera, sheria, taratibu, uratibu
na ushirikiano wa kitaasisi.
Maendeleo ya uchumi ni lazima yaende sambamba na
maendeleo ya watu. Ili kuhakikisha hilo, vipaumbele vitakuwa ni kuhakikisha
watu wanaondokana na umaskini, njaa na ukosefu wa ajira. Aidha, tutaboresha
huduma za jamii, hususan afya na elimu, kwa kuhakikisha zinapatikana
kwa uhakika na ubora unaostahili. Tutahakikisha watu wengi wanajiunga
na mifuko ya hifadhi ya jamii na pia panakuwepo na usawa wa jinsia na
watu wenye ulemavu, utawala bora, mipango miji na kuogeza juhudi za
kukabiliana na athari za tabianchi.
Matumaini yetu ni kwamba utekelezaji wa Mpango huu
utaleta matokeo chanya kwa nchi yetu kwa kukuza uchumi kutoka asilimia 7 mwaka 2015 hadi asilimia 10 mwaka 2020;
kuongeza mapato ya yatokanayo na kodi kutoka asilimia 12.1 ya pato la
taifa mwaka 2014/15 hadi asilimia 17.1 mwaka 2020;
kuongezeka kwa kasi ya kupunguza umaskini ambapo pato la wastani kwa
kila mwananchi litaongezeka kutoka wastani wa dola za Marekani 1,006 mwaka 2015 hadi 1,500 mwaka 2020; umaskini
wa mahitaji ya msingi kupungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 16.7 mwaka 2020/21;
huduma za msingi za afya na elimu zitaimarika; kuongezeka kwa mauzo
nje ya nchi ya bidhaa za viwandani; kuongeza idadi ya watalii na kuongeza
uwekezaji wa moja kwa moja kutoka dola la kimarekani bilioni 2.14 mwaka 2014/15
hadi bilioni 5 mwaka 2021. Hayo
ndiyo malengo yetu.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu
Wananchi
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa utagharimu
takriban shilingi trilioni 107,
zikiwemo trilioni 59 kutoka Serikalini.Kwa
kuanza, kwenye bajeti ijayo, Serikali imetenga kiasi cha jumla ya shilingi trilioni 11.82 kwa ajili
ya bajeti ya maendeleo sawa na asilimia 40 ya bajeti yote
kutoka asilimia 26 mwaka uliopita.
Kati ya fedha za bajeti ya maendeleo, shilingi 8.702 trilioni sawa na asilimia 74 ya bajeti ni
fedha za ndani na fedha za nje ni shilingi 3.117 trilioni
sawa na asilimia 26.
Kama mnavyoona, sehemu kubwa ya ugharamiaji wa mpango
huu itafanyika kwa kutumia fedha za ndani. Hii ishara tosha kuwa tumedhamiria
kufanikisha azma yetu ya kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka
2025 ili kuleta maendeleo nchini mwetu na kuwaondolea wananchi kero
mbalimbali.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu
Wananchi;
Bila shaka baadhi yenu mtashangaa kwa nini nimetumia Sherehe hii ya Wafanyakazi kuongelea
malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitano
ijayo. Jibu ni moja tu. Imenilazimu kueleza hayo yote ili sisi wafanyakazi
wote hapa nchini tufahamu kazi kubwa iliyopo mbele yetu. Sisi ndio tunategemewa
kuwaongoza Watanzania katika kutekeleza na kufikia malengo ya Dira ya
Maendeleo ya Taifa 2025. Hivyo, tunaposherehekea sikukuu hii ya wafanyakazi
duniani hatuna budi kila mmoja wetu kujiuliza ni kwa namna gani tutachangia
katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango huu wa Maendeleo kwa nchi yetu.
Kwa kifupi, naweza kusema kuwa mipango yote mizuri niliyoieleza hapo
juu haiwezi kufanikiwa kama wafanyakazi hawatashiriki kikamilifu.
