Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya, Michael Mhando (meza kuu katikati) akizungumza na
waandishi wa habari kuhusiana na mikakati ya Mfuko huo ya ujenzi wa
Vituo vya mfano vya matibabu.
……………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu.
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unatarajia kuanza ujenzi
wa vituo vya matibabu vya mfano katika mikoa ya Mtwara na Kigoma katika
mwaka huu wa fedha wa 2015/2016.
Mikakati hiyo imesemwa na Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Michael Mhando wakati akizungumza na waandishi
wa habari Dar es Salaam jana kuhusiana na mikakati ya Mfuko katika
uboreshaji wa miundombinu ya Matibabu.
“Tunatarajia kuwanza ujenzi wa
Kituo cha matibabu cha mfano mkoani Mtwara na hasa kwa kuzingatia kuwa
Wizara yetu ya afya pia inao mpango wa kujenga Hospitali mkoani humo.
Tunawasiliana na Wizara ili tuunganishe nguvu zetu. Eneo tayari lipo na
Mfuko umetenga kiasi cha Tsh bilioni 3 kwa mwaka 2015/16, lakini pia
ujenzi Kituo cha Matibabu cha Mfano Mkoani Kigoma ambacho kitatoa huduma
kwa wanachama na wananchi wa mkoa huo na mikoa ya jirani,” alisema Bw.
Mhando.
Aidha Mfuko umejipanga kupunguza
msongamano wa wagonjwa katika Mkoa wa Dar es Salaam ambapo umeanza
kushirikiana na Uongozi wa mkoa ili kuziwezesha hospitali za Amana,
Mwananyamala na Temeke kuwa na vifaa vya kisasa zaidi ili kuhudumia
wanachama wengi kupitia huduma za matibabu na kliniki maalum
zitakazokuwa zinaendeshwa na madaktari bingwa wa hospitali hizo.
“Katika Jiji la Dar es Salaam
mfuko utajenga kituo cha madaktari bingwa (Doctors Plaza) katika eneo la
Ubungo Maziwa ambako mfuko utaweka pia miundo mbinu kwa ajili ya huduma
mbalimbali. Kituo hicho kitawawezesha wanachama na wananchi kupata
huduma za kuwaona madaktari bingwa wa fani mbalimbali kwa urahisi na
katika eneo moja, hali ambayo itapunguza msongamano wa wagonjwa katika
baadhi ya vituo na kuboresha huduma jijini.
Bw. Mhando alisema kuwa mbali na
juhudi za uboreshaji wa huduma za afya zilizotajwa hapo juu, Mfuko pia
umewekeza katika ujenzi wa Ofisi zake katika Mikoa ya Mbeya, Dodoma na
Tabora ambapo majengo hayo yatawezesha upatikanaji wa nafasi kwa huduma
za Hospitali za Doctors Plaza ambazo zimekuwa zikihudumia wanachama
wengi wa Mfuko.
EmoticonEmoticon