Baadhi ya wenyeviti toka Halmashauri ya wilaya ya Kishapu wakimsikiliza mkufunzi (hayupo pichani) wakati wa mafunzo yao yaliyofanyika wilayani hapo.
“Unakuja
kwenye ofisi yangu na kutoa taarifa za ubadhirifu wa mtendaji wa kijiji.
Nakuuliza, je umechukua hatua zipi kama kiongozi wa kijiji kabla kuja kwenye
ofisi yangu? Unanijibu hapana, hii si sahihi,” Hayo ni maneno ya mkuu wa wilaya ya
Ngorongoro, Hashim Mgandilwa, aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wenyeviti wa vijiji, watendaji wa kata na
vijiji kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Loliondo.
Alisema
hayo kwa lengo la kufafanua dhana ya uwajibikaji kwa viongozi kama njia muhimu
ya kutatua kero zinazowakabili wananchi wa maeneo ya vijijini katika wilaya
yake. Ni dhahiri kwamba viongozi wa ngazi za vijiji na kata wanakabiliwa na
changamoto mbalimbali za kiutendaji katika maeneo husika. Kuna nafuu kwa watendaji wa kata na
vijiji, ambao ni waajiriwa wa serikali
na hupewa kazi kutokana na miongozo,
lakini siyo kwa wenyeviti wa vijiji na madiwani, wakati mwingine hata wabunge.
Akielezea
changamoto hiyo wakati wa mafunzo ya wenyeviti wa vijiji kupitia mradi wa
Chukua Hatua yaliyofanyika Septemba mwaka huu na shirika mdau la CABUIPA,
mwenyekiti wa kijiji cha Nyakafulu kilichopo wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita, Salum
Said amesema: “Baada ya kuchaguliwa kuwa
mwenyekiti wa kijiji hiki, hakika sikufahamu vya kutosha kuhusu majukumu yangu
mapya kama kiongozi. Na hii ni changamoto kubwa kwa wenyeviti wa vijiji karibu
vyote vya wilaya yetu.”
Yeye
ni mmoja kati ya wenyeviti 200 wanaopatiwa mafunzo katika mikoa ya Shinyanga,
Geita na Simiyu. Wakati
wananchi wakiwezeshwa kuwasimamia viongozi wao, viongozi hawakuwa wakiwezeshwa kutimiza
majukumu yao kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi wao. Hivyo kuna haja ya kutoa mafunzo kwa viongozi hao
ili waweze kutimiza majukumu yao kwa wananchi waliowachagua, ilikuwa lazima.
Wanakijiji wa Kijiji cha Uchunga wilayani Kishapu wakiendelea na mkutano pamoja na viongozi wa kijiji na wazee Maarufu
Akielezea
umuhimu wa kuwawezesha wenyeviti wa vijiji
wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wenyeviti na watendaji wa kata Julai
2015, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri
ya Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, Jane Mutagurwa alisema “Kwa muda
mrefu wenyeviti mmekuwa mkilalamika kusahaulika kwenye programu zetu za mafunzo,
fursa ndio hii imekuja. Tunafahamu kwamba wenyeviti wetu mnakutana na changamoto
nyingi za kiutendaji zinazotokana na uwelewa mdogo katika majukumu yenu, hasa kwa
wale wanaoingia madarakani kwa mara ya kwanza. Hivyo mtumie mafunzo haya
vizuri.”
Pamoja
na umuhimu wa mafunzo hayo kwa viongozi wa ngazi ya kijiji na kata, bado imekuwa ni changamoto
kubwa kwa serikali kuwawezesha wenyeviti kujua majukumu yao. Na hii inatokana
bajeti kuwa na vipaumbele vingine ambavyo halmashauri huwa wamejiwekea katika kutimiza majukumu yao."
Kwa
upande wa Ngorongoro, mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya hiyo mkoani Arusha
anaeleza:“Tangu tulipofanya uchaguzi mwaka jana hatujawahi kutoa mafunzo kwa
wenyeviti. Kwa hiyo tunaunga mkono mafunzo haya yanayotolewa na PALISEP
yatasaidia sana kwenye kuwawezesha viongozi hawa na watendaji wetu,” Kutokana na hali hii, wenyeviti wamekuwa na
changamoto za kuelewa mipaka ya majukumu yao, hivyo muda mwingine hujikuta kwenye
mzozo na watendaji wa vijiji vyao.
