K wa
mujibu wa Sheria ya Sikukuu za Kitaifa (The Public Holidays Act, Cap
35) pamoja na Sheria zingine zinazompa mamlaka Rais kutangaza siku
yoyote kuwa sikukuu au mapumziko, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameamua kuwa
maadhimisho ya Sherehe za Uhuru na Jamhuri zitakazofanyika tarehe 9
Desemba, 2015, yatumike kwa kufanya kazi. Kwamba maadhimisho ya Uhuru
ya mwaka huu (2015) yatatumika kama kichocheo cha kujenga tabia ya
kufanya kazi (Uhuru na Kazi) katika Taifa letu. Mheshimiwa Rais
ameelekeza Watanzania wote siku hiyo waitumie kwa kufanya kazi
mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini, sokoni, viwandani na usafi
wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi kwa vitendo.
Aidha, kwa kuwa Sherehe za Uhuru na Jamhuri huendana na
Maandalizi mbalimbali ambayo yanatumia fedha, kwa kuzingatia kuwa siku
hiyo itaadhimishwa kwa kufanya kazi, fedha zilizokuwa zimetengwa kwa
ajili ya sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli zingine za kijamii
ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia
dawa za hospitali, vitanda vya hospitali n.k. kadri kamati za maandalizi
zitakavyoamua.
Ieleweke kuwa sherehe za Uhuru
na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru wa nchi
yetu. Hivyo, sherehe hizi zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama
kawaida kuanzia mwaka 2016.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
23 Novemba, 2015
EmoticonEmoticon