Mahmoud Ahmad,Arusha
…………………………………………
Watuhumiwa 60 wa kesi za ugaidi jijini Arusha wamemuomba
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha Nestory Barro kuchukua uamuzi
mgumu wa kufanyia kazi kwa vitendo makosa yaliyomo kwenye Sheria dhidi
ya tuhuma zinazowakabili.
Madai hayo waliyatoa mwishoni mwa wiki iliyopita wakati
kesi zao zilipokuwa zimepangwa kwa ajili ya kutajwa, ambapo Mwendesha
Mashitaka wa Serikali Augustine Kombe aliziahirisha hadi Mei 8, Mwaka
huu kutokana upelelezi wa polisi kutokamilika.
Akizungumza mahakamani hapo kwa niaba ya wenzake mara baada
ya kunyoosha mkono na kupewa nafasi na Hakimu Barro, mtuhumiwa Jafar
Lema aliyeomba kujulishwa wanapokuwa mahakamani hapo wanakuwa chini ya
mamlaka ipi.
Hatua ya kuuliza swali ilikuja baada ya mtuhumiwa mwenzake
kutaka kujua suala la dhamana dhidi ya mashitaka yanayowakabili ilihali
akidai wapo watuhumiwa wenzao waliopewa dhamana wakiwa polisi na
wanaendelea kuripoti kituoni hadi leo.
Akitoa ufafanuzi kwa mtuhumiwa na wenzake Hakimu alisema,
kosa waliloshitakiwa nalo halina dhamana, kwani hata hao aliodai
walipewa dhamana polisi na kutakiwa kuripoti wanaweza kuwa wana mambo
yao na ndio maana hawapo mahakamani.
“Unajua sheria yetu hii bado ina makosa kwasababu mtuhumiwa
unatakiwa uwe mahabusu wakati kesi yako ikiwa imeanza kusikilizwa na si
wakati wa upelelezi,” alisema Hakimu Mkazi Baro.
Hata hivyo majibu hayo yalimpa fursa mtuhumiwa Lema kuomba
kufahamishwa kwamba wanapokuwa mahakamani hapo wanakuwa chini ya nani,
Polisi au Mahakama, ambapo Hakimu Mkazi Barro alimueleza kuwa ni
Mahakama.
“Mheshimiwa Hakimu, sasa nakuomba usiogope, hakuna mtu
atakayekufunga kwani Taifa litakuona wewe ni shujaa, nakuomba na
wenzangu ufanyie kazi kwa vitendo makosa hayo yaliyopo kwenye
sheria,”alidai mtuhumiwa Lema na kuongeza:
“Nakuomba umwambie Mwendesha Mashitaka wa Serikali Kombe
ayarudishe majalada yote ya kesi hizi hadi hapo upelelezi
utakapokamilika, kama watakusumbua nipo tayari mimi na wewe tushirikiane
kufungua kesi ya Kikatiba,”alidai Lema
Hata hivyo Hakimu Mkazi Barro alilazimika tena kutoa
ufafanuzi kwa mtuhumiwa huyo na wenzake akieleza kwamba alichokuwa
akikisema mtuhumiwa kina ukweli kwamba sheria ina makosa lakini kwa
shauri hilo yeye hana mamlaka yoyote.
“Katika mashitaka haya ya PI aisee sina mamlaka nayo, labda
kama ingekuwa na makosa ya wizi wa kuku na mengine kama hayo huku nina
mamlaka napo, sio katika hili,” alisema Hakimu Mkazi Barro.
Kwa upande wake Mwendesha Mashitaka Kombe akijibu maadhi ya
madai ya watuhumiwa hao aliwashauri kuandika barua kwa Mkurugenzi
Mashitaka nchini (DPP), kuelezea kuhusu kuchelewa kukamilika kwa
upelelezi wa kesi zao.
Watuhumiwa hao wameshitakiwa kwa makosa yaliyo chini ya
Sheria ya kuzuia ugaidi, ambapo Sheria namba 22 ya Mwaka 2002 inasema
upelelezi wa shauri hilo ukishakamilika, Mahakama Kuu ndiyo yenye
mamlaka ya kusikiliza na kutoa uamuzi.
Watuhumiwa hao 60 waliopo katika kesi mbalimbali
wanakabiliwa na mashitaka ya kuua, kujaribu kuua, kusajili na
kusafirisha vijana kujiunga na kikundi cha ugaidi cha Al-Shabaab.
Mbali na mashitaka hayo wanahusishwa na tukio la
milipuko ya mabomu Bar ya Arusha Night Park, mlipuko wa Bomu Viwanja
vya Soweto na mlipuko uliotokea Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi
Olasite jijini Arusha ambapo ilisababisha vifo na majeruhi.
EmoticonEmoticon