1.0 UTANGULIZI
1.1.0 Historia ya Jeshi la Magereza Tanzania Bara
Jeshi la Magereza lilianzishwa
rasmi mwezi Agosti 25, 1931, Dhima yake kuu ni kuchangia ipasavyo katika
kuimarisha usalama wa jamii kupitia usimamizi wa kifungo na huduma za
mahabusu, utekelezaji wa program za urekebishaji wa wahalifu na kutoa
ushauri wa kisera kuhusu uzuiaji wa wahalifu.
- Majukumu na malengo ya Jeshi la Magereza
Jukumu la msingi la Jeshi la
Magereza ni kuwahifadhi wafungwa na mahabusu wa aina zote na jukumu la
urekebishaji wa tabia za wafungwa pia hufanyika kupitia program za
mafunzo kwa njia ya vitendo katika miradi ya kilimo, viwanda vidogo
vidogo na ujenzi. Vile vile, ushauri nasaha hutolewa kwa wafungwa kwa
kutumia waalimu wa dini na maafisa ustawi wa jamii pale inabainika
kuhitajika kulingana na hali ya mfungwa husika.
2.0 MAFANIKIO
- Katika utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi cha Serikali ya awamu ya nne mwaka 2005 hadi 2015 Jeshi limepata mafanikio katika maeneo makuu kama yafuatayo:-
- Uimarishaji wa Magereza yenye Ulinzi Mkali (Central Prison)
Mfano ukarabati wa majengo na
uboreshaji wa miundo mbinu ya Magereza yenye ulinzi mkali umefanyika
katika Magereza ya Butimba, Uyui, Lilungu, Maweni, Isanga, Keko na
Ukonga.
- Ujenzi, ukamalishaji, upanuzi wa majengo ya Ofisi
Mfano, Ujenzi wa Ofisi za Wakuu
wa Magereza Mikoa ya Singida, Ofisi ya Magereza Mkoa wa Dar Es Salaam
unaendelea na ukarabati wa Jengo la Makao Makuu ya Magereza lililoanza
rasmi kutumika Desemba 31, 2007.
- Ujenzi wa nyumba za askari
Mfano, ghorofa la kuishi askari
takribani familia 16 mkoani Iringa, ujenzi wa nyumba za maofisa na
askari unaendelea kufanyika katika Magereza mbalimbali nchini.
- Maji safi na maji taka Magerezani
Uimarishaji wa miundombinu ya
maji safi umefanyika katika Magereza ya Kwamngumi, Kambi Kimbiji, Kikosi
Maalum (KMKGM), kambi Chikuyu, Segerea na sehemu zingine unaendelea
- Kupunguza Msongamano Magerezani
Jeshi la Magereza katika jitihada
za kupunguza msongamano Magerezani limefanikiwa kuongeza uwezo wa
magereza kutunza wahalifu kutoka nafasi 22,699 zilizokuwapo mwaka 2005
hadi nafasi ya 29,552 zilizopo sasa. Ongezeko hili la nafasi za kulala
wafungwa 6,853 ni sawa na asilimia 30.2 ya nafasi zilizokuwepo kabla
mwaka 2005.
- Kuimarisha Viwanda vidogo vidogo
Jeshi la Magereza limeendelea
kuimarisha Viwanda vidogo vidogo kwa kuendelea na ufungaji wa mashine
katika karakana ya Uhunzi Ukonga, kiwanda cha viatu Karanga Moshi,
nakadhalika.
- Kuimarisha Mashamba ya Kilimo na Mifugo
Jeshi la Magereza linahudumia
ng’ombe wa nyama, wa maziwa pamoja na Mbuzi, Kondoo, Nguruwe, Sungura,
Kuku wa mayai na Bata weupe. Aidha, Jeshi la Magereza lina mashamba ya
mbegu bora za kilimo kwa kushirikiana na Wakala wa Mbegu za Kilimo
nchini Agricultural Seed Agency (ASA) katika mikoa ya Arusha, Dodoma,
Manyara, Lindi, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro na Morogoro
- Matumizi ya Nishati mbadala Magerezani
Jeshi limeendelea na juhudi zake
za kupunguza matumizi ya kuni na badala yake kutumia nishati mbadala
kama vile gesi itokanayo na tungamotaka (Biogas) na Makaa ya mawe kwa
upikaji wa chakula cha wafungwa
- Mafunzo mbalimbali
Mafunzo mbalimbali yaliendeshwa
ndani ya Jeshi la Magereza na watumishi 7,683 walihitimu kozi
mbalimbali, kwa upande wa mafunzo katika vyuo vya nje ya Jeshi watumishi
519 wamehitimu masomo ya taaluma. Aidha, watumishi wa kada mbalimbali
wapatao 169 wamepata fursa ya kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo
mbalimbali au kushiriki kwenye vikao vya kimataifa.
- Usafirishaji Mahabusu
Jeshi limepanua utekelezaji wa
jukumu la kuwapeleka mahabusu Mahakamani kusikiliza kesi. Zoezi hilo
lilianza rasmi tarehe 19 Mei, 2008 kwa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Kwa sasa zoezi hilo linaendelea katika Mkoa wa Arusha na baadhi ya
Wilaya za Mkoa wa Dodoma.
- Utoaji wa Huduma za Afya
Kwa kushirikiana na Shirika la
PharmAccess International, New life in Christ na baadhi ya Halmashauri
hapa nchini tumefaninikiwa kujenga Zahanati na Vituo vya Afya katika
mikoa Ishirini (20).
- Kuwawezesha askari na watumishi kupambana na umaskini
Jeshi limeendelea na mchakato wa
kufungua Maduka ya Bidhaa zisizolipiwa kodi (Duty Free Shops) ili
kupunguza makali ya maisha kwa watumishi wa Jeshi la Magereza na familia
zao. Maduka ya aina hii yamefunguliwa Ukonga – Dar es Salaam, Gereza
Isanga – Dodoma, Gereza Karanga – Moshi, Chuo KPF – Morogoro, Gereza
Butimba – Mwanza, Gereza Ruanda – Mbeya, Gereza Keko na Gereza Uyui –
Tabora.
- Uhifadhi wa Mazingira
Hadi kufikia Aprili, 2015 miti
4,321,450 imepandwa nchi nzima na katika Miradi maalumu inayofadhiliwa
na mashirika mbalimbali kwa mfano UNDP/NORAD ikishirikiana na Wizara ya
Maliasili na Utalii Idara ya Tanzania Forestry Fund (TFF) katika
magereza ya Isupilo, Msalato, Idete, Mgagao, Kambi Mkwaya, Kambi Ihanga.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
DAR ES SALAAM
8 Julai, 2015
EmoticonEmoticon