Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akiwasili kwenye Hoteli ya Rainbow, jijini Harare, Zimbabwe kwa
ajili ya kuhudhuria Mkutano wa dharura wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa
SDC, uliofunguliwa leo Aprili 29, 2015 na Rais wa Zimbabwe, Robert
Mugabe, Jijini unaojadili kuhusu Uendelezaji wa Viwanda. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal (katikati), akiwa na baadhi ya Viongozi wenzake katika Mkutano wa
dharura wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa SDC, uliofunguliwa leo Aprili
29, 2015 na Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, Jijini Harare, Zimbabwe,
kuhusu Uendelezaji wa Viwanda. Picha na OMR
R
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akifuatilia hotuba ya Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, wakati akifungua
rasmi Mkutano wa dharura wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa SDC,
uliofunguliwa leo Aprili 29, 2015, kuhusu Uendelezaji wa Viwanda. Picha
na OMR
Baadhi
ya Mawaziri wa Tanzania, waliohudhuria mkutano huo wakimsikiliza kwa
makini Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, wakati akisoma hotuba ya
ufunguzi rasmi wa Mkutano wa dharura wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa
SDC, uliofunguliwa leo Aprili 29, 2015, kuhusu Uendelezaji wa Viwanda.
Picha na OMR
………………………………………………………………………………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo Jumatano Aprili 29,
2015, ameiwakilisha Tanzania katika mkutano wa dharura wa Umoja wa Nchi
za Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika jijini Harare, chini ya
Uenyekiti wa Rais Robert Mugabe, Rais wa Zimbabwe, Mwenyekiti wa sasa wa
SADC pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU). Mkutano huo wa siku
moja pia umehudhuriwa na Rais Seretse Ian Khama, Rais wa Botswana na
Makamu Mwenyekiti wa SADC, Mfalme Muswati III wa Swaziland, Rais wa
Msumbiji Filipe Nyusi, Rais wa Namibia Hage Geingob, Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Watu wa Lesotho Pakalitha Mosisili, Rais wa Afrika Kusini
Jacob Zuma na Rais wa Zambia Edgar Lungu.
Awali akifungua mkutano huo Rais
Mugabe alisisitiza umuhimu wa nchi za SADC kuwa na mpango madhubuti wa
Viwanda kwa kuwa uwepo wa viwanda utasaidia kupunguza tatizo kubwa
linalozikabili nchi hizi hasa ajira, pamoja na uchumi duni unaotokana na
ukosefu wa viwanda vya kuboresha bidhaa zinazozalishwa katika nchi za
ukanda huu. Mkakati huu uliopitishwa na Wakuu wa nchi na Serikali wa
nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaanza mwaka huu 2015 hadi mwaka 2063.
Katika mkakati huu nchi za SADC zinalenga kutanua uhuru wa soko katika
utatu wa kanda za Kibiashara yaani SADC, EAC na COMESA ikiwa ni pamoja
na kutenga eneo huru la ukanda wa kiuchumi wa nchi za kanda hizi, huku
lengo likiwa kufanikiwa upatikanaji wa eneo huru la ukanda wa biashara
kwa nchi za Afrika. Masuala mengine ni pamoja na kukuza bidhaa
zinazozalishwa katika nchi hizi katika masoko ya Asia ambao ni walaji na
watumaji wakubwa wa malighafi zinazozalishwa katika nchi hizi.
Rais Mugabe alifafanua pia kuwa,
nchi hizi kwa umoja wake zikiunganishwa utakuta ndizo zina rasimali
kubwa ya madini ya Dhahabu, Almasi na hata Gesi na kwamba kama
mtengamano huu utakamilika nguvu ya pamoja inaweza kugeuza hali ya
maisha ya wananchi wa nchi hizi sambamba na maendeleo ya kiuchumi katika
nchi hizo.
Awali akizungumza kabla ya hotuba
ya ufunguzi ya Rais Mugabe, Katibu Mtendaji wa SADC Dkt. Stargomena
Lawrence Tax aliishukuru serikali ya Zimbabwe kwa maandalizi mazuri ya
mkutano huu ambao ulikuwa ni mwendelezo wa ule uliofanyika Victoria
Falls, Zimbabwe Agosti 17, 2014 mkutano uliotaka nchi wanachama wa SADC
pamoja na kupitisha mkakati wake wa Kimaendeleo, upange dira ya utanuaji
na uendedlezaji viwanda katika ukanda huu.
Matukio mengine katika mkutano huu
ni pamoja na makabidhiano ya Kituo cha Mafunzo ya Utunzaji Amani katika
nchi za SADC, makabidhiano yaliyofanywa na nchi ya Zimbabwe chini ya
Rais wake Robert Mugabe kwa Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt Stargomena Tax.
Kufuatia makabidhiano haya, Chuo hiki sasa kitakuwa kinamilikiwa na
SADC na matumizi yake yatahusisha vyombo na wataalamu mbalimbali
wanaohusika na masuala ya utunzaji amani ndani ya nchi hizi, ili kupata
mafunzo ya kuboresha kazi zao kufuatia migogoro kuwa mingi katika nchi
mbalimbali Afrika.
Pia Rais Mugabe alitumia muda huo
kuutaka Mkutano huu wa Dharura kutoa heshima zao kufuatia kifo cha
Brigedia Jenerali Hashim Mbita aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Kamati ya
Ukombozi kwa kutambua mchango wake katika uhuru wa nchi zilizomo SADC na
pia mchango wake kwa ajili ya maendeleo ya nchi hizi. Raia Mugabe
alimtaja Hayati Brigedia Mbita kama mpiganaji mahiri na kiongozi
aliyefanya kazi kwa maslahi ya watu wengi bila kuchoka na kwamba Afrika
na SADC vitamkumbuka daima kwa mchango wake huo.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Harare, Zimbabwe
Aprili 29, 2015
EmoticonEmoticon