Kikundi
cha Ngoma za Asili cha Simba kutoka Dodoma (kushoto) kikitumbuiza
mbele ya Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia
katikati, aliyevaa koti la kahawia) kabla ya uzinduzi wa huduma za
leseni kwa njia ya mtandao uliofanyika mjini Dodoma.
Kamishna
Msaidizi wa Madini- Kitengo cha Leseni, Mhandisi John Nayopa (Kulia)
akielezea mfumo wa huduma za leseni kwa njia ya mtandao unavyofanya
kazi kabla ya kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Nishati na Madini, George
Simbachawene (wa pili kutoka kushoto, aliyekaa meza kuu).
Kamishna
wa Madini Nchini, Mhandisi Paul Masanja (Kulia) akielezea mafanikio
katika uboreshaji wa huduma za utoaji leseni kwenye uzinduzi huo.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia) akisoma hotuba ya uzinduzi wa huduma za leseni kwa njia ya mtandao.
Waziri
wa Nishati na Madini, George Simbachawene (katikati) akibonyeza kitufe
kuashiria uzinduzi wa huduma za leseni kwa njia ya mtandao. Wa pili
kutoka kulia ni Kamishna wa Madini Nchini, Mhandisi Paul Masanja na wa
kwanza kushoto mbele ni Kamishna Msaidizi wa Madini- Kitengo cha
Leseni, Mhandisi John Nayopa.
Waziri
wa Nishati na Madini, George Simbachawene (wa nne kutoka kulia,
waliokaa mbele); Kamishna wa Madini Nchini Mhandisi Paul Masanja ( wa
tano kutoka kulia, waliokaa mbele) na Kamishna Msaidizi wa Madini-
Kitengo cha Leseni, Mhandisi John Nayopa ( wa pili kutoka kushoto,
waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Wizara ya
Nishati na Madini waliohudhuria uzinduzi huo.
…………………………………………………………………
Greyson Mwase na Samuel Mtuwa, Dodoma
Wizara ya Nishati na Madini
imezindua mtandao utakaowezesha wachimbaji wa madini kutuma maombi ikiwa
ni pamoja na kufanya malipo ya leseni za madini unaojulikana kwa jina
la Online Mining Cadastre Transactional Portal (OMCTP).
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mtandao huo iliyofanyika
mjini Dodoma, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema
kuwa lengo la mtandao huo ni kuwezesha shughuli za uchimbaji madini
kufanyika katika uwazi na kukomesha rushwa.
Akielezea hatua mbalimbali katika uboreshaji wa huduma za leseni
zilizopitiwa na Wizara Simbachawene alisema mwaka 1990 leseni
zilishughulikiwa kwa njia ya mkono hadi kufikia mwaka 2005 ambapo Wizara
ilianzisha mfumo wa kompyuta katika utoaji wa leseni uliojulikana kwa
jina la MapInfo ambao bado ulitegemea uchambuzi kwa njia ya mkono.
Alisema ili kuboresha huduma ya utoaji wa leseni za madini,
mwaka 2007 Wizara ilianzisha mfumo wa utoaji wa leseni za madini
uliojulikana kama Mining Cadastral Information Management System (MCIMS)
ambao uliwezesha ofisi za madini kuunganishwa kwa njia ya mtandao na
kuwezesha uchambuzi wa maombi ya leseni kufanyika kwa njia ya kompyuta.
Alisema mfumo huo ulirahisisha sana upokeaji na uchambuzi wa maombi ya leseni na kurahisisha usimamizi wa leseni za madini.
Aliendelea kusema kuwa kupitia mfumo huo Wizara imeweza kupokea
na kuchambua wastani wa maombi 1,400 ya leseni kubwa na 5,000 ya
uchimbaji mdogo kwa mwaka.
Alisema mfumo huo umewezesha utolewaji wa wastani wa leseni 500
kubwa za madini na leseni zipatazo 1,500 za uchimbaji mdogo kila mwaka.
Waziri Simbachawene aliendelea kusema kuwa kuanzia mwaka 2010
Wizara iliendelea kuboresha mfumo wa flexicadastre chini ya Mradi wa
Usimamizi Endelevu wa Rasilimali ya Madini (SMMRP) unaofadhiliwa na
Benki ya Dunia.
