Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, imewataka wachezaji wa Ligi Kuu Bara kuwa
na wanasheria wao wa kusimamia wakati wa kusaini mikataba yao.
Kauli hiyo ya serikali imekuja baada ya kiungo mshambuliaji
Ramadhan Singano ‘Messi’ kuwa katika mgogoro wa kisheria na Klabu ya Simba
kuhusu mkataba wake na timu hiyo.
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia,
ameliambia Championi Jumamosi kuwa, kupitia mgogoro huo ni vizuri wachezaji
wakatumia wanasheria katika kutazama mikataba yao ili kuzuia migogoro inayoweza
kujitokeza siku za mbele.
“Hili sakata la Messi na Simba nalisikia juu juu tu, lakini
ukitazama vizuri utagundua mchezaji hakuwa na msimamizi wa maana katika kusaini
mkataba ule, ndiyo maana sasa wanapingana.
“Hivyo kuanzia sasa wachezaji wanapaswa kuwa na wanasheria wao
binafsi ili wawasimamie katika mambo ya mikataba kwani wengi wanasaini mikataba
bila kujua kilichomo ndani yake,” alisema Nkamia ambaye amewahi kuwa katibu
mwenezi wa Simba.
“Siyo jambo jema kwa mchezaji kukimbilia fedha tu bila kujali
kilichomo katika mkataba na kusaini akiwa haelewi kilichoandikwa au kukisoma na
kukubaliana nacho.”
Katika madai ya msingi, Messi anasisitiza mkataba wake unaisha
Julai Mosi, mwaka huu wakati Simba wanasema mkataba huo unaisha Julai Mosi,
mwakani, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limewataka wawili hao kuketi upya
kuzungumzia mkataba mpya huku likivunja mikataba ya awali kwa kuwa ina dosari.
Messi amejitangaza kuwa mchezaji huru na Simba inasisitiza kuwa kiungo huyo bado ni mali yao na hapaswi kuzungumzia mkataba wake kwenye vyombo ya habari.
EmoticonEmoticon