Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia Taifa katika Salamu zake za Mwaka mpya wa 2015 kwa Watanzania. |
Elimu
Jambo jipya sana na la kihistoria katika Sera mpya ya Elimu ni dhamira ya Serikali ya kuondoa ada katika elimu
ya sekondari kuanzia mwaka 2016. Mpaka sasa hatuna ada kwenye shule za
msingi, sasa wakati umefika kufanya hivyo pia kwa elimu ya sekondari.
Ujenzi wa Maabara
Ujenzi wa maabara za
Fizikia, Kemia na Baiolojia katika shule za sekondari za Kata 3,463
umekwenda vizuri kiasi. Kwa idadi hiyo ya shule inatakiwa zijengwe
maabara 10,389 ilipofika Novemba, 2014. Hadi kufikia Desemba 29, 2014,
maabara 4,207 sawa na asilimia 40.5 zilikuwa zimekamilika, maabara 5,688
sawa na asilimia 54.8 zilikuwa katika hatua mbalimbali za
ukamilishwaji, na maabara 494 sawa na asilimia 4. zilikuwa katika hatua
za awali za ujenzi.
Umeme
Hivi sasa wananchi
milioni 17.3 nchi nzima sawa asilimia 36 wamefikiwa na huduma ya umeme
ikilinganishwa na watu milioni 8.1 sawa na asilimia 18.4 waliokuwa
wamefikiwa na huduma hiyo mwaka 2012. Mwaka 2015 tunatarajia watu
milioni 18.2 sawa na asilimia 38 watafikiwa na umeme.
Chakula
Mwaka 2014 ulikuwa mzuri
sana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini. Uzalishaji ulikuwa tani
milioni 16.02 ukilinganisha na uzalishaji wa tani milioni 14.38 mwaka wa
jana 2013. Hili ni ongezeko la tani milioni 1.64. Kwa mujibu wa
mahitaji yetu ya chakula nchini kuna ziada ya tani milioni 3.25.
Mfumuko wa Bei
Mfumuko wa bei uliendelea
kushuka na kufikia asilimia 5.8 Novemba, 2014 ukilinganisha na Januari
2014 ulipokuwa asilimia 6.0. Ni matumaini yangu kuwa mfumuko wa bei
utaendelea kushuka na kufikia asilimia 5 ifikapo Juni, 2015.
Ujangili
Kwa ujumla kasi ya
ujangili imeendelea kupungua. Katika mwaka 2014 ndovu 114 waliuawa
ikilinganishwa na ndovu 219 waliouawa mwaka 2013 au ndovu 473 mwaka
2012. Aidha, majangili 1,354 wamekamatwa na pembe za ndovu 542 na silaha
mbalimbali 184 nazo zilikamatwa.
Dawa za Kulevya
Mwaka huu watuhumiwa 935
wakiwemo vigogo wa biashara hii haramu duniani wamekamatwa. Jumla ya
kesi 19 zimefunguliwa Mahakamani. Aidha, kiasi cha kilo 400 za heroine,
kilo 45 za cocaine na kilo 81,318 za bangi zimekamatwa.
Mapato ya Serikali
Makusanyo ya mapato ya
Serikali kwa mwezi, kati ya Julai hadi Novemba, 2014 yaliongezeka kutoka
shilingi bilioni 3,555.5 kipindi kama hicho mwaka 2013 hadi shilingi
bilioni 3,924.1 mwaka huu. Hata hivyo, makusanyo hayo yalikuwa asilimia
90 ya lengo tulilojiwekea la kukusanya shilingi bilioni 4,459.7.
EmoticonEmoticon