Mwenyekiti anawajibika kwa mwananchi aliyemchagua, wakati mtendaji
anawajibika kwa mkurugenzi aliyemwajiri. Kutokana na tofauti hizo, mafunzo ya
sasa ya wenyeviti na watendaji yanaendeshwa kwa pamoja kuwafanya waelewe mipaka
yao ya kiutendaji, hivyo kuboresha utendaji wao.
Afisa Programu wa CABUIPA, Michael
Ikila anafafanua: “Tunawafundisha vitu sita muhimu; taratibu za uendeshaji
serikali za mitaa, majukumu na haki za
wenyeviti wa vijiji, uwajibikaji na utawala bora, mamlaka za vijiji, masuala ya fedha, ikiwamo
uandaaji wa bajeti na mawasiliano mazuri
baina ya viongozi wa vijiji.” Mada hizi ni kwa mujibu wa mwongozo wa wizara
ya Tawala za Mikoa and Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Majukumu mengine ya wenyeviti hawa ni pamoja
na kuhamasisha shughuli za maendeleo,
utawala na kuhakikisha usalama wa watu
katika maeneo yao kwa kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji.
Kwa
upande wa Wilaya ya Ngorongoro, hii ni mara ya kwanza kwa wenyeviti kufundishwa
majukumu yao. Mwanzoni mafunzo haya yaliwalenga madiwani ambao kimsingi hawakuyapenda
kwa sababu ya kutokuwapo kwa posho. Hivyo mafunzo yao yakaamishiwa kwa
wenyeviti wa vijiji ambao walipokea mwaliko kwa furaha pasipo kudai posho. “Mafunzo
haya yatatusaidia kuboresha mahusiano na utendaji wetu. Mara kadhaa unakuta
wenyeviti wanaingilia mipaka yetu ya kazi, hivyo kuathiri uhamasishaji wa
shughuli za maendeleo. Na hii hutokea pale mwenyekiti mpya anapotaka
kuwaonyesha wapigakura wake kwamba mwenzake aliyepita hakufanya kazi,”
anaelezea mmoja wa watendaji wa kijiji aliyehudhuria mafunzo hayo.
Pamoja
na changamoto hizo, bado washiriki ambao ni wenyeviti, watendaji wa kata na
vijiji wamekiri kwamba mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kumaliza tofauti zinazojitokeza
baina yao. Lakini si hivyo tu, viongozi wa wilaya wameonyesha kuunga mkono
mafunzo hayo kwa kuwa yanasaidia kuhamasisha wananchi kutimiza majukumu yao. Lakini
pia viongozi hao walionyesha umuhimu wa kufikia wajumbe wengi zaidi ya
halmashauri za serikali ya kijiji. Kwa mfano, wakati akizungumza na wakufunzi
kwenye ofisi yake, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu, alisema: Halmashauri
ya Wilaya ya Kishapu ina jumla ya vijiji 117 vyenye wajumbe 2,925.
Katika mazingira hayo, mkurugenzi alitoa ombi maalumu la kusaidiwa
kuwawezesha wakufunzi 25 wa wilaya watakaotoa mafunzo kwa wajumbe wa
halmashauri za vijiji hivyo. Gharama za wakufunzi hawa kuwafikia wajumbe
wengine zitakuwa ni za serikali. Na huu
ni ushirikiano unaotakiwa baina ya sekta ya umma na binafsi kwa kuwa ni jukumu
letu sote kwa mustakabali wa maendeleo yetu.
Regards
Tone Multimedia Company Limited
Plot No.223/225 Block 46, Umoja Street
Kijitonyama P.O Box 32529 Dar es salaam Tanzania
Tel +255 22 2772919 Fax +255 22 2772892
E-Mail info@tonemg.com
Facebook: www.facebook.com/blogszamikoa
Web: www.tonemg.com
EmoticonEmoticon