Meli Kubwa yenye Urefu wa Mita 244 yatia nanga Bandari ya Dar

February 11, 2015

unnamed 
Meli kubwa MSC Martina yenye urefu wa mita 244 na upana wa mita 32.2 ikiwa na uwezo wa kubeba makontena 2,411 imefanikiwa kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka, Mhandisi Madeni Kipande amesema, mafanikio hayo ni juhudi zilizofanywa na Mamlaka kuzitangaza bandari zake pamoja na uboreshwaji wa huduma.
“Ujio huu wa meli kubwa za mizigo kama hizi ni faraja kubwa sana kwetu kwani pia utaongeza uingiaji wa mizigo kwa wingi na hatimaye kuleta unafuu kwa mtumiaji wa mwisho,” alisema Mhandisi Kipande.
MSC Martina Kampuni ya Mediterranean Shipping Company (MSC) ni miongoni mwa meli kubwa na za kisasa ambazo zimefanikiwa kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam na kupakia na kupakua mzigo.
Meli nyingine kubwa na ya kisasa kuja nchini kwa mara ya kwanza ilikuwa ni Maersk Cubango mali ya Maersk Line iliyokuwa na urefu wa mita 250 na upana wa mita 38 ikiwa na uwezo wa kubeba kontena 4,500.
Mhandishi Kipande ameomba ushirikiano uliopo kati ya Mamlaka na mawakala wa meli uendelee ili kuleta ufanisi zaidi na amewataka mawakala wengine kuleta meli kubwa kama walivyofanya, Maersk and Mediterranean.
Kwa upande wake Nahodha aliyeingiza meli hiyo ndani ya Bandari ya Dar es Salaam, Abdulah Mwingamno alisema mabadiliko ya teknolojia yameongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia meli kubwa zaidi.
“Tuliweza kuingiza meli yenye urefu wa mita 250 ya kampuni ya Maersk iitwayo Maersk Cubango na sasa tumeingiza meli nyingine kubwa ya kampuni ya MSC iiitwayo MSC Martina yenye urefu wa mita 244, haya ni mafakio makubwa kwetu,” alisema.
Nahodha Mwingamno aliongeza kwamba meli hiyo ya mizigo iliingia salama katika lango la Bandari ya Dar es Salaam bila tatizo lolote kama ziingiavyo meli nyingine.
Alisema kwamba ujio wa meli hiyo na kufanikiwa kutia nanga katika bandari yetu bila tatizo lolote ndio kumefungua milango kwa meli hiyo na nyingine za aina hiyo kuanza safari zake kuja Dar es Salaam.
“Tunatarajia ujio wa meli kubwa zaidi ya hii yenye urefu wa mita zipatazo 260 katika bandari yetu kwenye miezi ya Machi na Aprili mwaka huu,” alisema.
Naye mwakilishi wa kampuni ya meli hiyo ya MSC nchini, Ndugu Ahmed Kamal alisema kwamba wanatarajia kuleta meli kubwa zaidi nchini, kwani kampuni yao ina meli kubwa zaidi zinazotia nanga katika bandari nyingine Duniani.
“Hii ni meli kubwa ya kwanza ya kampuni yetu kuja nchini lakini lengo letu ni kuleta meli kubwa zaidi ya hii nchini,” amesema Kamal.
Meli nyingine kubwa zaidi zilizowahi kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam zilikuwa na urefu wa mita 220 na mita 234, zikiwa na uwezo wa kubeba makontena kati ya 2800 na 3000. Awali meli zilizokuwa zinaruhusiwa kuingia katika bandari ya Dar es Salaam hazikutakiwa kuzidi urefu wa mita 234.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »