Timu ya Taifa ya Nigeria (Super Eagles) inatarajiwa kuwasili kesho
alhamis saa nne usiku kwenye uwanja wa JK Nyerere jijini Dar es salaam
kwa usafiri wa ndege binafsi tayari kwa mchezo dhidi ya Tanzania siku ya
jumamosi uwanja wa Taifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na
Mawasiliano cha Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Nigeria (NFF),
kupitia kwa Toyin Ibitoye msafara huo unatarajiwa kuwa na wachezaji 23
pamoja na viongozi wa benchi la ufundi linaloongozwa na kocha mkuu
Sunday Oliseh pamoja na viongozi wengine waandamizi wa shirikisho hilo.
Nigeria inatarajiwa kufanya mazoezi siku ya ijumaa saa 10 jioni
katika uwanja wa Taifa, ikiwa ni mazoezi mepesi ya kuelekea kwenye
mchezo huo.