Hivyo basi, nitoe wito kwa wafanyakazi kote nchi
kila mmoja kwa nafasi yake kujipanga vizuri katika kutekeleza Mpango
huu. Ni lazima tufanye kazi kwa bidii na kujituma, ueledi mkubwa na
uadilifu. Nchi yetu haitaweza kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa kwa
viwanda kama tutaendelea kulea uvivu, uzembe, ubadhirifu, rushwa, ukwepaji
kodi, kutotimiza wajibu wetu na wafanyakazi hewa. Kwa kutambua
hilo, Serikali yenu imeanza kuchukua hatua za kuimarisha nidhamu na
uwajibikaji kwa watumishi Serikalini. Tayari tumeanza kuwashughulikia
watumishi wachache ambao ni wazembe, wavivu, wala rushwa, wabadhirifu
na wasio na maadili.
Nafahamu, watumishi wazembe na wabadhirifu ni wachache.
Lakini watumishi hao ndio wamekuwa wakiharibu sifa nzuri ya watumishi
wa umma. Hawa ndio wamekuwa wakirudisha nyuma gurudumu la maendeleo
la nchi yetu. Hawa ndio wamekuwa wakinufaika na kunyonya jasho la wafanyakazi
walio wengi wa Tanzania. Sasa mwisho wao umefika. Serikali ya Awamu
ya Tano imejipanga kuwashugulikia popote walipo. Hatutawaonea aibu au
huruma watumishi wa aina hii. Nimefurahi kusikia Vyama vya Wafanyakazi
viko pamoja na Serikali na havitaunga mkono mtumishi mzembe, legelege
na fisadi. Mmezidi kutupa nguvu zaidi ya kuendelea na jitihada tulizozianzisha
za kurejesha nidhamu ya kazi kwenye utumishi wa umma. Niwaombe pia tushirikiane
katika kushughulikia wafanyakazi hewa. Wafanyakazi hewa wameigharimu
Serikali fedha nyingi ambazo zingeweza kuboresha maslahi ya wafanyakazi
halali na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hadi leo idadi ya wafanyakazi hewa waliopatikana
ni 10,295. Kati ya wafanyakazi
hao 8,373 ni kutoka Serikali
za Mitaa na 1,922 ni wa Serikali Kuu.
Kutokana na wafanyakazi hao hewa Serikali imekuwa ikilipa kiasa cha shilingi 11,603,273,799.41
kila mwezi sawa na shilingi 139,239,285,592.92
kwa mwaka sawa na shilingi 696,196,427,964.6
kwa miaka mitano. Fedha hizi zingeweza kujenga barabara za juu (flyovers)
tano au kuboresha maslahi ya watumishi halali ama kuboresha huduma mbalimbali
za jamii. Aidha, nafasi hizo hewa zingeweza kutoa ajira kwa wahitimu
wa vyuo vikuu mbalimbali ambao wanatafuta kazi na hivyo kuleta manufaa
kwa taifa.
Ndugu Wafanyakazi;
Wakati nikitoa rai kwa watumishi legelege, wabadhirifu
na wala rushwa kubadilika, napenda pia kutumia fursa hii kuwapa moyo
wafanyakazi wote ambao ni wachapakazi na ambao wanatekeleza majukumu
yao kwa ueledi na uadilifu. Endeleeni kufanya kazi kwa kujiamini, kujituma
bila ya kuwa wasiwasi wowote. Nafahamu wapo baadhi ya watu wamekuwa
wakiwatisha na kuwaeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haijali wafanyakazi.
Wapuuzeni watu hao. Hao ndio wale waliokuwa wakinufaika au kushirikiana
na watumishi mafisadi, wala rushwa na wabadhirifu. Sasa wanatapatapa
baada ya kuona Serikali inachukua hatua mahsusi kwa watumishi wa namna
hiyo. Serikali ya Awamu ya Tano haitambuguzi mfanyakazi yeyote ambaye
anajituma na kufanya kazi kwa ueledi na uadilifu. Nipende kusema tu
Serikali yangu itawalinda na kuwatetea wafanyakazi waadilifu na wachapakazi.
