NA MWANDISHI WETU,TANGA.
JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limejiwekea mikakati
kabamba ya kukabiliana na uhalifu kwa mwaka huu kwa kuishirikisha jamii kwa
kutumia viongozi wa serikali za mitaa na vijiji kusimamia mpango wa ulinzi
shirikishi kwa kutoa taarifa na kuhuisha vikundi vya ulinzi shirikishi.
Kauli hiyo ilitolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Tanga, Fresser Kashai wakati akizungumza na MTANDAO HUU ambapo alisema jambo
jingine ni kuhamasisha matumizi ya daftari la makazi ili kubaini wageni
wanaoingia na kuweza kuwafuatilia nyendo zao.
Alisema kuwa kitu kingine ni kuimarisha usalama
kwenye maeneo ambayo yameonekana kuwa na tatizo kubwa la kiuhalifu kwa
kuimarisha doria na misako ya mara kwa mara kwa kushtukiza ili kuweza kuwabaini
wahusika na kuchukuliwa hatua.
Kamanda huyo alisema licha ya hayo watahakikisha
wanawapima madereva wanaoendesha magari yanayosafiri kwenda nje ya mkoa wa
Tanga ikiwemo kuwapima vilevi kila wanapotoka stendi kuu ya mabasi iliyopo
mkoani hapa kwenda mikoa mingine
Aidha alieleza kuwa watatumia pia wakaguzi wa Tarafa
na mfumo wa polisi kata kwa ujumla kama vyanzo muhimu vya taarifa zinazoonyesha
dalili za awai za kuwepo kwa uhalifu au mgogoro wa makundi fulani ya jamii na
kuyashughulikia mapema kwa kushirikiana na wadau wengine.
Hata hiyo alisema kuwa ndani ya mwaka huu watatoa
elimu kwa pande zilizo katika migogoro juu ya hatua za kisheria zifaazo
kuchukuliwa ili kufikia ufumbuzi wa kudumu wa migogoro husika kwa kupitia
askari kata ikiwemo kuendelea kufuatilia hatua za utatuzi wa migogoro hiyo
katika vyombo husika ili kuendelea
kushauri kitu gani cha kufanya kama rufaa badala ya kuchukua sheria mkononi.
EmoticonEmoticon