Mkuu
wa Mkoa wa Tanga Mhe. Magalula S. Magalula akizungumza na Waandishi wa Habari Leo Ofisini kwake
Kaimu
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bw. Ramadhani Kaswa
(Kushoto ) na baadhi ya Waandishi wakati wa mkutano
Baadhi
ya Waandishi wa Habari wakati wa mkutano
Taarifa zaidi
Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Tanga kwa niaba ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Muungano wa
Utepe Mweupe wa Uzazi Salama Tanzania inapenda kuwatangazia Wananchi kuwa Mkoa wa Tanga unatarajia kuwa mwenyeji
wa maadhimisho ya Siku ya Utepe Mweupe
Kitaifa itakayofanyika Machi 15,
Mwaka huu.
Siku ya Utepe
Mweupe ni mwendelezo wa juhudi za Serikali katika kupunguza na kutokomeza kabisa vifo vya akina mama na
watoto wachanga.Maadhimisho haya ambayo hufanyika Machi 15 kila mwaka yana lengo la kuwakumbuka
na kuwaenzi wanawake waliopoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi.
Siku hii pia
hutumika kujadili mikakati ya kuzuia vifo vingine visitokee. Kauli mbiu ya
mwaka huu ni “WAJIBIKA MAMA NA MTOTO MCHANGA
AISHI”. Kauli mbiu hii inalenga
kuhamasisha uwajibikaji wa kila mmoja wetu kuanzia mama mjamzito nwenyewe na
familia yake, jamii na uongozi katika
kuhakikisha kuwa hakuna mama wala mtoto mchanga anayepoteza maisha kutokana na
sababau ambazo zingeweza kuzuilika.
Aidha, kutakuwepo
na shughuli mbalimbali ambazo zitaambatana na maadhimisho haya katika wiki ya
kuelekea siku yenyewe ambazo ni pamoja na uchangiaji damu salama, kushiriki
katika zoezi la sauti ya jamii,kushiriki katika matembezi ya mshikamano na
mkutano siku ya kilele.
Asilimia
75 ya vifo vingi nchini vinatokana na kutoka damu kwa wingi, maambukizi,
shinikizo la damu na utoaji mimba. Wanawake
24 wanafariki kila siku na wengine hupata ulemavu wa kudumu.
Serikali kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuweka mikakati madhubuti ili
kupunguza vifo vya mama na mtoto. Kwanza imeelekeza nguvu zake katika kutoa elimu
ya uzazi salama na pia imeelekeza Halmashauri zote Mkoani kuwa na kipengele
mahususi cha bajeti kinacholenga kuhakikisha kuwa huduma za dharura za uzazi
zinapatikana karibu na akina mama na watoto.
Kutokana na juhudi
za serikali na wadau mbalimbali, matunda yameshaanza kuonekana miongoni mwetu.
Kwa mfano katika Mkoa wa Tanga vifo vya mama na mtoto vimepungua kutoka idadi
ya akina mama 101 kati ya wakina
mama 45,256 waliojifungua kwa mwaka 2013 hadi kufikia idadi ya akinamama 69 kati ya wakina mama 47,692 waliojifungua kwa mwaka 2014 na idadi ya watoto 429 kati
ya watoto 44,852 waliozaliwa kwa
mwaka 2013. Serikali inaendelea na mapambano kuhakikisha
afya ya mama na mtoto iko salama.
Kupunguza vifo vya
mama na mtoto vinavyotokana na matatizo wakati wa kujifungua ni moja ya malengo 8 ya Milenia. Hili ni lengo namba tano ambalo linalenga kupunguza
vifo vya akina mama vinavyoyokana na matatizo wakati wa kujifungua kwa asilimia
sabini na tano (75%) ifikapo mwaka 2015.
Nawashukuru na
kuwapongeza wenzetu wa Utepe Mweupe na wadau wengine kwa kujikita katika
kampeni ya uhamasishaji ili kupunguza na kutokomeza vifo vya mama na mtoto.
Napenda kutoa wito
kwa wananchi kuhakikisha kuwa kila mmoja anatekeleza wajibu wake ili kuokoa
maisha ya mama na mtoto. Pia naviomba vyombo vya habari kuungana na makundi
mengine katika jamii kuwa sauti ya akina mama ili kupunguza vifo vya mama na
mtoto.
Kwa pamoja tunaweza
kuzuia vifo vya mama na watoto wachanga
“Wajibika
Mama na Mtoto Mchanga Waishi”