Wachezaji wa timu ya Yanga
wakishangilia mara baada ya kufuga goli la pili katika mchezo wao wa
ligi kuu kati yao na timu ya Simba zote za jijini Dar es salaam kwenye
uwanja wa Taifa mjijini Dar es salaam, katika mchezo huo Yanga imeibuka
na magoli 2 huku simba ikiangikia pua kwa kutoka uwanjani bila goli.
Mchezaji wa timu ya Simba ya
jijini Dar es salaam akitapatapa kuutafuta mpira katikati ya wachezaji
wa Yanga wakati wa mchezo wao uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini
Dar es salaam.
Mashabiki wa timu ya Yanga
wakishangilia kwa nguvu mara baada ya timu yao kuibuka na ushindi mnono
wa magoli 2-1 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam leo.
……………………………………………………………………………………………………………………..
YANGA leo imeendeleza umwamba kwa
Simba katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baada ya kuinyuka kwa
mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo wa duru la kwanza
baina ya timu hizo kwenye uwanja huohuo Septemba mwaka jana, Yanga
ilishinda kwa idadi kama hiyo ya mabao.
Bao moja katika kila kipindi kama
ilivyokuwa mchezo wa Septemba yalitosha kuwapa furaha mashabiki wa
Yanga na kuanza kuimba nyimbo za furaha kuwasifu wachezaji wao.
“Nyama ya Simba halali kwa Yanga…
Yanga… nani kaua? Tambwe…Tambwe,” vilikuwa baadhi ya vibwagizo vya
mashabiki wa Yanga katika mchezo huo wa jana.
Yanga ilianza kuhesabu bao dakika
ya 37 mfungaji akiwa Donald Ngoma baada ya beki Hassan Ramadhan ‘Kessy
kurudisha mpira mfupi kwa kipa wake Vincent Angban na Ngoma kuuwahi na
kupachika bao.
Simba iliyoanza mchezo wa jana
kwa kasi kubwa na kuwapa matumaini mashabiki wake, ilijikuta muda mrefu
ikicheza pungufu baada ya beki wake Abdi Banda kuoneshwa kadi ya pili ya
njano iliyofuatiwa na nyekundu baada ya kumchezea madhambi Ngoma dakika
ya 23.
Awali dakika ya 20 mwamuzi
Jonensia Rukyaa wa Kagera alimpa kadi ya njano Banda baada ya kumchezea
vibaya Ngoma, lakini dakika chache baadaye beki huyo alirudia tena
kufanya madhambi na kupewa adhabu hiyo.
Dakika 15 za kwanza timu hizo
zilishambuliana kwa zamu, huku Simba ikifika mara nyingi golini ikiwa ni
pamoja na kupata kona za mara kwa mara, lakini umaliziaji ulikuwa butu.
Simba ilipoteza nafasi nzuri ya
kufunga dakika ya 16 wakati shuti la Jonas Mkude lilipookolewa na beki
Mbuyu Twite wakati mpira ulipokuwa ukielekea langoni huku mashabiki wa
Simba wakiwa tayari wameamka katika viti kushangilia.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga,
Amis Tambwe jana aliingia katika rekodi nyingine ya wachezaji waliopata
kucheza Simba na Yanga na kufunga mabao katika kila timu aliyocheza.
Tambwe aliifungia Yanga bao la
pili dakika ya 73 kutokana na pasi ya Godfrey Mwashiuya, bao ambalo
lilifanya mashabiki wa Simba kuanza kutoka uwanjani.
Hata hivyo bado Kiiza anaongoza katika ufungaji akiwa na mabao 16 akifuatiwa na Tambwe mwenye mabao 15 na Ngoma mwenye mabao 11.
Yanga ingeweza kuongeza idadi ya
mabao, lakini washamuliaji wake wakiongozwa na Tambwe, Ngoma na Msuva
walishika na papara za miguu kila walipokaribia lango la Simba.
Licha ya Simba kufungwa mabao
hayo ilionekana kuzindunduka dakika za mwisho na kufanya mashambulizi ya
kushtukiza, lakini bado suala la kutumbukiza mipira nyavuni lilikuwa
tatizo.
Kutokana na matokeo hayo Yanga
imefikisha pointi 46 na kushika uongozi wa ligi hiyo ikiiacha Simba
ikiporomoka hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 45, baada ya jana Azam
kuifunga Mbeya City mabao 3-0. Yanga ipo nyuma ya Simba kwa mchezo
mmoja.
Kipigo hicho ni cha kwanza kwa
Simba tangu iwe chini ya kocha Jackson Mayanja aliyerithi mikoba ya
Dylan Kerr aliyetimuliwa mwezi uliopita.
Mayanja ameiongoza Simba kushinda
mechi sita mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo jana ilikuwa
mara yake ya kwanza kucheza na Yanga akiwa kocha wa Simba.
Yanga: Ally Mustafa ‘Barthez’
Juma Abdul, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Mwinyi Hajji Mngwali, Pato
Ngonyani, Deus Kaseke/Godfrey Mwashiuya, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe
Donald Ngoma na Haruna Niyonzima/Simon Msuva.
Simba: Vicent Angban, Hassan
Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Abdi Banda, Justice
Majabvi, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto/Novaty Lufunga, Hamisi
Kiiza/Danny Lyanga, Ibrahim Ajib/Brian Majwega na Said Ndemla,
Naye Mwandishi Alexander Sanga
anaripoti kuwa timu ya JKT Ruvu na Stand United ya Shinyanga jana
zilifungana bao 1-1 katika mchezo wa ligi hiyo Uwanja wa Kambarage.
Stand ilikuwa ya kwanza kupata
bao dakika ya saba mfungaji akiwa Elias Maguli kwa shuti la mbali
lililomshinda kipa Shaaban Dihile.
JKT Ruvu inayoshika mkia katika
msimamo wa ligi ilisawazisha dakika ya 13 mfungaji akiwa Abdulrahman
Mussa baada ya makosa ya kipa wa Stand Frank Muwonge.
Nayo Toto Africans na Kagera
Sugar zilitoka sare ya bao 1-1 Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, ambapo Toto
Africans ilitangulia kufunga bao dakika ya 24 mfungaji akiwa Japhary
Vedastus.
Mfungaji alimalizia kazi nzuri ya Miraji Athumani kabla ya Kagera kusawazisha dakika ya 66 mfungaji akiwa Mbaraka Yusuph.
Nayo Azam FC ambayo ilifungwa
mchezo wake uliopita, ilizinduka jana Uwanja wa Sokoine Mbeya baada ya
kuifunga Mbeya City mabao 3-0 na hivyo kufikisha pointi 45 na kuchupa
hadi nafasi ya pili ikitoka ya tatu.
EmoticonEmoticon