Ndugu Wafanyakazi;
Wakati wa Kampeni na hata nikifungua Bunge niliwaahidi wafanyakazi wote wa umma na sekta binafsi
kuwa ningeboresha maslahi na mazingira yenu ya kufanya kazi, ikiwemo
kuongeza mishahara, kuwapatia vitendea kazi, pamoja na kulinda na haki
za msingi za hifadhi ya jamii kama huduma za afya na malipo ya pensheni
baada ya kustaafu kazi. Ahadi yangu hii bado ipo pale pale na nawaahidi
tena sitawaangusha. Kwa bahati nzuri hata kaulimbiu ya Mei Mosi mwaka
huu ambayo; “Dhana ya Mabadiliko Ilenge Kuinua
Hali ya Wafanyakazi” inasisitiza umuhimu wa kuboresha
maslahi na mazingira ya kazi ya wafanyakazi.
Kama alivyosema Katibu Mkuu wa TUCTA kuwa tangu tumeingia
madarakani, tumeweza kuongeza ukusanyaji wa mapato kutokana na kuziba
mianya mingi ya ukwepaji kodi na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima.
Hata hivyo, sio dhamira yetu na bila shaka sio dhamira ya Watanzania
walio wengi kuona fedha zote tunazokusanya tunazitumia kwa ajili ya
kulipia mishahara watumishi tu. Nasema hivi ili mfahamu kwamba mapato
haya yanawahitaji wengi sana. Wananchi walio wengi wamepata matumaini
kuwa kutokana na kuongeza kwa mapato sasa huduma mbalimbali zitapatikana
kwa ubora na uhakika. Hivyo, niwajibu wetu sisi mliotukabidhi kuongoza
Serikali kuhakikisha tunatumia vizuri rasilimali za nchi kwa manufaa
ya Watanzania wote. Na ninapenda kutumia fursa hii kuwahakikishia kuwa
tutaelekeza fedha tunazozipata katika maeneo muhimu ambayo yanamgusa
kila Mtanzania, wakiwemo wafanyakazi.
Ndugu Mwenyekiti
wa TUCTA;
Ndugu Katibu
Mkuu wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Hivi punde nimetoka kusikia risala yenu nzuri iliyosomwa na Katibu Mkuu wa TUCTA, Bwana Nicholas Mgaya. Sitaweza
kujibu hoja zote zilizotajwa kwenye risala yenu. Lakini napenda kuwahakikishia
kuwa Serikali imezipokea hoja zenu zote na tutazifanyia kazi. Hata hivyo,
naomba mniruhusu nieleze japo kwa uchache baadhi ya hoja mliyotaja kwenye
risala yenu:
Kwanza, kuhusu suala la kupunguza kodi ya mapato ya mshahara
(PAYE) kwa wafanyakazi. Napenda kuwaarifu kuwa Serikali yangu
kama nilivyoahidi wakati wa kampeni zangu nimeamua kuwapunguzia Wafanyakazi
kodi ya Mapato ya Mishahara kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 9 kuanzia mwaka
wa fedha wa 2016/17 kutegemea Wabunge watakavyopitisha bajeti yetu.
Tuna uhakika kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumewapunguzia wafanyakzi mzigo
mkubwa wa makato katika mishahara yao. Nimeamua kuanza na hili kwanza
ili changamoto zilizopo sasa za kiuchumi tuweze kuzivuka na baadaye
mambo yakiwa mazuri tutaangalia suala la kupandisha mishahara.
Pili, suala la tofauti ya mishahara. Tayari tumeanza kuchukua
hatua kuhakikisha tunakuwa na mfumo wa mishahara ambao unazingatia vigezo
vya uzito wa kazi na kupunguza tofauti kubwa ya malipo ya mshahara kwa
kuoanisha mishahara ya watumishi wa Umma walioajiriwa Serikali Kuu,
Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma. Tunataka Watumishi
wa Umma wafaidi matunda ya kazi kwa kuzingatia uzito wa kazi wanazozifanya
kwa misingi ya haki na usawa.
