Na Anna Nkinda – Maelezo, Masasi
…………………………………
Jamii imehimizwa kuhamasisha
kinamama wajawazito kujifungua katika vituo vya afya ambako watasaidiwa
na wakunga wenye ujuzi kwa kufanya hivyo vifo vya kinamama na watoto
wachanga vinavyotokana na tatizo la uzazi vitapungua.
Mwito huo umetolewa jana na Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wananchi waliohudhuria hafla
ya makabidhiano ya gari la wagonjwa la Hospitali ya mji wa Masasi
ilijulikanayo kwa jina la Mkomaindo iliyofanyika katika viwanja vya
ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo.
Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti
wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema mtoto wa kike akibeba
mimba katika umri mdogo, mama mjamzito asipohudhuria kliniki mapema
na kwa muda uliopangwa na kutojifungua katika vituo vya afya mama
anaweza kupata matatizo ikiwa ni pamoja na kupotea maisha wakati wa
kujifungua.
“Wanaume mnapaswa kuunga mkono
juhudi hizi katika kipindi cha ujauzito kina mama waondolewe majukumu ya
kazi nzito muwe nao karibu, wahurumieni na kujiepusha na aina yoyote ya
unyanyasaji. Wawezesheni wake zenu kuhudhuria kliniki na kupima
ujauzito kipindi chote cha ujauzito na ifikapo tarehe ya kujifungua
wasindikize katika vituo vya afya.
“Pale watakapogundulika kuwa na
matatizo ya kujifungua wapeni ushirikiano wa kutosha ikiwemo rasilimali
fedha kwa ajili ya huduma yoyote ya rufaa itakayohitajika”, Mama Kikwete
alihimiza.
Kwa upande wa vifo vya watoto
alisema hutokana na kutokuwa na uwezo kama vile fedha za kumpeleka mama
mjamzito aliyeshindwa kujifungua, kumuwahisha mtoto Hospitali mara
apatapo matatizo kama vile ya kupumua, homa, na kuharisha.
Mama Kikwete alisema , “Huduma ya
gari la dharula la wagonjwa ni muhimu sana katika kuokoa maisha ya watu.
Taarifa za kila siku zinaonyesha ni jinsi gani kina mama wajawazito
wanapoteza maisha kutokana na kucheleweshwa kufika katika vituo vya
afya”.
Aidha Mwenyekiti huyo wa WAMA
aliupongeza uongozi wa wilaya hiyo na watumishi wa sekta ya afya kwa
kupunguza kasi ya maambukizi ya VVU kutoka asilimia 5.07 hadi kufikia
2.13 kwa mwaka 2014 ukilinganisha na mwaka 2013 ambapo kasi ya
maambukizi ilikuwa asilimia 7.13.
Akisoma taarifa ya Idara ya afya
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya mji wa Masasi Dkt. Albano Nditi
alisema katika mji huo kuna vituo nane vinavyotoa huduma ya afya ya
uzazi na mtoto ambazo ni upimaji wa kina mama wajawazito na watoto,
kuzalisha na ufuatiliaji wa makuzi ya watoto.
Dkt. Nditi alisema idadi ya
wasichana wanaobeba mimba wakiwa na umri wa chini ya miaka 20 ni kubwa
hali hiyo inatokana na uelewa mdogo wa jamii juu ya athari za kubeba
mimba katika umri mdogo. Pia asilimia 55 ya wanawake wajawazito
wanaoanza kliniki hawakamilishi mahudhurio yote manne kwani waliowengi
huanza kliniki wakiwa wamechelewa.
Alifafanua, “Kwa mwaka 2014 kina
mama waliojifungua katika vituo vya kutolea huduma ni ni 4,762 kati
ya hao wenye umri wa chini ya miaka 20 ni 1541 na zaidi ya miaka 20 ni
3,221. Waliojifungulia majumbani na kwa wakunga wa jadi ni 278 kati ya
hao wenye umri wa chini ya miaka 20 ni 68 na zaidi ya miaka 20 ni 210”.
Vifo vilivyotokana na uzazi kwa
mwaka jana vilikuwa 22, tatizo la vifo vya uzazi bado ni kubwa hii
inatokana ana uhaba wa watumishi wenye ujuzi, mahudhurio duni ya kina
mama Kliniki, kuchelewa kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya
wakati wa kujifungua na uhaba wa vifaa kwenye wodi ya wazazi”.
Alizitaja changamoto
zinazowakabili kuwa ni upungufu wa madaktari, wauguzi wenye ujuzi,
maafisa afya mazingira na madereva, upungufu wa magari ya kubebea
wagonjwa, upungufu na uchakavu wa majengo, uhaba wa vitanda na mashuka
katika wodi za wagonjwa na ukosefu wa vituo vya kutolea huduma za afya
katika baadhi ya maeneo hasa yaliyo pembezoni mwa mji.
Kuhusu Mfuko wa Afya ya Jamii
(CHF) Dkt. Nditi alisema jumla ya kaya 274 kati ya 28,875 zilizopo
katika mji huo zimejiunga na mfuko hali hiyo inatokana na mwitikio na
uelewa mdogo kutoka kwa wananchi juu ya kujiunga na huduma hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya
mji wa Masasi Andrew Mtumusha alimshukuru Mama Kikwete kwa msaada wa
gari alilowapatia na kusema kuwa litaokoa vifo vingi vya wakinamama
wajawazito, watoto na wanaume ambavyo vinatokea pale ambapo mgonjwa
anacheleweshwa kufikishwa Hospitali kubwa kutokana na tatizo la
usafiri.
“Ninakupongeza kwa moyo wa huruma
na upendo ulionao, nakuomba uendelee kutukumbuka zaidi na zaidi kwenye
mambo mbalimbali. Nina kuahidi gari hili litatumika kwa matumizi
yaliyokusudiwa ya usafirishaji wagonjwa bila upendeleo wowote”, Mtumusha
alishukuru.
Taasisi ya WAMA iliamua kukabidhi
gari hilo liliopatikana kwa kushirikiana na Shirika la Sayeed
Corporation katika Hospitali ya Mkomaindo kutokana na wakina mama wengi
kuhitaji huduma ya usafiri ili waweze kufika Hospitali kwa wakati na
uwepo wa huduma ya mama na mtoto ambayo inatolewa mahali hapo.
EmoticonEmoticon