SERIKALI
imesema itajitahidi kuhakikisha inalipa deni lote la mahindi
yaliyonunuliwa kutoka kwa wakulima na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA) ifikapo Machi 30, mwaka huu.
Akizungumza na maelfu ya wananchi
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana (Jumapili, Machi 2, 2015)
kwenye uwanja wa CCM wa Vwawa wilayani Mbozi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda
alisema Serikali imedhamiria kufuta deni lote.
“Hapa Mbozi tulikuwa tunadaiwa sh.
bilioni 21 lakini tumetoa sh. bilioni 4.5 kwa hiyo tutabakia na deni la
kama sh. bilioni 16 ambalo tunajitahidi liwe limeisha ifikapo mwishoni
mwa mwezi huu,” alisema.
“Tunachoweza kuahidi kama Serikali
ni kwamba, msimu huu hatutarudia kosa la mwaka jana ingawa mtihani
mkubwa tulionao ni wa kushughulika na hifadhi ya chakula kwa kujenga
vihenge (SILOS) ili hata kama kuna ziada n tusipate taabu ya kuhifadhi,”
aliongeza.
Alisema alishakwenda Poland kwa
maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete na wao wameshakuja kuona hali halisi
ilivyo. “Tumependekeza vihenge vijengwe kwenye kanda za Mbeya, Rukwa,
Dodoma, Dar es Salaam, Arusha au Kilimanjaro na Shinyanga ili iweze
kuhudumia kanda ya Ziwa,” alisema.
Wakati huo huo, Mbunge wa Mbozi
ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Godfrey
Zambi amesema Serikali imekwishalipa zaidi ya sh. bilioni 81 na kwamba
deni lililosalia linafikia sh. bilioni 59.
“Hadi mwishoni mwa mwaka jana,
tulikuwa tumeshalipa sh. bilioni 51.5/- na mwaka huu tumepata sh.
bilioni 15 kutoka CRDB na hivi majuzi kuna bilioni nyingine 15 zimetoka
Hazina… Agizo la Serikali ni kwamba mahindi yote yawe yamelipwa ifikapo
Machi 30, naamini tutakamilisha,” alifafanua.
Alielezea pia tatizo la maji
linaloukabili mji wa Mbozi na vitongoji vyake na kueleza kwamba Serikali
inashughulikia tatizo hilo katika programu mbalimbali.
Mapema, akiwa katika ghala la
nafaka la NFRA katika makao makuu ya wilaya ya Mbozi, Vwawa, Waziri Mkuu
alielezwa kwamba kanda ya Makambako ambayo inajumuisha vituo vya
Makambako na Vwawa imezidiwa uwezo na sasa wanalazimika kuhifadhi
magunia ya mahindi nje kwa vile maghala yamejaa.
Meneja wa Kanda hiyo wa NFRA, Bw.
Abdillah Nyangasa alisema kanda hiyo ina uwezo wa kuhifadhi tani za
nafaka 34,000 ambapo kati ya hizo, tani 22,000 ni maghala ya Makambako
na tani 12,000 ni maghala ya Vwawa, Mbozi.
Hata hivyo, Bw. Nyangasa alisema
kanda hiyo kwa sasa kina tani za mahindi 79,496.8 zikijumuisha tani
15,738.9 za msimu uliopita licha ya tani 63,757.8 ambazo zimenunuliwa
katika msimu huu
“Ili kukabiliana na uhaba wa
maghala, kanda yetu hulazimika kufanya hifadhi ya nje (outside storage)
kwa kutumia maturubai (tarpaulins) ili mahindi yasiharibiwe na hali ya
hewa kama mvua au jua kali,” alisema Bw. Nyangasa.
Waziri Mkuu anamaliza ziara yake ya siku saba mkoani Mbeya leo kwa kufanya majumuisho na kisha kurejea jijini Dar es Salaam.
EmoticonEmoticon