MIDO’ MZIMBABWE AWASILI YANGA SC TAYARI KUSAINI MIAKA MIWILI

August 05, 2015


Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
NAHODHA wa FC Platinum ya Zimbabwe kiungo, Thabani Kamusoko (pichani) amewasili Dar es Salaam jioni hii kwa ajili ya kusaini Mkataba wa kujiunga na Yanga SC.
Kamusoko amepokewa na Meneja wa Yanga SC, Hafidh Saleh jioni hii Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na moja kwa moja kupelekwa kwenye kikao na viongozi.
Kamusako aliyewahi pia kuchezea Dyanamos FC ya Zimbabwe anatarajiwa kusaini Mkataba wa miwili Yanga SC.
Rasta huyo aliyeivutia Yanga SC ilipokutana na klabu yake, FC Platinum katika Kombe la Shirikisho mwanzoni mwa mwaka huu, anatarajiwa kuchukua nafasi ya Kpah Sherman aliyeuzwa Mpumalanga Black Aces ya Afrika Kusini.
Lakini pia, Yanga SC inafikiria kuwaacha wachezaji wake wengine wawili wa kigeni, beki Mghana Joseph Tetteh Zutah na kiungo Mbrazil, Andrey Coutinho.
Dirisha la usajili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara linatarajiwa kufungwa Saa 6:00 usiku wa kesho na kutakuwa na nafasi ya kusajili wa wachezaji huru tu kwa wiki moja ya mwisho kabla ya kuanza msimu mpya. 
Thabani Kamukoso (kushoto) akiwa na Meneja wa Yanga SC, Hafidh Saleh baada ya kuwasili JNIA

Baada ya Yanga SC kutolewa katika Robo Fainali michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame imekitathmini kikosi chake na kugundua Zuttah na Coutinho hawana faida.
Coutinho alijiunga na Yanga SC msimu uliopita akiletwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mbrazil mwenzake, Marcio Maximo na hadi sasa ameichezea timu hiyo mechi 33 na kuifungia mabao sita.
Mbrazil huyo alikuwa ana wakati mzuri chini ya kocha Maximo, lakini tangu ujio wa Mholanzi, Hans van der Pluijm amepoteza nafasi katika kikosi cha kwanza.
Zuttah amesajiliwa Juni mwaka huu kufuatia kupendekezwa na kocha Pluijm, lakini baada ya wiki mbili za Kombe la Kagame, uongozi umeona hana umuhimu.
Mbali na Sherman, Coutinho na Zuttah wachezaji wengine wa kigeni Yanga SC ni Mkongo, Mbuyu Twite, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma.
Yanga SC ilifungwa kwa penalti 5-3 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 katika Robo Fainali ya Kagame dhidi ya Azam FC wiki iliyopita na tathmini ya baada ya mashindano, inaonyesha timu inahitaji marekebisho madogo. 
Na kwa kuona uimara wa Azam FC iliyotwaa Kombe la Kagame mwishoni mwa wiki na namna wapinzani, Simba SC wanavyojiimarisha, Yanga SC imeona kuna umuhimu wa kuleta wachezaji wengine bora zaidi kuchukua nafasi za Coutinho na Zuttah.
Tayari wakala Mganda, Gibby Kalule aliyewahi kuwauzia Yanga SC Sherman amependekeza beki wa kimataifa wa Togo, Vincent Bossou mwenye umri wa miaka 29 anayechezea Goyang Hi FC ya Korea Kusini

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »