*Asema Tanzania kuadhimisha miaka 100 ya Maskauti mwaka 2017
……………………………………………………………
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
amekutana na Waziri Mkuu wa Uganda, Dk. Ruhakana Rugunda na kufanya naye
mazungumzo kuhusiana na masuala mbalimbali yahusuyo nchi hizi mbili.
Akizungumza na mwenyeji wake jana
jioni (Alhamisi, Agosti 20, 2015), kwenye kikao kilichofanyika Ofisi ya
Waziri Mkuu wa Uganda jijini Kampala, Waziri Mkuu alisema amefurahishwa
na juhudi zinazofanywa kwenye mipaka ya nchi hizo mbili na hasa mpaka
wa Mutukula.
“Nimearifiwa kwamba juhudi za
ujenzi wa one-border-post pale Mtukula zinaendelea vizuri. Tunachotakiwa
kufanya kwa sasa ni kuangalia kwa kiasi gani tunaweza kutumia kituo
hiki kama fursa ya kukuza biashara baina ya nchi zetu mbili,” alisema.
Alisema masuala ya kuimarisha
uchumi ni ya msingi na hayana budi kupewa kipaumbele katika kipindi hiki
cha sasa. “Kikubwa ni kwa nchi zetu kuendelea kuimarisha amani iliyopo
kwa faida ya wananchi wake, maana bila amani hakuna kitakachofanyika,”
alisema.
Waziri Mkuu Pinda alitumia fursa
hiyo kumtakia heri yeye na wananchi wa Uganda wakati wakijiandaa kufanya
Uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Februari, 2016.
Pia alimwalika Waziri Mkuu wa Uganda aje kutembelea Tanzania pindi apatapo nafasi ya kufanya hivyo.
Naye Waziri Mkuu wa Uganda, Dk.
Rugunda alisema nchi yake bado inatambua na inathamini mchango wa
Tanzania katika kuleta amani nchini mwao.
“Tanzania itaendelea kukumbukwa
na Waganda kwa mchango mlioutoa katika harakati za kuikomboa Uganda
kutoka kwenye makucha ya Iddi Amin Dada. Maneno aliyokuwa akiyasema
mwalimu Nyerere bado yamo akilini mwetu na yanaendelea kuishi mioyoni
mwa Waganda wengi,” alisema.
“Waganda wengi wanaiona Tanzania
kama ni nyumba yao ya pili (second home) na wanafurahia wanapokuja huko
akiwemo Rais wetu, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni. Sote tunathamini
mchango wa Tanzania na tutaendelea kuuezi,” alisema Dk. Rugunda.
Alisema yeye binafsi anafurahi
kwamba Tanzania na Uganda zimeunganishwa kwa njia ya kieletroniki
(mtandao na mawasiliano ya simu); lakini akaongeza kuwa kiasili, nchi
hizo zimeunganishwa kwa njia ya barabara na maji kupitia Ziwa Victoria
na kwamba ana imani uhusiano uliopo utaendelea kudumu vizazi na vizazi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
amesema Tanzania itaadhimisha miaka 100 ya Chama cha Maskauti cha
Tanzania ifikapo Agosti, 2017. “Hivi sasa tunao maskauti wapatao 800,000
nchi nzima lakini lengo letu ni kufikisha maskauti milioni moja ifikapo
mwaka 2017 kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 100 nchini kwetu,”
alisema.
Waziri Mkuu Pinda aliwasili
nchini Uganda Jumatano usiku kwa ziara ya siku moja akimwakilisha Rais
Jakaya Kikwete kwenye maadhimisho ya miaka 100 ya Chama cha Maskauti cha
Uganda (Uganda Scouts Association – USA). Amerejea nchini jana usiku.
Rais Yoweri Museveni ndiye mlezi wa chama hicho na alikuwa amemwalika Rais Kikwete kwenye maadhimisho hayo.