Alisisitiza kuwa maboresho hayo yalikuwa ni pamoja na kuwezesha
uondoaji wa mlundikano wa maombi ya leseni, kuhuisha takwimu za leseni
za madini na pia kuweka tovuti maalumu iliyowezesha wananchi kupata
taarifa ya leseni za madini, maboresho yaliyochochea ari ya wananchi
kufuatilia masuala ya leseni kwa njia ya mtandao, na kuweka uwazi katika
usimamizi wa sekta ya madini kwa mujibu wa Mpango wa Kuongeza Uwazi na
Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji Nchini (TEITI)
Aliongeza kuwa kufikia Mei, 2015 jumla ya leseni 3,500 za
utafutaji mkubwa wa madini, leseni 14 za uchimbaji mkubwa wa madini,
leseni 389 za uchimbaji wa kati na leseni 39, 921 za uchimbaji mdogo wa
madini zilitolewa.
Alisisitiza kuwa kwa sasa Wizara imeamua kuboresha huduma za
leseni za madini kwa njia ya mtandao kama utekelezaji wa agizo la
serikali la kuhakikisha kuwa malipo ya serikali yanafanyika kwa njia ya
kielektroniki.
Simbachawene aliongeza kuwa mfumo huo mpya utawawezesha wateja
waliosajiliwa kutuma maombi, kuhakiki taarifa za leseni wanazomiliki,
kutuma taarifa za utendaji kazi na kufanya malipo ya leseni na mrabaha
kwa njia ya kielektroniki.
Alisema mfumo huu pia utawawezesha wateja kuoanisha ramani za
maeneo ya leseni na ramani za kijiolojia zilizoandaliwa na Wakala wa
Jiolojia Tanzania (GST)
Aidha, Waziri Simbachawene aliwataka wamiliki wa leseni na
wananchi wote kwa ujumla kujisajili katika mfumo huo kwa kuwa lengo la
Wizara ni kuhakikisha kuwa huduma zote za leseni zinakuwa kwa njia ya
kielektroniki ifikapo Agosti 31, mwaka huu.
Pia aliwataka makamishna wa madini pamoja na watendaji wake
kuhakikisha kuwa wanaweka utaratibu mzuri wa kuwasajili wachimbaji
wadogo ili nao waweze kutumia huduma hizo la kielektroniki bila kikwazo.
Wakati huo huo akielezea faida za mfumo huo, Kamishna wa Madini
Nchini Mhandisi Paul Masanja alisema kuwa mfumo huu unawawezesha wateja
waliosajiliwa kutuma maombi, kuhakiki taarifa za leseni wanazomiliki,
kutuma taarifa za utendaji kazi, kupata historia ya leseni zao, kuhuisha
leseni zao, kuongeza ukubwa wa maeneo ya leseni zao na kufanya malipo
ya leseni na mrabaha kwa njia ya kielektroniki.
Mhandisi Masanja aliongeza kuwa mfumo huu utawawezesha wamiliki
wa leseni kuwa na usimamizi wa leseni zao kwani utakuwa ukimjulisha
mmiliki wa leseni lini leseni yake inatakiwa kulipiwa na lini leseni
yake itaisha
“Mfumo huu pia umesheheni takwimu mbalimbali za madini ikiwa ni
pamoja na ramani za maeneo ya leseni na ramani za kijiolojia
zilizoandaliwa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST)” Alisema Mhandisi
Masanja
Aliongeza kuwa, mfumo huu utawapunguzia mzigo watalam wa Wizara
kwa kuwa wateja wenyewe wataingiza maombi ya leseni na hivyo wataalam
kufanya uchambuzi kwa haraka zaidi na kupata muda wa kutosha kusimamia
leseni zilizopo.
Alisisitiza kuwa mfumo huu umelenga kuondoa upotevu wa fedha za
serikali kutokana na vitendo vya rushwa na makosa mengine ya kibinadamu.
Akielezea hatua iliyofikiwa ya usajili wa wateja katika mfumo
huo, Mhandisi Masanja alisema tangu kuanzishwa kwa mfumo huo mwaka 2013
hadi sasa ni wateja 140 tu kati ya wateja wapatao 400 wamesajiliwa na
wachimbaji wadogo 20 kati ya wamiliki wapatao 4,000 wamesajiliwa katika
mfumo huo na kuwataka wadau wote waone umuhimu wa kujisajili na kutumia
huduma hizi ili kuondoa matatizo ya ucheleweshaji wa kushughulikia
maombi yao.
Mhandisi Masanja aliongeza kuwa kuanza kutumika kwa mfumo huu
kunaiweka nchi ya Tanzania katika nchi chache za Afrika zilizo na mfumo
wa kisasa wa huduma za leseni kwa njia ya mtandao.