Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na
wajumbe wa Kamati ya uongozi wa Chama cha Wafugaji Tanzania, wakati
walipomtembelea Ofisini kwake Ikulu Dar es salaam leo Juni 02,2015.
………………………………………………………………….
Na Mwandishi Maalum
Asema :Jitahidini kuepusha migogoro-Dkt. Bilal awaasa wafugaji .
Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amewataka
wafugaji nchini kuhakikisha wanafuata sheria na kuachana na tabia ya
kuchukua sheria mkononi ili kuhakikisha usalama wao na watu wanaopakana
nao unakuwepo wakati wote. Mheshimiwa Makamu wa Rais amezungumza hayo
leo Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kupokea ujumbe kutoka Chama cha
Wafugaji Tanzania ulioongozwa na Mwernyekiti wao Ally Hamis Lumiye.
Makamu wa Rais
alisema, si busara kwa wafugaji kujichukulia sheria mkononi na kwamba
matatizo yanayowakabili wafugaji ni muhimu yakatatuliwa kwa kufuata
sheria za nchi. “Jitahidini kuepusha migogoro hasa ile inayosababisha
watu kupoteza maisha. Tusichukue sheria mkononi, sote lazima tuwe watii
wa sheria,” Makamu wa Rais alisema.
Awali
akizungumza kwa niaba ya Baraza la Wazee wa Chama cha Wafugaji Tanzania,
Mwenyekiti wa Chama hicho Ally Hamis Lumiye alisema, chama cha wafugaji
kwa sasa kinakabiliwa na changamopto kubwa hasa baada ya kuwepo
mgawanyiko unaolenga kukimomonyoa chama hicho hasa kufuatia kujitokeza
baadhi ya wafugaji kuamua kupora madaraka ya chama hicho na hivyo
akaitaka serikali kuungana nao katika kuzima nguvu za waporaji hao.
“Mheshimiwa
Makamu wa Rais leo hii tumekuja kwako kwa jambo moja nyeti. Wapo baadhi
yetu wasiotaka kuona wafugaji tunajikomboa kwa kuwa na umoja kama huu.
Wamefikia hatua ya kupora chama hiki na jitihada zetu za kutaka
kuwadhibiti zinaonekana kuwa ngumu kufuatia baadhi ya viongozi wa
serikali kuwatambua waporaji hao,” alisema mwenyekiti huyo.
Mheshimiwa
Makamu wa Rais alisisitiza kuwa jambo la uporaji wa chama kamwe haliwezi
kuachwa kimya kwa kuwa wafugaji na chama chao kimesajiliwa hivyo
wafuate sheria hizo hizo ili kupata haki yao kama inaonekana kutokuwepo.
Pili alisisitiza kuwa atalifanyia kazi suala hilo kupitia nafasi
ziliozpo chini yake na kulipatia ufuimbuzi wa haraka.
“Mimi nami ni
mfugaji, chama hiki ni muhimu kwa maslahi ya wafugaji. Kwa kuwa tuna
katiba inayokiongoza na kwamba tunazo sheria ambazo zilifuatwa hadi
kukipatia chama hiki usajili, basi hakuna haja ya kusikitika sana.
Tutumie taratibu hizi hizi ili kuondokana na hao wanaotaka kupora
mamlaka ya chama hiki,” alisema na kuongeza:
“Ni muhimu
kiwepo chama imara kwa maslahi ya wafugaji wote. Chama hiki kinaweza
kuwasaidia sana katika kukabiliana na changamoto mlizonazo maana kwa
kuwa wamoja ni nguvu.”