Aidha, kufuatia marekebisho ya Sheria ya Taasisi
za Kazi Na.7 ya Mwaka 2004, tumeunda Bodi mbili za mishahara. Bodi ya
mshahara katika Sekta Binafsi inayosimamiwa na Waziri mwenye dhamana
ya masuala ya Kazi na Ajira, na Bodi ya Mshahara katika Utumishi wa
Umma inayosimamiwa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma. Majukumu
ya Bodi hizi ni kufanya uchunguzi na kupendekeza kima cha chini cha
mshahara katika sekta husika. Ni matarajio yetu kwamba bodi hizi zitatekeleza
majukumu yake kwa weledi kwa kupendekeza viwango vinavyozingatia hali
halisi ya uzalishaji, tija na uchumi wetu. Nilikwisha tamka sitarajii
kuwa na mfanyakazi anayelipwa zaidi ya milioni 15 wakati wengine
wanalipwa laki tatu kwa mwezi.
Tatu, suala la hifadhi ya jamii. Serikali ya Awamu ya
tano inalenga katika kuhakikisha kwamba wananchi wengi zaidi watafaidika
na mfumo wa hifadhi ya Jamii nchini kuliko ilivyo sasa. Kwa mfano
tunataka wananchi wengi zaidi wajiunge na Bima ya Afya ili wawe na uhakika
wa matibabu. Tunaendelea na juhudi ya kupanua wigo wa Mfuko wa Bima
ya Afya vijijini (Community Health Fund) na pia kuwezesha wafanyakazi
wengi wa sekta binafsi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (National
Health Insurance Fund). Aidha, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeanza kusajili
wananchama toka sekta isiyo rasmi. Lengo la Serikali ni kuhakikisha
kwamba wananchi wengi wanapata huduma za msingi za hifadhi ya jamii.
Kwa upande wa kuimarisha Mifuko ya hifadhi ya jamii
pamoja nakuboresha malipo ya Pensheni, Serikali imekwishaelekeza Mifuko
ya Hifadhi ya jamii kuachana na uwekezaji kwenye miradi isiyokuwa na
tija. Wawekeze kwenye maeneo kama viwanda ili kuzalisha fursa za ajira
na kujipatia wanachama zaidi. Aidha, ushauri wenu wafanyakazi kupitia
shirikisho lenu la TUCTA kwa Serikali kuhusu kupunguza idadi ya Mifuko
ya Pensheni nchini na matumizi yasiyo ya lazima umepokelewa na kukubalika.
Lakini ni vyema mfahamu kwamba kutokana na historia tofauti ya kuanzishwa
kwa mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo sasa, hatua zozote za marekebisho
zinahitaji umakini mkubwa. Napenda niwahakikishie kwamba kazi ya kurekebisha
mifuko ya Pensheni nchi tutaikamilisha ndani ya mwaka 2016/2017.
Nne, suala la Vyama vya Wafanyakazi. Napenda kutoa rai
kwa waajiri kote nchini kutambua kwamba suala hili sio la hiari
bali ni wajibu wao kuwaruhusu wafanyakazi kuanzisha na kujiunga kwenye
vyama vya wafanyakazi sehemu za kazi bila ya kushurutishwa au kuchaguliwa
chama cha kujiunga. Hivyo, waajiri wote wanaovunja takwa hili la sheria
watachukuliwa hatua kali. Lakini pia nitoe wito kwenu Viongozi na wafanyakazi
vyama hivyo visitumike kuchocheo migogoro ya kikazi, uzembe na uvivu
kazini na wala visiwe vyama vya kisiasa kazini. Vyama hivyo vinapaswa
kutumika kuimarisha uhusiano kati ya waajiri na waajiriwa, kuhamasisha
utendaji kazi na kuleta utulivu sehemu za kazi.
Tano, suala la mikataba ya ajira. Waajiri wengi wamekuwa
hawatekelezi matakwa sheria kama yalivyobainishwa katika Sheria ya Ajira
na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 pamoja na marekebisho yake ambayo
tumeyafanya mwaka 2015. Bado yapo malalamiko mengi ya wafanyakazi
kutokuwa na mikataba ya kazi, kufanya kazi bila vifaa kinga, michango
ya pensheni kuchelewa kuwasilishwa au kutowasilishwa kabisa kwenye mifuko
ya hifadhi ya jamii. Serikali ya Awamu ya Tano ninayoongoza haitavumilia
ukiukwaji huu wa sheria.
