Baada ya kustaafu kutoka soka la kimataifa aliposhinda Kombe la Dunia
nchini Brazil, Philipp Lahm ametangaza kuwa anapanga kuzitundika njumu
zake kabisa mwaka wa 2018, na kuiambia kwaheri klabu yake ya Bayern
Lahm, akizungumza na gazeti la michezo la Ufaransa, L'equipe, amesema
wakati huo atakuwa na umri wa miaka 34, na anahisi huo ndio wakati mzuri
wa kustaafu kabisa kutoka kandanda.
Septemba 2014, Lahm aliliambia gazeti la michezo la Ujerumani “Sport
Bild” kuwa alikuwa na uhakika angeweza kucheza kwa miaka mingine minne
katika kiwango cha juu, na katika Bayern Munich kwa sababu ni klabu
yake.
Licha ya kuwepo na mtindo wa wachezaji wenye umri mkubwa kuhamia Qatar
au Marekani, Lahm anasema anataka kustaafu akiwa kileleni kama tu
alivyofanya katika rangi za timu ya taifa ya Ujerumani.
Huku akiwa amesalia na miaka mitatu kwenye mkataba wake, nahodha huyo wa
timu ya Ujerumani iliyonyanua Kombe la Dunia 2014 angali na ndoto kubwa
katika klabu ya Bayern, ambayo ni kunyakua Kombe jingine la Ligi ya
Mabingwa Ulaya – UEFA Champions League baada ya lile walilotwaa mwaka wa
2013.
Japokuwa Laham hatakuwa uwanjani kucheza akiwa na umri wa miaka 34, beki
huyo amesema ni “bayana” kuwa atasalia katika mchezo huo kwa sababu
“kandanda ni kitu anachokipenda”.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu
Mhariri: Yusuf Saumu