MAMA SALMA KIKWETE AWATAKA WAKAZI WA MKOA WA LINDI KUJITOKEZA KWA WINGI KUJIANDIKISHA KATIKA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

February 11, 2015

Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi

Wakazi wa mkoa wa Lindi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kushiriki kwenye zoezi la kuipigia kura Katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Mwito huo umetolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika tawi la Msinjahili wilayani humo.

Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema zoezi la uandikishaji litafanyika kwa muda wa wiki moja na katika mkoa huo litaanza tarehe 16 hadi 22 mwezi huu  hivyo basi ni muhimu wananchi wakajitokeza kwa wingi kutumia haki yao ya msingi ya kujiandikisha.

“Mkoa wetu ni mmoja kati ya mikoa minne ya mwanzo itakayoanza zoezi hili, mikoa mingine ni Mtwara, Ruvuma na Njombe. Ni muhimu wananchi mkajitokeza kwa wingi kujiandikisha kwani uandikishaji utafanyika kwa njia ya mashine na baada ya wiki moja mashine hizi  zitahamia katika mkoa mwingine”, alisema Mama Kikwete.

Kuhusu Katiba inayopendekezwa alisema ni ya watanzania wote kwa maendeleo yao kwa kuwa inamgusa kila mtu. Ili wananchi waweze kuipigia kura ni muhimu wakajiandikishe katika daftari la kudumu la wapiga kura na ifikapo tarehe 30 ya mwezi wa nne mwaka huu wakaipigie kura ya Ndiyo. 

Aidha MNEC huyo alisema Tanzania yenye neema inawezekana kwani maisha bora ni kuhakikisha binadamu anafunguka kiakili kwa kupata elimu kwa kuona umuhimu wa hayo yote Serikali imejenga shule nyingi za Sekondari za Kata ambazo zimeweza kuwasaidia watoto wengi kutoka  familia maskini kupata elimu jambo ambalo halikuwepo katika miaka ya nyuma.

Mama Kikwete anasema, “Hivi sasa huduma za afya zimeboreshwa na zinapatikana kirahisi ukilinganisha na miaka ya nyumba kwani Serikali imejenga Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali, idadi ya wafanyakazi katika sekta hii imeongezeka na vifaa tiba pamoja na madawa vinapatikana.

“Barabara zimejengwa kwa kiwango cha lami katika maeneo mengi nchini na hivyo kurahisisha usafiri, wananchi wanasafirisha bidhaa zao kutoa eneo moja hadi lingine haya ndiyo maendeleo kwani mkulima analima mazao yake na kuwa na uhakika wa kuyafikisha sokoni kwa mnunuzi na walaji”,.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Lindi Mzee Alli Mtopa aliwasihi wanachama wa Chama hicho  kuondoa tofauti zao za makundi ya wagombea waliyokuwa nayo katika uchaguzi uliopita bali  waungane na kuwa kitu kimoja  na kufanya kazi za chama kwa kufanya hivyo watapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi ujao.

Mzee Mtopa alisema vyama vya upinzani vinaona maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya CCM lakini havitaki kukubali ukweli bali wanapita mitaani na kuwarubuni watu kuwa hakuna maendeleo yoyote yaliyofanyika jambo ambalo siyo sahihi na kuwataka wananchi hao kuwapuuza na kuendelea kufanya  kazi ili wajiletee maendeleo.

Mama Kikwete pia alifanya vikao na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho  katika matawi ya Sheikh Badi, Msonobari na Msinjahili  alizungumza nao  mambo mbalimbali yanayohusu kazi za chama hicho na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.

Akiwa katika tawi la Msonobari alikipatia kikundi cha utengenezaji batiki cha wanawake wa mtaa wa Msonobari juu na chini shilingi laki tano ili ziweze kuwasaidia kununua vitendea kazi na malighafi kwa ajili ya uzalishaji wa batiki.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »