SERIKALI imesisitiza mpango wa
ujenzi wa Bandari mpya ya Mwambani mkoani Tanga si kutokana na kuwepo kwa kina
kirefu tu cha maji bali kuhakikisha kuwa inatumika kuwa kichocheo cha madaliko
ya kiuchumi ndani ya mkoa huo kwa kuongeza Shehena za
mizigo za ndani na nje ya nchi kutoka tani milioni moja za sasa hadi tani milioni 15 kwa mwaka.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa
Uchukuzi Samuel Sitta wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya usimamizi
wa Bandari(TPA)mkoani Tanga kufuatia ziara yake ya kikazi ya kukagua Bandari
hiyo na eneo linalotakiwa kujengwa Bandari mpya ya Mwambani.
Sitta alisema mradi huo wa Bandari
mpya ya Mwambani unaenda sambamba na ujenzi wa miundo mbinu ya Barabara kutoka
Pangani,Bagamoyo hadi Dar es Salaam pamoja na njia ya reli ya kutoka Tanga
Arusha,Musoma mpaka Ziwa Victoria kuelekea Uganda.
Alisema tayari serikali
imeshaliagiza Shirika la Rahco ili kuwa na kituo kikubwa cha kuegeuzia treni na
mabehewa, na kwamba mchakato wa ujenzi
wa njia hiyo ya reli kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gage) yenye spidi 100 ambayo inabeba kontena zaidi
ya mbili kwa mtindo wa ghorofa mradi unatarajiwa kukamilika katika
kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa.
“Rais Museven wa Uganda alitoa rai
kwa Rais Jakaya Kikwete kujenga reli itakayokwamua uchumi wa Uganda na
ukitazama ramani ya Afrika hususan Afrika Mashariki Bandari ya Tanga ndiyo njia
fupi karibu kabisa kwa kuweza kusafirisha bidhaa za Jamhuri ya Uganda”,alisema
Waziri huyo.
Sitta alisema fursa hiyo inachangiwa pia na ugunduzi wa madini aina ya Red Nicol katika mkoa wa Simiyu eneo la
Dutwa pamoja na Soda Arsh katika Ziwa Natron
rasilimali ambazo zote zinatafutwa Duniani na zitasafirishwa kwa njia ya
reli kupitia Tanga kuelekea kwenye soko la Kimataifa.
Kwa mujibu wa Kiongozi huyo ni
kwamba mradi huo wa njia ya reli unatarajiwa kugharimu zaidi ya dola Bilioni 4
sawa na shilingi za kitanzania takriban Trilioni 8 na unatarajiwa kufanyika
chini ya Mkandarasi wa Kampuni ya China Engineering Company ambaye atajenga kwa
gharama zake mwenyewe.
“Kwa hali hii nakuja kwenu watumishi
wa Bandari ya Tanga msijiinamie inamie kufikiria hatma zenu hatma ya bandari
Tanga ni nzuri sana na itabidi kuongeza na watumishi zaidi kwa sababu mtatoka
kwenye kiwango cha chini ya tani milioni moja kwenda kwenye tani milioni 15 kwa
kipindi cha miaka 10 ijayo”,alisisitiza.
Kufuatia hatua hiyo aliiagiza
Halmashauri ya Jiji la Tanga kuhakikisha inajiandaa na mikakati hiyo katika
suala zima la upanuzi wa maeneo yake ili na kutumia fursa hiyo kwa mabadiliko ya
kiuchumi na maendeleo ya wakazi wa mkoa huo kwa jumla.
Awali akizungumza katika kikao hicho
Meneja wa TPA mkoa wa Tanga Henry Arika aliishukuru serikali kwa kufikia uamuzi
wa kupitisha mafuta katika bandari hiyo na kwamba mpaka kufikia Julai 2 hadi 4
mwaka huu Meli yenye shehena ya mafuta takribani tani 20,500 inatarajiwa kutia
nanga kwenye Bandari ya Tanga.
Arika alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza
mapato kwa Bandari na serikali kwa ujumla na kwamba mpaka sasa tayari
mamlaka hiyo imeshapata vifaa vya kisasa ikiwemo baji 3 zenye ukubwa wa tani
3500 zenye uwezo wa kupakua makontena ya futi 20 zaid ya makontena 120 na hivyo
kuongeza ufanisi wa Bandari.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa
TPA Awadh Massawe alisema kuwa aliishukuru serikali kwa kufanya mabadiliko ya
dhati yenye lengo la kuboresha huduma za mamlaka hiyo ikiwa ni pamoja na Bandari
ya Tanga ambayo ni ya pili katika utoaji wa huduma na utendaji kazi bora
nchini.
|