Ili kuhakikisha waajiri wanatekeleza kwa hiari bila
shurti sheria za kazi, tuanza kurekebisha tena Sheri ya Ajira na mahusiano
kazini kwa kuanzisha adhabu za papo kwa papo ambapo waajiri watalazimika
kulipa faini kwa kila kosa la kutotekeleza sheria za kazi. Pia, katika
mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga fedha kuajiri maofisa kazi zaidi
wapatao 21 ili kuimarisha huduma za ukaguzi sehemu za kazi. Nitoe wito
kwa Vyama vya wafanyakazi, kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Waziri
Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu). Aidha, ninaziagiza Mamlaka
zinazohusika kusimamia utekelezaji wa Sheria za kazi kusimamia sheria
husika bila woga kwa lengo la kuwalinda wafanyakazi wasiendelee kutumikishwa
na kunyonywa.
Aidha, naziagiza mamlaka husika kushughulikia suala
la ajira za wageni ambazo zinaweza kufanywa na wazawa. Hakuna nchi yoyote
duniani ambayo jukumu lake kubwa ni kuwatafutia ajira wageni kazi ambazo
ingeweza kufanywa na wazawa. Naagiza Wizara zote zisimamie hili suala
kwa nguvu zote ili wazawa wapate ajira kwanza. Sambamba na hilo, wahusika
wote mshirikiane pia kuwafichua wale wote watakaofanya kazi bila vibali.
Nakumbuka zoezi hili lilianza sitaki kuamini kuwa ilikuwa ni nguvu za
soda. Mheshimiwa Waziri tafadhali simamia hili.
Suala jingine ambalo nalo limekuwa ni tatizo
sugu ni baadhi ya waajiri kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi
wao kwenye mifuko ya hifadhi kwa wakati. Ingawa wafanyakzi wamekuwa
wakikatwa kila mwezi lakini fedha hizo hazifiki kunakohusika. Tatizo
hili pia linaihusu Serikali kutokana na Hazina kutopeleka michango.
Hivyo, natoa wito kwa waajiri wote nchini kuwasilisha michango ya wafanyakazi
wao kila mwezi bila kukosa. Hivyo, natoa wito kwa waajiri wote nchini
kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kila mwezi bila kukosa.
Kwa upande wa Serikali tayari tumeanza kulishughulikia
suala hili la michango kwa kutambua wafanyakazi wote halali ili michango
yao iwasilishwe. Mathalan, kwenye Mfuko wa PSPF Serikali ilikuwa ikidaiwa
shilingi takriban bilioni 710 bilioni lakini hadi
sasa tumelipa takriban shilingi 500. Ni imani yangu kuwa michango ya
inayotakiwa kulipwa na Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi itapungua kutokana
na zoezi la kuwaondoa wafanyakazi hewa. Tunaomba Vyama vya Wafanyakazi
vishirikiane na Serikali kufichua watumishi hewa.
Ndugu Mwenyekiti
wa TUCTA;
Mheshimiwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu
Waheshimiwa Mawaziri
na Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Ndugu Katibu
Mkuu wa TUCTA;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wafanyakazi;
Mabibi na
Mabwana:
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwashukuru
tena Viongozi wa TUCTA na Vyama vya Wafanyakazi nchini kwa heshima mliyonipa
ya kushiriki kwenye Sherehe hizi. Aidha, napenda kurudia tena wito
wangu kwa Wafanyakazi na wananchi wote kwa ujumla, tuendelee kufanya
kazi kwa bidii, kwa nguvu zetu zote, kwa maarifa yetu yote na
kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji na uadilifu ili tuweze kusukuma
gurudumu la maendeleo ya nchi yenu. Tuachane na mazoea ya watu kuingia
kazini asubuhi na kuondoka saa nne.
Tukumbuke ya kuwa kazi ni utu, kazi sio fursa ya
kupata mshahara kwa manufaa ya familia zetu tu bali ni fursa nzuri ya
kutoa mchago kwa taifa lako kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mungu Wabariki Wafanyakazi Watanzania!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni kwa Kunisikiliza”.