Balozi
wa Uholanzi Nchini Tanzania Mr. Jaap Frederiks akizungumza na baadhi ya
watendaji wakuu wa Wizara ya Afya kabla ya utiaji saini makubaliano ya
uboreshwaji wa wodi ya wazazi na watoto Unguja na Pemba, hafla hiyo
imefanyika Wizara ya Afya Zanzibar.
Katibu
Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Saleh M. Jidawi (wa kulia waliokaa)
na Meneja wa Kampuni ya Simed International Services ya Uholanzi Nd.
Michor Pleijzer wakitia saini mkataba wa uboreshwaji wa wodi ya wazazi
na watoto Unguja na Pemba huku wakishuhudiwa na Waziri wa Afya Rashid
Seif Suleiman na Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania Mr. Jaap Frederiks
katika hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mjini Zanzibar. (Picha na
Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar).
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Saleh M. Jidawi (kulia)na
Meneja wa Kampuni ya Simed International Services ya Uholanzi Nd. Michor
Pleijzer wakibadilishana hati za makubaliano ya uboreshwaji wodi ya
wazazi na watoto za Unguja na Pemba katika hafla iliyofanyika Wizara ya
Afya Mjini Zanzibar.
Balozi
wa Uholanzi Nchini Tanzania Mr. Jaap Frederiks (wakatikati mbele walio
simama)katika picha ya pamoja ya viongozi wa Wizara ya Afya ya Zanzibar
wakiongozwa na Waziri wa Afya Rashid Seif Suleiman wa mbele kulia.
Sherehe hiyo ilifanyika Wizara ya Afya Mjini Zanzibar
(Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar).
……………………………………………………………………………..
Na Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuokoa maisha ya Wanawake na Watoto kwa kuimarisha Miundombinu ya Afya.
Hayo ameyaeleza Katibu Mkuu wa
Wizara ya Afya Dr. Saleh M. Jidawi wakati akisaini Mkataba kwa ajili ya
utekelezaji wa kuanza kwa mradi wa kuimarisha Afya za Mama na Watoto
uliyofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo iliyopo Wilaya ya Mjini
Unguja.
Mkataba huo uliosainiwa na Wizara
ya Afya Zanzibar kupitia Katibu Mkuu Dr. Saleh M. Jidawi kwa pamoja na
Meneja wa Kampuni ya Simed International ya Uholanzi Nd. Michor
Pleijzier uliofanyika siku ya tarehe 11/02/2015 ni miongoni mwa
muendelezo wa utekelezaji wa mradi huo ambao awali ulitiwa saini mnamo
tarehe 23/12/2014.
Dr. jidawi amesema kuwa dhamira
kuu ya mradi huo ni kuimarisha afya za kina mama na watoto waliozaliwa
chini ya mwaka mmoja pamoja na kutoa huduma kwa watoto wengine.
Ametanabahisha kuwa utekelezaji wa
mradi huo unakwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya
2020 uliotafsiriwa na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini
Zanzibar (MKUZA ii).
Amesema kuwa mradi huo unajumuisha
maeneo mbalimbali ya utekelezaji ikiwemo upatikanaji wa vifaa, tiba,
ukarabati wa vifaa, uboreshaji wa miundombinu pamoja na utoaji wa
ushauri elekezi kwa Hospitali ya Mnazi Mmoja.
Amesema sambamba na hayo mradi huo
unakusudia kuviboresha vituo vya Afya 19 vya Unguja na Pemba ili vipate
kutoa huduma bora kwa jamii.
Ametanabahisha kuwa kwa upande wa
Hospitali ya Mnazi Mmoja mradi huo utajumuisha vitengo mbalimbali
vikiwemo chumba cha upasuaji, maabara, duka la dawa, chumba cha wagonjwa
mahututi cha watoto na wazazi, kitengo cha huduma za X-ray, wodi za
wazazi, kitengo cha kutakasisha vifaa tiba, eneo maalumu la kuteketeza
taka za hospitali pamoja na kitengo cha wagonjwa wa nje (OPD).
Dr. Jidawi ameeleza kuwa mradi huo
wa sekta ya Afya unaakisi maazimio ya Serikali zote mbili ambazo ni
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Uholanzi kwa kufanya
kazi pamoja katika nyanja mbalimabali za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na
uchimabaji wa gesi, uhifadhi wa mwambao wa bahari, uendelezaji wa
bandari pamoja na uhifadhi wa Mji Mkongwe.
Nae Balozi mdogo wa Uholanzi Nd.
Jaap Frederiks ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
kuharakisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya mradi huo na kazi
iliyobakia ni kuanza rasmi kwa maazimio ya mradi huo ambao utachukua
takriban Miezi 33 hadi kukamilika kwake.
Mradi huo utagharimu shilingi
Bilioni 19.5 Tsh, ambapo asilimia 50% ya fedha hizo zimetolewa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na 50% zilizobaki zimetolewa na
Serikali ya Uholanzi, zaidi ya gharama hizo pia Serikali ya Uholanzi
imetoa fedha kwa ajili ya uandaaji wa michoro pamoja na ushauri elekezi
uliogharimu shilingi Milioni 720
EmoticonEmoticon